Monday, 9 August 2010

Ni dhahiri kwamba CCM ikipata mpinzani wa saizi yake inatikisika.Sio siri,tangu Chadema wamtangaze Dkt Wilbroad Slaa kuwa mgombea wao wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu ujao,chama hicho tawala ambacho kimekuwa madarakani kwa takriban nusu karne,kimeanza kupatwa na "mchecheto".Hakijiamini.

Kituko cha kwanza ni uamuzi wa chama hicho kukataa wazo lililotolewa na Dkt Slaa kwamba uandaliwe mdahalo kati ya wagombea urais.Akipingana na wazo hilo,Katibu Mkuu wa CCM,Yusuph Makamba alidai kwamba mgombea wao,Jakaya Kikwete,hawezi kupimwa kwa mdahalo, bali kwa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na mwekeleo wa sera za Chama.Makamba alidai, "Wananchi hawana sababu ya kumpima Rais Kikwete, kwani walishampima kutokana na utekelezaji Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005... utafiti wa taasisi za kimataifa umeonyesha anakubalika pamoja na serikali yake,"

Ikumbukwe kuwa Kikwete alikacha wazo la mdahalo kwa wagombea katika uchaguzi uliopita mwaka 2005.Ungeterajia kwamba chama kilichokaa madarakani miaka nenda miaka rudi kijiamini,na kisiwe na hofu ya kumpambanisha mgombea wake na wagombea wa vyama vingine kwenye jukwaa huru ili wapiga kura wapate fursa japo moja ya kuwapima wagombea hao.CCM wanafahamu fika kuwa wazo la mdahalo kwa sasa ni hatari kwa vile wana maswali mengi ya kujibu lakini hawana majibu.Unadhani,kwa mfano, JK akiulizwa kuhusu Kagoda atajibu nini!Hizo ndizo sababu halisi zinazopelekea chama hicho tawala kuingia mitini kwa mara ya pili.

Kabla kiroja hicho hakijatulia,CCM wametuthibitishia tena namna gani walivyopandwa na "mchecheto" baada ya kuanza "kulialia" kuwa Chadema wanakiuka taratibu kwa kuanza kampeni kabla ya wakati stahili.Hivi CCM wanatufanya Watanzania wote tuna akili za kitoto au?Hivi ile hotuba ya JK wakati anachukua fomu za kuwa mgombea wa CCM haikuwa sehemu ya kampeni?Na alipohutubia Bunge na kueleza mlolongo wa mafanikio ya serikali yake ya Awamu ya Nne hakuwa anajipigia kampeni?Na alichoongea majuzi alipochukua fomu ya kugombea urais hapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi sio kampeni?Jamani,mbona CCM inajiabisha kiasi hiki?Mgombea wake anatamka bayana kuwa "vipaumbele vyake akipewa ridhaa ya kuongoza tena Tanzania vitakuwa A,B,C,nk" lakini kwa mtizamo finyu wa chama hicho hizo sio kampeni.

Kinachowatia tumbo joto CCM sio "Chadema kuanza kampeni mapema" bali ni dalili zinazoonyesha bayana kuwa chama hicho tawala kinaweza kuanguka kwenye uchaguzi ujao.Kimeanza kupaniki baada ya kuona halaiki za Watanzania wakojitokeza kwenye mikutano ya Dkt Slaa.Wametahayari baada ya kuona mgombea wao amedhaminiwa na watu elfu 14 na ushee tu ilhali Dkt Slaa kapata wadhamini zaidi ya milioni 1.Taratibu wanaanza kuona dalili ya upinzani wa dhati unaoweza kuwang'oa madarakani.

Kwanini CCM isijibidiishe kusafisha uozo unaoendelea kwenye mchakato wake wa kupata wagombea wake?Yayumkinika kusema kuwa japo hata huko nyuma zoezi hilo lilitawaliwa na rushwa lakini hii ya msimu huu ni kubwa kuliko zote.

CCM wanapaniki kwa vile wanamfahamu fika Dkt Slaa.Wanakumbuka vema namna alivyowaumbua na "List of Shame" (orodha ya mafisadi sugu),ambapo watajwa walitishia kwenda mahakamani lakini hakuna mmoja aliyediriki kufanya hivyo.Wanaelewa fika kuwa hoja ya ufisadi haijatolewa majibu ya kutosha na ni vigumu kwa chama hicho kujitenganisha na mafisadi wanaokilea.

Chama hicho tawala kinakabiliwa na mtihani mkubwa katika kufanya mchujo wa wagombea wake.Tayari kuna tetesi kuwa baadhi ya wagombea walioshinda wamepewa maksi pungufu.CCM inafahamu bayana kuwa baadhi ya waliokuwa wabunge wake wanaweza kuhamia Chadema na kuunganisha nguvu za chama hicho (Chadema) katika kuweka wazi uozo,madudu,ufisadi na uharamia mwingine uliofanyika katika utawala wa chama hicho.

Ushauri wa bure kwa CCM ni kwa chama hicho kilichopo madarakani hadi muda huu kufanya vitu vya "kiutu uzima" kwa kufuata kanuni zilizopo (ikiwa ni pamoja na kukabiliana na sualam la rushwa ndani yake) kabla ya kuangalia nani anafanya nini.Of course,two wrongs do not make a right lakini kwanini walalamike kuwa Chadema imeanza kampeni kabla ya muda ilhali CCM ilianza kampeni hizo kitambo?Mkuki kwa nguruwe....

Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha wale wote wenye uchungu na mapenzi ya dhati kwa Tanzania yetu kwamba kwa namna kampeni za ndani za CCM zilivyotawaliwa na rushwa iliyopindukia ni vigumu mno kwa chama hicho kupata wagombea safi watakaoweza kuwatumikia wapiga kura wao.Wakichaguliwa watakuwa bize zaidi kurejesha gaharama walizoingia katika kutoa rushwa wakati wa kampeni zao.Kura hizo za maoni zinapaswa kuwa msumari wa mwisho kwenye jeneza la chama hicho ambacho ni mahiri sana katika kuahidi makubwa lakini utekelezaji ni sifuri,zero,nada,zilch!

1 comment:

  1. Nani kakwambia kuwa Chadema wakishinda kutakuwa na maendeleo?Kama mwandishi lazima ujue maendeleo yanatokana na nini?Kwa kifupi nchi yetu haitakuwa na maendeleo kama sisi wananchi wenyewe hatutojituma(kufanya kazi kwa bidii)watu ni wavivu sana,maendeleo hayaji kwa maneno au mnataka Rais agawe pesa kwa kila mwananchi ndiyo maendeleo?Fanyeni kazi kwa bidii maendeleo mtayaona wacheni bla bla nyingi.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget