RAIS Jakaya Kikwete amewekewa pingamizi kortini kugombea urais mwaka huu kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka na ufujaji wa fedha za umma katika safari zake za nje.
Hayo yameelezwa na Mwalimu Mstaafu na Mkazi wa Dar es Salaam, Bw. Paul Mhozya ambaye amefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kupinga mgombea huyo katika uchaguzi wa Oktoba 31, mwaka huu.
Akizungumza na Majira jana, Bw. Mhozya alisema amefungua pingamizi hilo chini ya hati ya dharura akiitaka mahakama kulisikiliza mapema kabla kampeni kuanza, hivyo akaishauri CCM kuteua mgombea mbadala mapema, badala ya kusubiri uamuzi wa mahakama.
Katika hati ya mashtaka yenye sababu kumi za kuiomba mahakama imuengue Rais Kikwete kwenye kinyang'anyiro cha urais Bw. Mhozya anasema, rais ametumia nafasi aliyopewa kwa mambo binafsi, amekiuka katiba na kuvunja haki za binaadamu pamoja na matumizi holele ya fedha za watanzania kwa mambo yake mwenyewe.
Gazeti la The Citizen toleo la jana lilimkariri Bw. Mhozya kuwa aliwahi kufungua kesi ya kikatiba kama hiyo mwaka 1993 dhidi ya Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kuwa alivunja katiba kwa kuruhusu Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu (OIC), lakini ikatupwa na Jaji Barnabas Samatta kuwa mamlaka ya kumwondoa rais madarakani yalikuwa mikononi mwa bunge peke yake, chini ya kifungu cha 46A cha katiba.
Bw. Mhozya alisema amefikia uamuzi wa kufungua kesi hiyo kutokana na ujeuri uliooneshwa na Rais Kikwete katika miaka mitano ya uongozi wake, hivyo ni vema akazuiwa kuurudia kwa kumzuia asirudi madarakani.
Alisema anayo orodha ndefu ya mambo mabaya aliyofanya Rais Kikwete wakati wa uongozi wake, ambayo anatarajia kuyatumia kama ushahidi na uthibitisho wa malalamiko aliyopeleka mahakamani, ambayo anaamini yatakubaliwa na kumwondoa kwenye kinyang'anyiro.
"Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame alikwishasema kuwa tume iko tayari kupokea pingamizi dhidi ya mgombea yoyote kwa maslahi ya umma na kuwa itachukua hatua stahili, ninasubiri kauli ya mahakama na ninaamini itasikiliza hoja zangu na kuzifanyia kazi," alisema.
Alisema kuwa yeye kama Mtanzania anayo mamlaka chini ya ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufungua kesi dhidi ya uvunjaji wa ibara yoyote ndani ya katiba hasa zinazohusu haki za binaadamu.
Ibara ya 30 (3) inasema "Mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika Sehemu hii ya Sura hii au katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano, anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu"
Bw. Mhozya anasema pamoja na kuwa Rais ana kinga kisheria lakini Kikwete hana kinga ya kuwekewa pingamizi kama mgombea kwa sasa, ndio maana akaamua kufungua kesi hii wakati huu badala ya kusubiri atakaposhinda na kuwa rais, kwani atakuwa na uwezo wa kutumia kinga yake.
Alisema katika kipindi cha uongozi wake rais amefanya safari za ughaibuni zisizo za lazima nyingi kwa fedha za umma, jambo ambalo limesababisha wananch wengi kuishi maisha ya taabu na umaskini mkubwa, huku akidai kuwa urais ni suala binafsi, akisema kuwa ndio maana alimteua mwanawe kumtafutia wadhamini.
Alisema sheria inaitaka NEC kutoa muda wa ziada kwa chama ambacho mgombea wake amekufa au ameshindwa kuendelea kukiwakilisha, ili chama hicho kiweze kuteua mgombea mwingine, hivyo anaamini kuwa baada ya pingamizi hilo kukubaliwa mahakamani, NEC itawaamuru CCM kufanya hivyo kwa kuwaongezea muda.
"Sasa kwa vile sheria inasema NEC itawaongezea muda wa kuteua mgombea mwingine, mimi nashauri wakateua kabisa mgombea mwingine na kumshauri niliyemwekea pingamizi kujitoa, hii itaepusha kupoteza muda pindi pingamizi likikubaliwa, hakuna jinsi," alisema Bw. Mhozya.
Alisema yeye anahofia zaidi mustakabali wa nchi na vizazi vijavyo kuliko anavyohofia maisha yake, hivyo pamoja na vitisho anavyopata bado hataogopa kusimamia ukweli na kuwafichua waovu kama anavyofanya.
"Nimetoka mahakamani leo (jana), nilikwenda kuwaona makarani wa wanipatie 'samansi'(hati ya kuhudhuria mahakamani iliyo na tarehe ya kusikilizwa kesi) lakini walisema bado haijatoka naamini itatoka hivi karibuni ili tukasikilizwe. Matatizo yapo na nilikwisha yazoea," alisema Bw. Mhozya.
CHANZO: Majira
Wakati hayo yakimkumba JK,aliyekuwa Mbunge wa CCM (Bariadi) Andrew Chenge a.k.a Mzee wa Vijisenti nae anakabiliwa na tishio la pingamizi kutoka kwa mmoja ya wana-CCM waliokuwa wakiwania nafasi ya kupitishwa kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho
. Bonyeza HAPA Kusoma Zaidi Kuhusu Chenge.
Watu wengine wanapenda kesi, na hii sio gharama kufungua kesi? Sawa hata hivyo ndio demokrasia hiyo
ReplyDelete