Kuna busara moja inayotuasa kuwa mpuuzi husema kwa vile anajiskia kusema (hata kama ni upuuzi) ilhali mwenye busara husema tu pale anapokuwa na kitu cha kusema (ikimaanisha kama hana cha kusema,au haoni umuhimu wa kusema kitu,atakaa kimya. Busara zaidi zinatuasa kuwa makini na tunayosema hadharani kwa vile mara nyingi jamii humtambua zaidi mtu kwa kauli zake.Sema upuuzi,utaonekana mpuuzi.Sema ya busara,utaonekana mwenye busara.Sasa kuna huyu msomi,Dokta Benson Bana,ambaye licha ya kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam,ni mkuu wa idara ya Sayansi za Siasa na Uongozi na pia ni Mwenyekiti Mwenza wa REDET.Yayumkinika kusema Dkt Bana amekuwa mahiri zaidi wa kutoa kauli zisizoendana na wasifu wake kitaaluma kuliko umahiri wa wa usomi wake
Na leo,kwa mujibu wa habari katika gazeti la Mwananchi,msomi huyo 'amelipuka' tena kwa kauli kwamba tuhuma zilizokithiri dhidi ya ufisadi zinaweza kusababisha taifa kukosa viongozi wazuri wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba.Huhitaji kuwa na hata asilimia moja ya kiwango cha elimu ya Dkt Bana kutambua kuwa tuhuma zilizotapakaa kuhusu ufisadi ni matokeo ya kuwepo kwa ufisadi.Msomi huyu anaishi Tanzania lakini yaelekea hafahamu mazingira yanayomzunguka,na hilo linaleta wasiwasi mkubwa kuhusu mchango wa wanataaluma katika maendeleo ya nchi yetu.
Katika habari hiyo Dk Bana aliwataka watu "waaache siasa chafu za kuhubiri na kudai kuwa watuhumiwa wa ufisadi hawafai kupewa kura au kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kana kwamba wameshathibitika".Huu ni zaidi ya ubabaishaji wa kitaaluma,na kwa kiasi flani inaaibisha Udaktari wa Filosofia tunaohenyea akina sie.Kwanza,Dkt Bana amepata wapi mamlaka ya kuwataka wananchi waache kulalamikia ufisadi?Usomi hautoi mamlaka ya kuizuia jamii kulalamikia maovu yanayoisumbua.Pili,kwa mtizamo wa msomi huyu,kwa vile tuhuma za ufisadi hazijathibitika basi watu wakae kimya hadi 'miujiza itapotokea kwa watawala wetu kuamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mafisadi'!Hii ni sawa na kuingiliwa ndani na kibaka halafu ukakaa kimya kwa vile tu wewe sio chombo cha sheria.Ukifanya hivyo,hata hao polisi watakuona mpumbavu na unawapotezea muda.La kufanya ni kumdhibiti kibaka au kupiga kelele kuwashtua majirani wakusaidie kumdhibiti.
Binafsi,pamoja na kuheshimu uhuru wa kutoa mawazo,nadhani tatizo kubwa la Dkt Bana ni tabia yake ya 'kusema chochote' hata kama hana cha kusema.Inaelekea aidha hafahamu athari za tabia hiyo au anapuuza tu.Matokeo yake ni kuonekana mbabaishaji wa namna flani.Si lazima jina lake lionekane magazetini au kusikika radioni kama hana la muhimu kuieleza jamii.Eti anatuasa kuwa "si vizuri kwa watu kunyimwa kura kwa sababu ya kutuhumiwa kwa ufisadi hadi hapo watakapothibitika na kutaka wanasiasa waache kuhukumu wenzao bila kosa".Kwanini hajiulizi inakuwaje watu hao wanatuhumiwa ufisadi in the first place?Kwanini ni wao na si Dokta Bana,kwa mfano?
Hivi lipi lililo muhimu zaidi kwa Tanzania kama taifa: kukosa viongozi bora kwa vile wanatuhumiwa kwa ufisadi au kupata viongozi bora watakaowajibika kulitumikia taifa kupambana na ufisadi?Wasiwasi wa Dkt Bana ulipaswa kuwa kwenye athari za ufisadi kwa jamii na sio tuhuma za wananchi dhidi ya mafisadi.Ni mlevi tu atakayeshindwa kuelewa kuwa kinachoumiza Watanzania kwa sasa ni UFISADI na sio TUHUMA DHIDI YA MAFISADI.
Mwanataaluma huyu anaongoza taasisi ya REDET ambayo mara imekuwa ikishutumiwa kwa upendeleo inapotoa taarifa za kura zake za maoni (opinion polls) kuhusu CCM na vyama vingine vya siasa.Sina hakika kuwa matokeo ya kura hizo huwa 'yanapikwa' ili kuridhisha watawala lakini kinachozua maswali dhidi ya polls hizo ni kutoendana na hali halisi na dalili za upendeleo.
Wito wangu kwa Dkt Bana ni huu: wakati mwingine jaribu kuitendea haki taaluma yako kwa kukaa kimya pale usipokuwa na cha kuongea.Kwa kufanya hivyo,utawatendea haki pia wasomi wenzako,taasisi unazoongoza na fani nzima ya usomi.Ni muhimu pia unapotoa matamshi mazito ukajitahidi kutumia theories za kusapoti matamshi hayo badala ya kutoa hisia zenye mwelekeo wa kijiweni.
.
0 comments:
Post a Comment