Kama nilivyoahidi siku chache zilizopita kuwa blogu yako ingekuletea mahojiano mengine exclusive kutoka kwa mmoja wa Watanzania wanaotuwakilisha vema,leo natimiza ahadi hiyo kwa kuwaletea exclusive interview na msanii mahiri wa Bongoflava,anayefahamika kama Mzee wa Commercial.Huyo si mwingine bali ni Ambwene Yesaya,au AY kama anavyofahamika na wengi.Kama ilivyokuwa katika mahojiano ya Mwana FA,interview hii itapatikana pia katika sura ya Kiingereza (English version).Tuaanza kwanza na WASIFU wa AY kabla ya kuingia kwenye mahojiano kamili.Pata vitu:
MSANII TANGU UTOTONI:
AY alianza kijihusisha na fani ya muziki tangu udogoni.Alipokuwa shule ya msingi alishiriki katika mashindano mbalimbali ya kutafuta vipaji na pia alitumbuiza katika hafla mbalimbali.Mwaka 1996 akiwa high school aliunda kundi la S.O.G lililojumisha wasanii watatu (akiwemo AY) na walirekodi albamu yao ya kwanza mwaka 2000.
KUKUA KISANII:
Mwaka mmoja baadaye,AY aliamua kufanya kazi za kisanii peke yake (solo) na kufyatua albamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina ‘Raha Kamili’.Wimbo wa kwanza kutambulisha albamu hiyo, ‘Raha Tupu’ ulipata mafanikio makubwa na kukamata chati za vituo vya radio na runinga,na hatimaye kumtambulisha rasmi AY katika anga za muziki nchi Tanzania.
‘Machoni Kama Watu’, single ya pili (kutoka katika albamu ya ‘Raha Kamili’) iliyomshirikisha Lady Jaydee ilifanya vizuri sana kwenye chati mbalimbali za muziki na ulisaidia sana kupaisha mauzo ya albamu hiyo katika soko.
KUJIIMARISHA KISANII:
Mwaka 2005,AY alitoa albamu yake ya pili aliyoipa jina ‘Hisia Zangu’, na ‘Yule’, single ya kwanza kutoka katika albamu hiyo, ilikamata chati mbalimbali za muziki.Katika albamu hii,AY aliwashirikisha wasanii mbalimbali maarufu katika Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Prezzo,Tattuu na Dexu Vultures (wote kutoka Kenya) na msanii Maurice Kirya kutoka Uganda.Hii ilisaidia sana kumtangaza zaidi AY nje ya mipaka ya Tanzania.Single yake ya pili, ‘Binadamu’,ilifanya vizuri sana ukanda mzima wa Afrika Mashariki na hatimaye kuteuliwa kugombea Tuzo za Kora,jambo lililoandika historia kwani AY ni msanii wa kwanza wa kiume kutoka Tanzania kuteuliwa kugombea Tuzo hiyo.
KUJIKITA ZAIDI KATIKA MUZIKI
Umaarufu wa AY ulizidi kuongezeka hasa baada ya kutoa albamu hiyo ya pili,na sasa alitambulika kama mmoja wa wasanii mahiri wa Afrika Mashariki.Mwaka 2006 alifanikiwa kupata mkataba wa kutangaza kinywaji (kikali) cha ‘Konyagi’ ambacho ni maarufu ndani na nje ya Tanzania.Mkataba huo ulichangia AY kutambulika zaidi kupitia matangazo ya kinyaji hicho,na ulifungua njia kwa makampuni mengine,kama Coca Cola,Vodacom,Celtel (sasa Tigo) na Kilimanjaro Lager kuingia mikataba na msanii huyo.
STAILI:
Staili ya muziki wa AY ni hip-hop inayozungumzia ishu na maisha ya Mwafrika hivi sasa.Maudhui hayo yanawasilishwa kwa ucheshi lakini pia yanaburudisha.Muziki wa AY unawagusa watu wa rika lote.
TUZO:
Msanii huyo amefanikiwa kuteuliwa katika/kushinda tuzo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.Tuzo hizo ni pamoja na
1 Mwaka 2005 aliteuliwa kugombea Tuzo ya Kora katika kundi (category) ya Msanii Bora wa Kiume kwa Afrika Mashariki na Kati.Wimbo ulioteuliwa ni ‘Binadamu’.
2 Mwaka 2006 aliteuliwa kugombea Tuzo za Kisima (nchini Kenya) katika kundi la Msanii Bora wa Kiume kutoka Tanzania.
3 Mwaka 2007 aliteuliza kugombea Tuzo za Kilimanjaro (Kilimanjaro Music Awards) katika kundi la single bora ya hip-hop.
4 Mwaka huohuo aliteuliwa tena kugombea Tuzo za Kisima (nchini Kenya) katika kundi la video bora ya hip-hop kutoka Tanzania.
5 Mwaka 2007 uliendelea kuwa wa mafanikio kwa AY baada ya kuteuliwa pia kugombea Tuzo za Lulu ya Afrika (Pearl of Afrika) katika kundi la single bora ya hip-hop kutoka Tanzania.
6 Mwaka 2008 AY aliteuliwa kugombea Tuzo za Kilimanjaro katika kundi la collaboration (ushirikiano wa msanii zaidi ya mmoja) bora.
7 Mwaka huohuo,msanii huyo aliteuliwa tena kugombea Tuzo za Lulu ya Afrika katika kundi la msanii bora wa kiume kutoka Tanzania.
8 Katika mwaka huo,Akon-msanii maarufu duniani kutoka Marekani,alikiri hadharani kuwa anavutiwa na staili ya muziki wa AY na akamtabiria kuwa anaweza kabisa kuwa msanii kutoka Afrika atakayefanya vizuri katika anga za muziki kimataifa.
9 Mwaka huu,AY ameteuliwa kugombea tuzo kadhaa ikiwa ni pamoja na Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (kundi la video bora na wimbo bora wa mahadhi ya Reggae),Tuzo za Teen Extra za nchini Kenya (kundi la video bora,msanii bora wa mwaka,collaboration bora ya Afrika,wimbo bora wa mwaka Afrika Mashariki,wimbo bora wa hip-hop, na msanii bora wa kiume).
10 Na hivi karibuni AY alishinda kuwa msanii bora wa Afrika Mashariki katika Tuzo za Teenez nchini Kenya.
MAFANIKIO:
Hadi sasa msanii huyo ameshajikusanyia Tuzo sita.Pia vibao vyake 14 vimefanikiwa kukamata chati mara katika ukanda wa Afrika Mashariki.Kibao chake kinachonyanyasa zaidi ni King and Queens (Wafalme na Malkia),na kimepelekea kumpatia tuzo na umaarufu zaidi kimataifa.Wakati mahojiano haya yanafanyika,wimbo wake ‘Habari Ndio Hiyo’ ulikuwa unakamata nafasi ya 10 katika chati za muziki kwa Afrika (Radio Express-Africa Chart).AY amefanikiwa kuwa msanii pekee wa Kitanzania aliyefanya collaboration nyingi zaidi na wasanii wa nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Chameleone na Ngoni (Uganda),Amani,Nameless na Juacali (Kenya), P Square na J. Martini (Nigeria) na wengineo.
Uzinduzi wa albamu za AY umekuwa wa kihistoria na wenye mafanikio makubwa chini ya udhamini wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na ulifanyika wakati wa matamasha ya wasanii wa kimataifa kama vile Fat Joe,Eve,Shaggy,nk nchini Tanzania.Kadhalika msanii huyo alikuwa miongoni mwa wasanii walioshiriki tamasha kubwa la kuhamasisha vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi (Music Against HIV/AIDS) liliodhaminiwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).Pia ameshiriki Coke Side of Life Tour kwa Afrika Mashariki,Tamasha la Vijana la Afro Arab nchini Uganda,Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (Zanzibar International Film Festival),na Tamasha la Sauti za Busara.Kadhalika,AY amewahi kualikwa kutumbuiza wakimbiki kutoka Burundi na Rwanda kwa udhamini wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR),alitumbuiza katika sherehe za kuukaribisha mwenge wa Olimpiki nchini Tanzania,na mwaka jana alialikwa kutumbuiza katika Tuzo za Muziki za MTV barani Afrika nchini Kenya.Vilevile,msanii huyo ameshatumbuiza katika nchi mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na eneo la Afrika Mashariki,Rwanda,Burundi,Dubai,Afrika Kusini,Marekani na Uingereza.
NINI KIPYA?
Hivi karibuni AY amezindua tovuti yake inayopatikana katika anuani www.ay.co.tz. Pia single yake ya ‘Binadamu’ itakuwa miongoni mwa nyimbo katika albamu inayoandaliwa na kampuni ya kimaifa ya muziki,Warner Music (Africa).Kadhalika,msanii huyo ameingia mkataba wa kutangaza kinywaji (kikali) cha Waragi nchini Uganda sambamba na mkataba na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.Kwa sasa anandaa ushirikiano na wasanii wa kimataifa kama J. Martin wa Nigeria na wengineo kutoka Afrika Kusini na Marekani.
JE WAJUA?
Kwamba jina halisi la AY ni Ambwene Yesaya?
Staili ya AY ni ‘simple and casual’?
AY alizaliwa Julai 5 na nyota yake ni Kansa?
Rangi aipendayo zaidi ni bluu?
Scent (harufu ya perfume au manukato) aipendayo ni DKNY?
Na msanii anayemvutia zaidi duniani ni Dr Dre?.
MAHOJIANO KAMILI YANAFUATA (BONYEZA) HAPA CHINI .
KULIKONI UGHAIBUNI (K.U): Kwanza blogu hii inatoa shukrani kwa kukubali ombi la kufanya mahojiano haya maalum. Pili, hongera sana kwa kuteuliwa na hatimaye kushinda Tuzo za Teneez Kenya 2010.Wasomaji wangependa kufahamu kwanini unajulikana kama Mzee wa Commercial
MAHOJIANO KAMILI YANAFUATA (BONYEZA) HAPA CHINI .
KULIKONI UGHAIBUNI (K.U): Kwanza blogu hii inatoa shukrani kwa kukubali ombi la kufanya mahojiano haya maalum. Pili, hongera sana kwa kuteuliwa na hatimaye kushinda Tuzo za Teneez Kenya 2010.Wasomaji wangependa kufahamu kwanini unajulikana kama Mzee wa Commercial
A.Y: Producer P.Funk ndio alianza kuniita hiyo baada kuwa kila nikienda Bongo Records alikuwa anaweka beats za aina tofauti na tukawa tunaflow na artists wengine so akaona kila beat naenda nayo na wengine walikuwa wanashindwa katika beats nyingine so akawa ananiita mzee wa commercial ila kwa sasa nimekuwa wa commercial ya muziki wa biashara na biashara kwa ujumla.
K.U: Laiti AY asingekuwa Mzee wa Commercial (yani usingekuwa msanii) unadhani leo angekuwa nani (katika fani gani)?
A.Y: nilikuwa na ndoto sana ya kusomea urubani na naamini ningeendelea nadhani ndoto yangu ingetimia coz nikiamua kufanya kitu naakikisha nimekifanikisha
K.U:Kitu gani kilichokusukuma kuingia kwenye fani ya muziki?
A.Y: kutokana na kusikiliza nyimbo za wasanii wengine wa nje na kuona mbona naweza kujitahidi nikafanya kama wao.
K.U: Kabla hatujagusia mafanikio yako kisanii ,nini hasa kimekuwezesha kubaki kwenye chati kwa kipindi kirefu kiasi hiki?
A.Y: bidii,nidhamu na malengo katika kazi,naipenda kazi yangu na najifunza kila siku na kukubali kuwa kila kitu kinaweza kubadilika
K.U: Tuje kwenye mafanikio yako kisanii.Licha ya kuweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza wa kiume kuteuliwa kugombea tuzo za Kora na baadaye tuzo za Kisima,kuna mafanikio gani mengine unayoyahusisha na fani ya muziki?
A.Y:Ni mengi. (Zaidi angalia wasifu hapo juu)
K.U: Miongoni mwa vilio vya wanamuziki wa Tanzania ni suala la ‘wadosi’.Kama msanii mwenye mafanikio makubwa umewezaje kupambana na suala hilo?
A.Y: hili nimeliongelea sana na sasa sihusiki nao kwa sasa naweza kusema ni tatizo sugu na linaweza kumalizika au kupungua ila naona wengi wenzangu wanaendelea kufanya biashara isiyo kuwa transparent
K.U: Nilidokezwa na Mwana FA kuhusu kampuni yako inayoshughulikia usimamizi na usambazaji wa muziki ijulikanayo kama Unity Entertainment.Wasomaji wangependa kufahamu japo kwa ufupi kuhusu wazo,maendeleo na ufanisi wa mradi huu.
A.Y:(angalia wasifu hapo juu) mpaka sasa kampuni yangu imekuwa na ni wakala wa wasanii wengi ukanda huu wa afrika mashariki kama mwana fa,shaa,nameless,j.martins wa nigeria ambae nimemleta kwenye new campaign ya zain,p.square,amani,chidi benz na wengine wengi wa afrika
K.U:Tuje kwenye ushiriki wako na hatimaye kujitoa kwenye kundi la East Coast Team.Sababu zipi zilipelekea wewe kujiengua?
A.Y: kutofautiana misimamo na malengo
K.U: Wakati ukiwa na kundi la East Coast kulikuwa na beef na wasanii wa Temeke.Je unadhani beefs zinasaidia au kudumaza maendeleo ya wasanii? (nauliza hivyo kwa sababu wakati mwingine baada ya kufifia kwa beef -kama hiyo yenu-baadhi ya wasanii nao wanafifia)
A.Y: zipo zinazojenga na zipo zinazobomoa
K.U: Je makundi (kama ilivyokuwa East Coast) yanaficha udhaifu wa wasanii dhaifu na kudumaza umahiri wa wasanii bora?(nauliza hivi kwa vile baadhi ya wana-East Coast ‘walipotea’ muda mfupi baada ya wewe na Mwana FA kujitenga):
A.Y: ni kweli kabisa,makundi mengi yakivunjika ndio mnapata ukweli kuwa nani anaweza na nani hawezi kujimanage
K.U: Unatambulika kama mwakilishi bora kabisa wa Tanzania kwenye tuzo mbalimbali za kimataifa (Kora,Kisima na sasa hii ya hivi karibuni ya Teneez 2010 huko Kenya ambapo umeibuka mshindi).Wasomaji wangependa kufahamu nini siri ya mafanikio yako?
A.Y: ni kama nilivyokwambia ni bidii na nidhamu na malengo bila hivyo huwezi kwenda mbali.na si hizo tu pia nimekuwa nominated kwa mtv awards 2009 (best hip hop artist nikiwa na jay z,kanye west na m.i)kili awards (2 categories),extra teneez awards (1category) na tuzo za Ghana zinaitwa moma (5categories-artist of the year- Africa,best male,collaboration,east African song,hip hop artist) nawaomba watanzania waweze kuvote online na kwa simu kwa walio Tanzania niweze kunyakua tuzo hizo,unaweza kugogle then upate informations
K.U: Kumekuwepo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wasanii kuhusu baadhi ya tuzo za hapo nyumbani hususan suala la upendeleo na mapungufu katika upangaji makundi (categories).Nini mawazo yako katika suala hili?
A.Y:zingine naweza kusema kweli na kuna wakati wasanii wanatakiwa kukubali matokeo maana ukikubaki kuingia katika mashinda jua kuna kushinda na kushindwa
K.U: Ukiwa kama msanii uliyedumu kwenye fani kwa muda mrefu,unaonaje maendeleo ya bongoflava ndani na nje ya Tanzania?
A.Y: inazidi kwenda mbele na kwa sasa wanaoipeleka mbele si wengi so nawaomba wenzangu tuongeze bidii na kutengeneza network zaidi ndani na nje ya nchi
K.U: Baadhi ya kazi zako zimetengenezwa na producers wa nje ya Tanzania.Je kuna tofauti yoyote kati ya kazi zako zinazotengenezwa na producers wa nyumbani na hizo zinazotengenezwa nje?
A.Y: ni ladha hazifanani,napenda sana kuchange plava mara kwa mara kwa audio na hata video
K.U: Swali linaloshabihiana na hilo lililopita.Je kufanya kazi na producers wa nje kunaweza kumsaidia msanii kufanya vyema katika nchi anayotoka producer huyo?
A.Y: sana tu mfano mzuri ni mimi mwenyewe na producer naofanya nao na nafurahi kuona wasanii wengine wa tz wameanza kufuata nyao zangu kwa kuanza kusafiri kurecord sehemu mbali mbali na kushirikiana na wasanii wa nje maana soko limeanza kuwa la afrika na si vile zamani kuwa la kibongo tu,angalia hata charts za redio records nyingi za nje na ndani zinaingia kwa pamoja
K.U: Umewahi kushiriki kwenye fani ya filamu (ambapo ulihusika kwenye filamu ya Girlfriend).Je una mpango wa kuendelea na fani hiyo huko katika siku za usoni?
A.Y:bado sijafikiria kwa kweli kama nitafanya movie
K.U:Vipi kuhusu umodo hasa ushiriki wako kwenye matangazo mbalimbali ya biashara.Je una mpango wa kuwa full-time model licha ya muziki?
A.Y:hapana ila muda wote huwa wananunua image au sauti yangu kwa ajili ya products zao au campaign zao.
K.U: Unawezaje kumudu majukumu yote hayo (muziki, umodo, biashara) pasipo kuathiri ufanisi wako?
A.Y:na masomo pia,nasomea business administration ktk chuo cha Learn IT,mi ni mtu wajukumu tangu zamani sana so najua kuhandle pressure zote na huwa naishi kwa ratiba maalumu ambazo naziweka kwa simu na calendar yangu.
K.U: Umefanikiwa sana kuteka soko la bongoflava katika eneo la Afrika Mashariki.Nini mipango yako ya baadaye kutanua mafanikio hayo maeneo mengine ya Afrika na nje ya bara hilo?
A.Y:Nimeanza kupata bookings za S.A,DJIBOUTI,NIGERIA na ZAMBIA na pia Ethiopia so nazidi kusogea zaidi.pia natoa wimbo wangu mpya niliomshirikisha J.MARTINS kutoka Nigeria so najua itanijenga zaidi.
K.U:Kwa uzoefu wako,na kwa kuzingatia mafanikio unayopata nje ya mipaka ya Tanzania,unadhani ni jambo gani linalopelekea wasanii wengine wengi wa hapo nyumbani kushindwa kufanya vizuri kwenye anga za kimataifa?
A.Y: wengi ni wagumu kujifunza,kufanya networking.maana vile wengine wengi wa nje ya tz wanavyojituma ndio maana natumia style wazotumia wao.
K.U: Moja ya mambo yanayoisumbua Tanzania kwa sasa ni ufisadi lakini wasanii wengi wa bongoflava wamekuwa wakikwepa kuzungumzia suala hili kwenye tungo zao.Je ni sahihi kuyumkinisha kuwa mnaistarehesha jamii kwa vibao vyenu ‘vikali’ lakini mnawatenga kwa kutolipa kipaumbele suala la ufisadi kwenye tungo zenu?
A.Y: sidhani kama ukiimba ufisadi utaisha, nilichongundua ni kuwa watu hawaipendi nchi yetu ndio maana tunawafumbia macho wanaofanya ufisadi na tuna ile hulka ya kulalamika tu then hakuna hatua tunazochukua ndio maana ktuna matatizo mengi sugu tunayalalamikia tu halafu tunanyamaza
K.U: Nini mipango yako ya baadaye katika fani ya sanaa?
A.Y:kuna surprise kubwa nitawatangazia muda si mrefu naakika nitasogea/tutasogea kisanaa
K.U: Mwisho,una ujumbe gani kwa mashabiki wako na wapenzi wa bongoflava kwa ujumla?
A.Y: tuthamini na kuvipenda vya kwetu kwanza kabla ya vya wengine cz hata wao mnaona jinsiwanavyosupport vya kwao kwanza hata kama ni vibaya ila ni vyao na wanavipush sana mpaka wengine wanavikubali..
Blogu hii inakushukuru sana kwa kutumia muda wako kujibu maswali haya mengi.Pia inakutakia kila la heri na mafanikio katika shughuli zako.Na ni matarajio ya blogu na wasomaji wake kuwa tutapata fursa nyingine ya kuongea huko mbeleni.Asante sana.
ANGALIZO KUTOKA KWA AY: Nyimbo zangu na video zangu zitaanza kupatikana very soon online kupitia moja ya kampuni kubwa duniani,pia May hii nafungua duka la nguo mchanganyiko lipo sinza madukani.karibuni sana na kwa mawasiliano tutaweza kuwasiliana katika email yangu ya ay@ay.co.tz. Na hapa chini ni wasifu wa kampuni ya Unity Entertainment
Unity Entertainment Profile 2010
I like it!
ReplyDeleteUshackia Ambwene, we bonge la artist...bonge la artist. Wasanii kama wewe ndo wanaotakiwa East Africa.
ReplyDeleteila 1 thing, mbona hautumii vzuri website yako?
The only prbm is that u dnt update it, yani ina contents za kama miaka 2 iliyopita...
I believe u have a lot of news to give to ur fans and the best way to do that could be thru your web, or if you dont like your web to be filled with those kind of issues may be u can also lauch a blog or some thing lyk that....
i think through that u can attract a lot of companies to do their advartisments thru your web/blog(yeah i have seen str8 music but u can attract more than Portsman Co Ltd,example telecom companies like Voda and the lyks), if not so it can also help to advertise your other business lyk this Unity Ent, your cloth shop!!
All in all you are doing great man...Keep it up!! CIAO