Wednesday, 25 August 2010


Takukuru yakamata mgombea aliyejitoa
Adaiwa kuwa alishawishiwa kwa fedha
Awekwa chini ya ulinzi Makao Makuu Dar

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Makao Makuu jijini Dar es Salaam, imemkamata na kumhoji aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Jimbo la Musoma Vijijini, Michael Makenji, kwa tuhuma za kupokea rushwa.

Makenji anadaiwa kupokea Euro 1,000 (Sh. 1,850,000) kisha kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa Makenji alihojiwa na maofisa wa Takukuru juzi jioni kuhusiana na tuhuma hizo na kwamba hadi jana alikuwa akiendelea kushikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Makenji ni miongoni mwa wanachama wa Chadema waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea katika jimbo hilo, lakini hakurejesha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi hivyo jimbo hilo kubaki na mgombea pekee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nimrod Mkono (pichani mwenye kibandiko).

Habari zinaeleza kuwa Makenji baada ya kutorejesha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Musoma Vijijini, alikwenda katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, lakini baadaye baadhi ya wanaChadema walimtilia shaka kutokana na mawasiliano kati yake na baadhi ya watu.

Chanzo chetu cha uhakika kimebainisha kuwa, baada ya wanaChadema kumtilia shaka, walimuweka chini ya ulinzi na kukuta taarifa mbalimbali alizokuwa anatumiana na watu hao kupitia ujumbe mfupi wa simu.Taarifa za ndani ya Chadema zinasema kwamba baada ya mgombea huyo kuhojiwa na kupekua kwenye simu yake ya mkononi, alipatikana na ujumbe kadhaa zilizoashiria kwamba kulikuwa na mkono wa mtu katika kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge.

Miongoni mwa jumbe hizo (sms) ambazo ziko sehemu ya zilizotumwa zilisema:
“Mzee ameshanikatia tiketi ya kwenda Dar sasa muhimize amalizie kiasi kilichobaki maana hali yangu ya kiuchumi si nzuri.”
Nyingine ilisomeka: “Tumeshamaliza kama tulivyokubaliana.” Na mwingine ukisema: “Niko Makao Makuu ya Chama niko chini ya ulinzi.” Ujumbe huo ulionekana kujibiwa hivi: “Nani kakwambia uende huko watakuua. Siwezi kuja huko kukutetea.” Simu iliyotuma ujumbe huo unadaiwa ni ya kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho.

Chadema baada ya kuona hali imekuwa hivyo, waliamua kuwasiliana na Takukuru na baada ya muda mfupi, maofisa wa taasisi hiyo walifika na kumchukua Makenji.Hata hivyo, Takukuru haikuwa tayari kuthibitisha tukio hilo licha ya jitihada za NIPASHE kuwatafuta maofisa wake tangu juzi jioni.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, juzi jioni alisema alikuwa katika mkutano mjini Arusha na kuahidi kuwa angepiga simu baadaye kutoa ufafanuzi. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni hakufanya hivyo.

Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwaya, jana alisema kuwa maofisa wa Makao Makuu wangeweza kulizungumzia, lakini mwandishi wetu alipokwenda katika ofisi hizo, aliambiwa kuwa ofisa anayeshughulikia kesi hiyo alikuwa katika kikao.

Hata hivyo, ofisa huyo aliyetambulika kwa jina moja la Kassim, alipoulizwa baadaye jioni, alisema: “Sina comment (sina la kusema) katika hilo, labda kama ungefuata zile taratibu zetu za kila siku kwa kupitia kwa ofisa Uhusiano wetu hadi kwa Mkurugenzi Mkuu.”

Dk. Hoseah alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu majira ya saa 18:20 jana jioni, alisema: “Sina taarifa, kwa sasa nipo nje ya Dar es Salaam, nani amekuambia hayo.”

Uongozi wa Chadema ulipoulizwa kuhusiana na taarifa hizo, ulithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kwamba mtuhumiwa (Makenja) alikiri kupewa kiasi hicho cha pesa.

“Kimsingi ni kwamba Idara yetu ya Ulinzi na Usalama ilimhoji mgombea wetu na akakiri kupewa fedha hizo, tena kwa maandishi ndipo tukawasiliana na Takukuru kwa hatua zaidi…lakini tunawasiliana na mamlaka mbalimbali ili kuona hatua stahili za kumchukulia kwa sababu amekiuka kanuni na sheria za uchaguzi,” alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Kufuatia hali hiyo, Mnyika alisema chama hicho kimelazimika kuwaandikia barua wagombea wake ambao hawakurudisha fomu ili kujua tatizo lililokwamisha kufanya hivyo.Alisema chama kimeamua kuchukua hatua hiyo ili kubaini kama kinafanyiwa hujuma na kwamba watakaobainika kutorudisha fomu makusudi, kitawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

CHANZO: Nipashe

2 comments:

  1. Inasikitisha sana, tena sana, kwa chama kikongwe kama ccm kuwa na watu kama akina mkono.Lakini watu waangalie historia ya huyu binadamu anayeitwa Mkono. Huyu ni kati ya mapapa wa ufisadi 10 ambao Mengi hajamaliza ile list.

    ReplyDelete
  2. Tanzania bila kuwa na wazalendo wakweli wasioyumbishwa na hela haiwezi kujikomboa.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget