Tuesday, 16 September 2008

Kigoma.Mwaka 1976.Nyumba kadhaa maeneo na NHC Mnarani zinaonekana zikiwa na magamba (outer cases) ya betri yaliyobandikwa vikaratasi vyenye maandishi ya Kiarabu.Habari zilizozagaa wakati huo ni kwamba pasipo kuweka "kinga" hiyo maafa yangeikumba nyumba husika.Weka usalimike,usiweke uone kitachokutokea.Kwa vile takriban kila nyumba katika mtaa naoukumbuka ilikuwa na "kinga" hizo,haikuwa rahisi kubaini nini kingetokea kwa waliopuuza.

Ifakara.Mwaka 1982.Watoto tunaangaliwa kwa karibu na wazazi kwa hofu ya kuchukuliwa na "wanyonya damu" au maarufu kwa jina la mumiani.Nakumbuka nyumba moja iliyokuwa eneo la Kwa Shungu ambayo nadhani mmiliki wake aliamua tu kuiwekea urembo wa msalaba kwa kutumia chokaa ilikuwa ikituhumiwa kwamba ndio kituo cha kukusanyia damu zinazonyonywa na mumiani.Hadi leo sijui kama kuna mtoto au mtu aliyenyonywa damu na mumiani waliodaiwa kuvamia Ifakara.

Tanga.Mwaka 1993.Madereva wanataharishana kuhusu jini la kike linalodaiwa kuonekana nyakati za usiku katika barabara ya Ngamiani.Jini hili linadaiwa kujibadili kama mwanamke mrembo sana,na  pindi dereva akithubutu kutoa lifti akidhani "ameopoa mzigo" basi ndio mwisho wake.Pia nyumba moja maeneo ya Makorora ambayo mmiliki wake amefuga mbuzi kadhaa inadaiwa kuhifadhi majini lukuki.Wajuzi wa mambo wanatahadharisha kupita maeneo hayo usiku mkubwa,na wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kushauri kwamba hata ukipita mchana usiangalie sana nyumba hiyo,majini yanaweza kukuvuta.Hadi naondoka Tanga mwaka 1995 sikuweza kuthibitisha ukweli au uongo wa habari hizo.

Nyanda za Juu Kusini.Miaka ya hivi karibuni.Taarifa zinatapakaa kwamba kuna biashara ya uchunaji ngozi za binadamu.Inadaiwa kwamba ngozi hizo hutumiwa na waganga kwenye masuala ya baishara.Pia inadaiwa kuwa ngozi hizo zina faida kubwa katika nchi moja jirani.Tarehe 8 mwezi Mei mwaka 2006 Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya inawakumu watu wawili,Dickson Shapwata na Nelson Mwazembe, kunyongwa baada ya kupatikana na tuhuma za kumuua na kumchuna ngozi Marehemu Loti Nzowa mnamo mwaka 2001.

Kanda ya Ziwa.Miaka ya hivi karibuni.Mauaji ya vikongwe wenye macho mekundu yanazidi kushika hatamu.Tuhuma dhidi ya vikongwe hao ni uchawi.Mtani wangu mmoja Msukuma wa Shinyanga ananinong'oneza kwamba amemshauri babu yake aache kuvuta ugoro ili macho yake yasiwe mekundu.Mtani wangu mwingine anadai kwamba vikongwe wenye macho mekundu wanauawa kwa sababu wekundu huo ni matokeo ya wao kukesha wakiwanga usiku.Utani kando,mauaji ya vikongwe bado yanaendelea japo hadi sasa ni vigumu kuelewa kwanini yashamiri Kanda ya Ziwa pekee.

Sehemu mbalimbali Tanzania.Mwaka 2008.Taarifa zinatapakaa kwamba maalbino wanawinda na wanauawa na watu wanaodaiwa kuhitaji viungo kutoka miilini mwa maalbino hao kutengenezea dawa za baishara.Mwandishi wa BBC,VIcky Ntetema,anapata vitisho wakati anatengeneza documentary kuhusu mauaji ya maalbino.Kwa mujibu wa mwandishi huyo,mwaka huu tayari maalbino 25 wameshauawa maeneo ya Mwanza,Shinyanga na Mara.Mwezi Machi mwaka huu,chama cha maalbino mkoani Tanga chatangaza sensa ya maalbino.Mwezi huohuo Serikali mkoani Mwanza inatangaza kuangalia uwezekano wa polisi kuwapatia ulinzi maalbino.

Hii ndio Tanzania yetu ambayo ushirikina unazidi kushamiri.Wapo watakaonipinga lakini ukweli ndio huo.Wanaofuatilia nyendo zisizo rasmi za siasa za nyumbani wanadai kwamba hata baadhi ya wanasiasa wanaosimama majukwaani kukemea mauaji ya vikongwe au maalbino nao wanategemea sana ndumba katika maisha yao ya kisiasa.Wengi tunakumbuka yaliyojiri katika kikao cha Bunge kilichopita ambapo mheshimiwa mmoja alituhumiwa kumwaga ndumba bungeni japo ishu hiyo iliisha kimyakimya.

Kwenye sosholojia ya dini tulifundishwa kwamba kabla ya ujio wa dini za kimapokeo (Ukristo,Uislamu,nk) jamii za Kiafrika zilikuwa zikifuata dini zao za asili (African Traditional Religions-ATRs).Na hadi sasa,dini za asili zina ushawishi mkubwa kwa waumini wa dini za kimapokeo.Tunafahamu Wakristo au Waislam wengi ambao pamoja na kwenda makanisani au misikitini hawasahau kuomba mizimu ya kale.Kwa waliozaliwa na kukulia Dar,sio rahisi sana kuelewa hili nalozungumzia lakini hilo linajulikana sana kwa "wakuja" wenzangu.Sasa,tatizo lipo katika kuchora mstari unaotenganisha dini za asili na ushirikina.Kule kwetu Undambani kuna mababu (wanaitwa "mambuyi" kwa Kindamba) wanaoaminika kufanya miujiza (kutibu,kuepusha ukame/njaa,nk) wanapoombwa kwa dhati.Inaaminika pia kwamba "mambuyi" hao wana uwezo wa kumduru mtu.

Tukirudi kwenye sosholojia ya dini tunaambiwa kuna roho mfu za aina mbili,dead-dead na living-dead.Marehemu wanaokufa na kuenziwa,hubaki kuwa mzimu yenye inayotarajiwa kuleta mema.Marehemu wanaotelekezwa (kwa mfano wanaokufa ajalini na maiti zao kuzikwa na jiji) hugeuka kuwa mzimu yenye uwezo wa kuleta mabaya kwa vile wamesahaulika.Pengine hapa ni vizuri kushauri wazazi kutosahau kutoa "sadaka" ya jina la marehemu babu,bibi,baba,mama au yeyote yule katika ukoo ili kuwaenzi kwa minajili hiyo ya baraka za mbeleni.

Ni vigumu kubashiri iwapo mauaji ya maalbino yatakwisha kwani hata hayo ya vikongwe bado yanaendelea.Tatizo kubwa zaidi linalozikabidili jamii zetu za Kiafrika ni watu kutafuta njia za mkato katika kutimiza malengo au matakwa yao.Ushirikina unashamiri zaidi kwa namna hiyo.Mtu anatafuta dawa ya kufaulu mtihani,anakwenda kwa mganga na kutakiwa apeleke kichwa cha mtu mwenye kipara.Huyu ni mzembe ambaye anataka kupata njia ya mkato ya kufaulu badala ya kusoma kwa bidii.Mheshimiwa flani anataka kurejea bungeni lakini anakabiliwa na upinzani mkali kwa vile hajaonekana jimboni tangu achaguliwe katika uchaguzi uliopita.Anakwenda kwa mganga anaambiwa alete moyo wa albino.Unategemea nini hapo?

Haya ya vikongwe wenye macho mekundu na maalbino ni mwendelezo tu wa ushirikina katika jamii zetu.Yayumkinika kuamini kuwa huko mbele wenye vipara,vitambi,matege,makengeza na pengine hata wenye mustachi wanaweza kuwa wawindwa wa hawa wanaotaka mafanikio kwa njia ya mkato.Mbinde itakuwa pale washirikina hao watakapoanza kuwinda watu wenye fedha nyingi katika akaunti zao ambazo hazikupatikana kihalali!Pengine ndio utakuwa mwisho wa ufisadi.Just thinking aloud!


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget