Rais wa Rwanda Paul Kagame amechaguliwa tena kuongoza nchi hiyo baada ya kushinda kwa asilimia 93 katika uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni,lakini kulikuwa na taarifa zilizosambaa kuwa waandishi wa habari na wanasiasa wa vyama vya upinzani wameuawa au kuwekwa jela.Sasa,ripoti iliyovuja (leaked) ya Umoja wa Mataifa inaashiria kuwa jeshi la Rwanda linaweza kuwa limetenda uhalifu wa kivita na kuua makumi ya maelfu ya watu mwishoni mwa miaka ya 90 (late 1990s).
Kagame anaheshimika sana kwa kuleta maendeleo na amani kwa nchi hiyo iliyotiwa kovu na mauaji ya kimbari mwaka 1994 ambapo Wahutu (kabila kubwa nchini humo) waliwaua Watutsi (kabila dogo nchini humo)-na Wahutu wenye msimamo wa wastani- takriban milioni moja.Chini ya Kagame,ambaye ni Mtutsi na kamanda wa zamani wa jeshi,Rwanda sasa ni salama,huku ikitajwa kuwa miongoni mwa zenye rushwakidogo zaidi barani Afrika.Matokeo yake,nchi hiyo imekuwa ikipokea mamilioni ya dola katika misaada ya kimataifa na inaendelea kujijenga.
Lakini,kwa mujibu wa gazeti la New York Times,mmoja wa wapinzani wa Kagame alikutwa amekufa kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 mwezi huu,huku kichwa chake kikikaribia kutenganishwa na kiwiliwili.Na wapinzani wengine "maarufu ambao waliongea hadharani kumpinga Kagame na pengine kuuweka majaribuni umaarufu wa Rais huyo walizuiliwa kushiriki katika uchaguzi",kwa sababu za kiufundi.Kagame amehalalisha hatua kali alizowahi kuchukua huko nyuma,kwa mujibu wa gazeti hilo,akidai kuwa Rwanda bado haijatulia vya kutosha.
Kwa jinsi gani hali nchi humo haijatulia inabainishwa na katika ripoti ya kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binadamu,iliyopatikana na gazeti la Le Monde la Ufaransa kabla haijachapishwa.Ripoti hiyo inabainisha,kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la Uingereza,mwaka 1996 wakati vikosi vya Watutsi vikiwakimbiza Wahutu kuelekea Jamhuri ya Kimekrasia ya Kongo (wakati huo Zaire),na mwaka 1998 katika uvamizi wa kudhibiti waasi wa Kihutu,jeshi la Rwanda na washirika wake liliwazingira mamia ya wanaume,wanawake na watoto na kuwachinja kwa kutumia majembe na mashoka.Nyakati nyingine,"wakimbizi wa Kihutu walichinjwa kwa kutumia sime za bunduki,kuchomwa moto au kupigwa nyundo".Matukio hayo,inaeleza ripoti hiyo,ni sawa na mauami ya kimbari.
Serikali ya Rwanda amepinga madai ya ripoti hiyo,na inadaiwa imetishia kuondoa askari wake katika jeshi la kulinda amani huko Darfur na kwingineko,iwapo ripoti hiyo itawekwa hadharani rasmi.Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa ripoti ililyovuja ni rasimu (draft) tu.Inasubiriwa kuonwa kama jumuiya ya kimataifa itasalimu amri kwa shinikizo kutoka serikali ya Kagame kuondoa mpambano na kupunguza makali ya lugha katika chapisho timilifu (final version).
Imetafsiriwa kutoka Jarida la Newsweek
0 comments:
Post a Comment