Tuesday, 24 August 2010

Tangu tukio la mashambulizi ya kigaidi ya September 11 mwaka 2001,Marekani inaelekea kupata sababu nyingine ya kuhalalisha ubabe wake.Miongoni mwa wahanga wakubwa wa aftermath ya mashambulizi hayo ni Waislamu,ndani na nje ya nchi hiyo.

Hivi karibuni kumejitokeza mzozo kuhusu ujenzi wa kituo cha utamaduni cha Kiislamu karibu na eneo yalipokuwa majengo maarufu ya Twin Towers ambayo yalishambuliwa na magaidi kwa kubamizwa na ndege.Licha ya ukweli kuwa miongoni mwa waliofariki au kujeruhiwa ni Waislam,kwa Wamarekani wengi mashambulizi hayo yalikuwa kama tangazo la vita vipya kati yao na Waislam na Uislam.


Urais wa Barack Obama,ambaye mmoja wa wazazi wake alikuwa Muislam,ni kama umeongeza mafuta kwenye moto wa chuki dhidi ya Waislam.Katika kutambua uhuru na haki ya kila Mmarekani,Rais Obama aliweka msimamo wake hadharani kuwa anaunga mkono ujenzi wa kituo hicho cha kidini,kauli iliyopelekea upinzani mkubwa dhidi yake huku wengine wakimnyooeshea kidole kudai naye ni Muislam,kana kwamba kuwa muumini wa dini hiyo ni dhambi. 

Japo taifa hilo kubwa na lenye nguvu za kutosha limeendelea kudumisha misingi ya imani ya kidini (hususan Ukristo) matendo ya Wamarekani walio wengi hayana tofauti na waumini wa shetani.Sote tunatambua kuwa dini mbalimbali zinahamasisha amani,upendo na kusamehe waliotukosea.Sasa,hata kama Wamarekani wanaamini kuwa waliofanya mashambulizi hayo walitenda hivyo kutokana na imani yao ya Uislamu haimaanishi kuwa kila muumini wa dini hiyo aendelee kunyanyaswa kwa makosa ya wengine.Kimsingi,wengi wa magaidi wana asili au dini flani lakini hatuendelei kuwanyanyasa watu wengine ambao hawakushiriki katika vitendo vya ugaidi lakini wana asili au dini moja na magaidi husika.Wanaofanya mashambulizi ya kigaidi huko Ireland ya Kaskazini ni Wakatoliki na Waanglikana,lakini hatuhitimishi kuwa kila Mkatoliki au Muanglikana na gaidi.

Hata Marekani kama nchi imeshafanya unyama mkubwa sehemu mbalimbali duniani hususan katika zama za Vita Baridi kati yake na Urusi.Nani asiyejua mchango wa Wamarekani katika kifo cha Patrice Lumumba,au sapoti yao kwa Savimbi?Na nani asiyefahamu namna Wamarekani Weupe walivyojenga taifa hilo kwa biashara ya kinyama ya utumwa dhidi ya watu Weusi?Lakini hatumhukumu kila Mmarekani kuwa ni gaidi au mtwana mwenye kumiliki watumwa.

Yanayotokea sasa dhidi ya Waislamu ni mwendelezo tu wa hisia za ubaguzi zilivyoshamiri miongoni mwa Wamarekani walio wengi.Hadi leo,miaka kadhaa baada ya kuharamisha ubaguzi wa rangi,Wamarekani wasio Weupe wameendelea kubaguliwa kwa namna moja au nyingine.Again,urais wa Mmarekani Mweusi Obama umewasha upya moto wa ubaguzi wa rangi.

Japo siungi mkono ugaidi,ni dhahiri kuwa siasa za kinafiki za nchi hiyo zimechangia sana kuzalisha magaidi.Osama bin Laden,kiongozi wa mshambulizi ya September 11ni zao la mafunzo na ufadhili wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).Yayumkinika kuhitimisha kuwa tatizo la baadhi ya sera za mambo ya nje za Marekani ni ufupi wa upeo (short-sightedness).Katika zama za Vita Baridi,nchi hiyo iliona kuwa ni jambo mwafaka kufadhili mujahidina waliokuwa wanapambana na Urusi.Guess what?Mujahidina hao ndio Osama na Taliban wa leo!

Ungedhani kuwa nchi hiyo ingejifunza kutokana na foreign policy blunders zake kama hiyo ya kusapoti Mujahidina lakini wapi!Makosa kama hayo yameendelea kurudiwa huko Irak na Afghanistan pasipo kuangalia madhara ya muda mrefu.Licha ya sapoti kwa vikundi vinavyotarajiwa kuunga mkono harakati za Wamarekani,nchi hiyo imeendelea kutoa sapoti kwa baadhi ya tawala za kidikteta alimradi uimara wa tawala hizo ni kwa maslahi ya Marekani.Miongoni mwa marafiki wakubwa wa nchi hiyo ni pamoja na utawala wa kifalme wa Saudia na utawala wa kidikteta nchini Misri.Matokeo ya muda mrefu ya uswahiba huu ni kuibuka kwa upinzani wa ndani dhidi ya tawala hizo,ambao in long run unaweza kabisa kuwa na madhara kwa Marekani yenyewe.

Kadhalika,tawala hizo dhalimu zimechangia baadhi ya wananchi wao kukimbilia kwa vikundi vyenye misimamo mikali ya kidini ambayo inaonekana kwa wananchi hao kama yenye kuleta tumaini katika kuwapatia ufumbuzi wa matatizo yao.Kwenye sosholojia ya dini tunafundisha kuwa miongoni mwa sababu za kuwepo dini ni kimbilio la wenye shida.Tawala dhalimu zinaweza kuwa chanzo cha kuibuka na kushamiri kwa vikundi vyenye misimamo mikali ya kidini kwa vile wananchi wanaviona vikundi hivyo kama sehemu ya ufumbuzi wa matatizo yao.

Siasa za jino kwa jino na jicho kwa jicho,sambamba na kuendeleza ubaguzi kwa watu wasio na hatia ni hatari zaidi kwa usalama wa Marekani kuliko ujenzi wa kituo cha utamaduni kinachopigiwa kelele sasa.Actually,uwepo wa taasisi kama kituo hicho cha utamaduni unaweza kusaidia sana katika kujenga maelewano na mshikamo miongoni mwa Wamarekani pasipo kujali tofauti zao za kiimani.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget