Nimekuletea habari sita zilizopelekea nijiulize swali hilo hapo juu:TUNAELEKEA WAPI kama Taifa?Tutafakari pamoja...
Mwananchi: Polisi waibiana Sh3 bilioni za posho
Salim Said
SIRI ya kuchelewa kwa posho za askari polisi mwezi Febuari mwaka huu imefichuka baada ya kudaiwa kuwa maafisa watatu wa jeshi hilo walitoweka na hundi ya malipo hayo yanayofikia Sh3 bilioni.
Baadhi ya maofisa wa polisi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wiki hii, walielezea mazingira ya wizi huo na kusisitiza kuwa ngazi ya juu ya jeshi hilo imekuwa ikificha taarifa hizo, kwa hofu ya kuchafua sifa ya chombo hicho cha dola.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walisema fedha hizo ziliibwa na maofisa hao watatu baada ya kubadili maelezo kwenye hati ya malipo na kuielekeza katika akaunti za mmoja wao.
Mwananchi: Tanesco yapoteza umeme wa Sh 100 bilioni kwa mwaka
Sadick Mtulya
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Cag), Ludovick Utouh amesema kuwa upo uwezekano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kufilisika baada ya kubaini kuwa kila mwaka linakabiliwa na upotevu wa Sh 100 bilioni.
Alisema fedha hizo zinapotea wakati wa kusambaza nishati hiyo kutoka kwenye vyanzo vyake hadi kwa watumiaji.
Utouh alieleza kwenye ripoti yake, ambayo gazeti hili lina nakala yake amebaini shirika hilo limepata hasara ya Sh Sh48 bilioni mwaka uliopita kutokana na ununuzi wa umeme kutoka katika kampuni binafsi, ikiwemo IPTL kufuatia mgawo mkubwa uliojitokeza Septemba na Oktoba, mwaka jana.
Ripoti hiyo ya Cag iliyowasilishwa Aprili 6, mwaka huu katika kikao baina ya watendaji wakuu wa Tanesco na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Masharika ya Umma (Poac) kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, Poac iliiagiza Tanesco kuhakikisha inafanya jitihada za kujinasua katika hali hiyo.
Tanzania Daima: Mitambo jengo jipya la Bunge yakwama
na Kulwa Karedia, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, jana alilazimika kuahirisha kikao cha Bunge kwa muda wa dakika 45 kutokana na hitilafu ya mitambo ya mawasiliano ndani ya jengo hilo jipya la Bunge.
Spika Sitta alifikia hatua hiyo baada ya kuingia ukumbini, majira ya saa 2.59 na kuanza kusoma dua kama kawaida, ingawa alilazimika kukatisha tena baada ya kipaza sauti chake kutofanya kazi.
Jambo hilo lilisababisha Spika kuendesha dua kwa sauti ya chini huku baadhi ya wabunge wakipigwa na butwaa.
Habarileo: Wagombea watarajiwa wadaiwa kuhonga majeneza
WATU kadhaa waliotangaza au kuonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ukiwemo ubunge wanadaiwa kutoa rushwa yakiwemo majeneza.
Kisheria kipenga cha kuanza kampeni za kuwania urais, ubunge na udiwani hakijapulizwa na hata kampeni za ndani ya vyama hazijaruhusiwa.
Kampeni hizo haramu zimekuwa zikifanyika hadharani katika mikusanyiko ya watu inayohusu mambo ya kijamii zaidi kuliko siasa na mbaya zaidi imebainika kuwa wagombea hao wamekuwa wakivizia misiba, wakati jamii ikiomboleza kuondokewa na ndugu au jamaa, wao wanafikiria kura za waombolezaji.
Kutokana na hali hiyo ambayo imeonekana kwa wanaotangaza nia za kugombea ubunge kupitia vyama mbalimbali, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imebainisha mwishoni mwa wiki kwamba inafahamu kuwepo kwa vitendo hivyo na imeanza kuwafuatilia wanasiasa hao.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma wa Takukuru, Mary Mosha alibainisha hayo alipokuwa anatoa mada kwenye semina ya kujadili mbinu sahihi za kuripoti habari za uchaguzi mkuu, inayowashirikisha waandishi waandamizi na wahariri wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo na HabariLeo Jumapili.
Raia Mwema: Utata mpya waibuka 'EPA namba mbili'
Mwandishi Wetu
Aprili 14, 2010
Ni fedha za stimulus package alizozitetea Kikwete bungeni
Gavana BoT aruka kiunzi, amtupia mpira msaidizi wake
SAKATA la matumizi yenye kutia shaka ya fungu la fedha lililopitishwa na Bunge kwa ajili ya kuhami uchumi, maarufu kama stimulus package , sasa limemrudia Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndulu, ambaye baada ya baadhi ya kampuni za ununuzi wa pamba kukosa mgawo huo katika mazingira yanayozua maswali zilimtaarifu naye akawajibu kuwa Serikali haina fedha.
Hata hivyo, wakati Gavana akitoa majibu hayo kuwa “Serikali haina fedha” si fedha zote Sh. trilioni 1.7 zilizoidhinishwa na Bunge la Tanzania ndizo zilizotumika katika mpango huo wa kunusuru uchumi uliotikiswa baada ya uchumi wa dunia kuyumba.
Wiki hii Gavana Ndulu amekwepa kuzungumzia suala hilo, akidai kwamba kwa sasa linashughulikiwa na mtu maalumu chini yake anayepaswa kutafutwa kuzungumzia suala hilo.
Raia Mwema ilipozungumza na Profesa Ndulu, ambaye alieleza kuwa yuko mkoani Mwanza kwa ajili ya mkutano, alisema masuala ya ‘‘stimulus package’’ yamekabidhiwa mtu maalumu ndani ya benki hiyo, na kwamba si yeye anayeweza kuyazumngumzia.
“Haya masuala ya stimulus package tumempa mtu maalumu ambaye ni mkuu wa kitengo cha sera na utafiti, mimi siwezi kuyazungumzia,” alijibu Ndulu hata alipotakiwa kujibu yale yanayomhusu moja kwa moja katika sakata hilo pia hakuwa tayari kuzungumzia.
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa fedha zilizokwishakutumika ni sehemu tu ya Sh trilioni 1.7 zilizopitishwa na Bunge, ambazo ni takriban Sh bilioni 870.8. Fedha hizo Sh bilioni 870.8 kwa mujibu wa taarifa zilizopo ndizo zilizokwishakutolewa na Benki Kuu (BoT), chombo ambacho kimepewa mamlaka ya kutoa fedha hizo.
Kwa mujibu wa utaratibu wa BoT, fedha hizo hutolewa kutoka benki hiyo kwenda katika benki ambazo zilikopesha kampuni zinazostahili kufidiwa, ambazo zimeathiriwa na mtikisiko wa uchumi duniani.
Nipashe: Sungusungu wawavua nguo walimu na kuwachapa vibokoNA ANCETH NYAHORE
14th April 2010
Walimu watatu wa kike na mke mmoja wa mwalimu wa kijiji cha Sakasaka, tarafa ya Kisesa wilayani Meatu, wamevuliwa nguo na kucharazwa viboko na walinzi wa jadi sungusungu wa kijiji hicho kwa madai ya kutohudhuria mkutano uliokuwa umeitishwa na jeshi hilo.
Imedaiwa kuwa walimu hao walishindwa kwenda kwenye mkutano huo kwa sababu ni wajawazito jambo ambalo sungusungu hao walipinga na kuwalazimisha wavue nguo kuthibitisha kama kweli ni wajawazito mbele ya mkutano huo.
Tukio hilo la aina yake na udhalilishaji kijinsia, lilitokea AprilI 7, mwaka huu kati ya saa na 4:00 na 5:00 asubuhi kijijini hapo.Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) wa wilaya ya Meatu, Baraka Owawa, aliiambia Nipashe kuwa walimu hao walikamatwa na sungusungu hao na kuanza kuwapiga, kuwavua nguo kwa madai ya kutohudhuria mkutano.Owawa alisema walimu hao hawakuwa na jinsi yoyote ya kukabiliana na sungusungu hao bali walitii amri hiyo ya askari hao wa jadi kunusuru maisha yao.
Mara baada ya walimu hao kufanyiwa unyama huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Julius Mtuli, alitoa taarifa kwa uongozi wa juu wilayani hapa ikiwemo polisi na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu na timu maalum kuundwa kwenda kijijini hapo kufuatilia suala hilo.
0 comments:
Post a Comment