Kama Mtanzania mzalendo na mwenye kupenda nchi yangu nawajibika kuwa na heshima kubwa kwa Rais wangu Jakaya Kikwete.Hata hivyo,heshima inapaswa kuendana na matendo ya mheshimiwa.Kwa maana hiyo,naamini simkosei heshima Rais wangu nikihoji baadhi ya busara zake.Mpaka muda huu sielewi nini kinaendelea kati ya JK,Husna Mwilima na Sophia Simba!Awali,Sophia Simba kama Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM alisimama kidete kuhakikisha Mwilima 'anapigwa chini'.Tuhuma zilizotolewa dhidi yake ni 'mapungufu katika utendaji wake wa kazi.'Sasa kama tukiamini kuwa ni kweli Mwilima alishindwa kumudu majukumu ya uongozi huko UWT,how come JK ameamua kumpa ukuu wa Wilaya? Na kwa kuonyesha kuwa mambo yanaendeshwa kienyeji,Mwilima hakuchelewa 'kutoa mipasho kwa wabaya wake' pale alipotamka bayana kuwa kuteuliwa kwake na JK kuwa DC wa Tandahimba ni 'majibu ya JK kwa akina Sophia Simba'.Huwezi kumlaumu kuwa 'ameropoka' kwa vile hakujiteua.
Lakini swali la msingi ni kwamba je ni kweli JK ameamua kumteua Mwilima kumwonyesha Sophia Simba na UWT yake kuwa mwanamama huyo (Mwilima)aliondolewa katika wadhifa wake huko UWT kwa mizengwe na si mapungufu ya utendaji kazi?Lakini kama jibu la swali hilo ni ndio,hivi JK si ndio Mwenyekiti wa CCM ambayo UWT ni jumuiya yake,na kwa maana hiyo alikuwa na uwezo wa kusimamia mtizamo wake kuwa Mwilima ni mtendaji kazi hodari?Kwanini aliacha mwanamama huyo adhalilishwe huko UWT kabla ya kuamua 'kumsafisha' kwa kumpa u-DC?
Katika picha kubwa zaidi,je inawezekana utoaji wa baadhi ya vyeo unafanyika sio kwa maslahi ya wananchi bali kusafishana na 'kupunguza maumivu ya kisiasa'?Nauliza hivyo kwa vile naamini kwamba kama Mwilima alikuwa ameonewa huko UWT,JK alikuwa na uwezo mkubwa wa 'kumlinda' kama alivyoamua 'kumlinda sasa' kwa kumpa u-DC.Kwa kukaa kwake kimya wakati Mwilima 'anapelekeshwa' huko UWT,inatafsiriwa kuwa alikuwa anaafikiana na maamuzi ya akina Sophia Simba.Lakini kwa uamuzi huu 'mpya' wa kumpa Mwilima u-DC,inatafsiriwa (kama anavyosema Mwilima) kuwa anafikisha ujumbe kwa akina Sophia Simba kuwa Mwilima 'alionewa tu huko UWT kwani bado ana sifa za kuongoza wananchi huko Tandahimba kama DC'!
Nilisema mwanzoni kuwa namheshimu Rais wangu JK lakini nadhani aidha ana washauri wabovu au yeye mwenyewe maamuzi yake ni dhaifu.Na bahati yake ni kwamba Watanzania wengi hawana muda wa kuhoji au 'kukomalia' baadhi ya maamuzi yake.Ni aibu kwa Rais wetu kugeuka sehemu ya mipasho ya akinamama hao (Mwilima na Sophia Simba).Ni dhahiri kinachofanyika hapo ni kupoza pande zote mbili,yaani JK kama Mwenyekiti wa Taifa wa CCM aliamua kukaa kimya pale Sophia Simba na wenzake walipomtimua Mwilima,lakini katika kumpoza Mwilima akaamua kumpatia 'zawadi' ya u-DC.
Halafu kwa mtindo huu tutarajie Maisha Bora kwa Kila Mtanzania?
Friday, 9 April 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment