Thursday, 9 September 2010

Image and video hosting by TinyPic
Waandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewazuia wagombea wake wa ubunge kushiriki katika mdahalo unaoendeshwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kuhusisha wagombea wa vyama vyote katika kila jimbo.
Kipindi hicho kinarushwa kila Jumanne kupitia Kituo cha Televisheni cha TBC1 kwa lengo la kuwasikiliza wagombea wakijinadi pamoja na kunadi sera za vyama vyao.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa wagombea wa CCM wamezuiwa kushiriki mdahalo huo kwa barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa chama hicho,Yusuf Makamba kwenda kwa makatibu wa chama wa wilaya na mikoa yote nchini.

"Ninawaandikia kuwajulisha kwamba, wagombea wetu wasishiriki katika aina hiyo ya mdahalo, mpaka hapo mtakapoelezwa vinginevyo.” imesema sehemu ya barua hiyo ambayo nakala yake imepelekwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC.

Hata hivyo tayari wagombea kadhaa wa ubunge wa CCM wameshiriki kipindi hicho kilichoanza kurushwa hewani mbili zilizopita kwa kuwakutanisha wagombea ubunge wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Baadhi ya wagombea ubunge wa CCM waliokwisha shiriki mdahalo huo ni pamoja na Hawa Ngh’umbi wa Jimbo la Ubungo na Chrispin Meela anayegombea ubunge katika jimbo la Vunjo.
"Kipindi hicho kimerushwa hewani kwa mara ya kwanza katika Jimbo la Ubungo Dar es Salaam na mgombea wa CCM alishiriki, sijui kwa maelekezo ya nani. Sina tatizo na kipindi. Nina tatizo na ushiriki wetu," ainasema sehemu ya barua hiyo ya Katibu Mkuu.

Katika kipindi hicho wagombea ubunge wa vyama mbalimbali huulizwa maswali na wasikilizaji na watazamaji wanahudhuria katika mdahalo huo.

Kipindi hicho kiliporushwa kwa mara ya kwanza katika Jimbo la Ubungo, mgombea wa CCM (Hawa Ngh’umbi )alipata wakati mgumu kujibu maswali ya watazamaji wa kipindi hicho na kuishia kupandwa na jazba nakutishia kumshitaki, mtu aliyemuliza swali gumu.

Katika barua yake hiyo ya Agosti 31, mwaka huu, Makamba licha ya kukitilia mashaka kipindi hicho na alihoji mgombea wao wa Ubungo alishiriki kwenye mdhahalo huo kwa maelekezo ya nani.
Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kwamba agizo hilo la Makamba limeanza kutekelezwa, juzi mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Arusha Mjini, Batilda Buriania hakushiriki kipindi hicho.

Hata hivyo, Batilda alisema hakuhudhuria mdahalo wa Arusha kutokana na chama chake kutopewa taarifa na yeye ni mgombea wa CCM sio mgombea binafsi.


“Nimekuwa nikitumiwa ujumbe wa simu kuwa nimeingia mitini katika mdahalo…mimi siwezi kuingia mitini nimedhuria midahalo mikubwa tena ya kimataifa ndani na nje ya nchi siwezi kukimbia hivi sasa,”alisema Dk Batilda.

Barua hiyo yenye kumbukumbu namba CCM/OND/SG/194/9 ya Agosti 31 ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona, Makamba aliwaambia makatibu hao wa CCM kuwa wagombea wote wa chama hich wasishiriki kipindi hicho hadi CCM itakapotafakari kwa kina manufaa itakayopata kwa kushiriki kwao
Alisisitiza kuwa CCM ina utaratibu wake wa kujinadi na kunadi sera zake kwa wananchi ambao anaamini kuwa bado unakidhi haja.

“Tuna utaratibu mzuri wa kijinadi na kunadi sera zetu kwa wananchi; utaratibu wa mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani. Utaratibu huo bado unakidhi haja. Tunaendelea nao,” alisema Makamba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamba alisisitiza akisema: "Hatutaki. Tumekataa ndio. Sisi yetu ni mikutamo ya hadhara. Tutaeleza huko malengo, ilani yetu na sera zetu kwa wananchi. Hatuoni sababu ya kukaa katika chumba kidogo na kuwapa nafasi ya ushiriki watu wachache."

Aliendelea: "Hatuoni sababu ya kwenda kwenye huo mjadala kwa kuwa mikutano yetu ya hadhara inajitosheleza."

Alipotakiwa kueleza kama chama kitawachukulia hatua wagombea wake waliokwishashiriki kipindi hicho, Makamba alijibu: "Hakuna adhabu watakayochukuliwa kwa sababu chama kilikuwa hakijatoa maagizo."

Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilieleza kwamba, agizo hilo la Makamba pia limepokelewa katika jimboni Karatu ambako mgombea ubunge wa CCM aliamua kujitoa kwenye mdahalo huo juzi.

Mdahalo wa wagombea wa jimbo hilo, ulipangwa kufanyika juzi katika ukumbi wa maendeleo Karatu, lakini wakati wagombea wengine wakiwa wanajiandaa, taarifa zilitolewa kuwa mgombea wa CCM, Dk Wilbard Lorry hawezi kuhudhuria.

Viongozi wa vyama vya Chadema na CUF, katika wilaya hiyo, walilalamikia kuahirishwa ghafla kwa mdahalo huo wakati walikuwa wamesitisha kampeni vijijini na kurudi Karatu.

Katibu wa CUF Wilaya ya Karatu, Stivin Siay alisema chama chao kilikuwa kimemwandaa mgombea wake kwa mdahalo huo.

“Tunashangaa kujiondoa kwa CCM katika mdahalo huu kumesababisha mdahalo kuahirishwa…,” alisema Siay.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe alisema walipata taarifa za kuahirishwa mdahalo huo dakika za mwisho kwa maelezo kuwa mgombea wa CCM hatahudhuria.

Alisema taarifa hizo kwanza zilipatikana ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, ambao ndio awali walitoa taarifa za kuwepo maombi ya TBC kuandaa mdahalo huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Karatu, Clemence Berege akizungumzia kuahirishwa kwa mdahalo huo alisema kwamba, ofisi yake haihusiki kwani waliotaka kuendesha mdahalo huo ni TBC.

Habari hii imeandaliwa na Mussa Juma, Arusha na Exuper Kachenje

Chanzo: Mwananchi

1 comment:

  1. nashukuru ndugu yangu kuliona hili, siyo blog zingine kutwa kuchwa kuwaweka watoto wa hawa vibosile. tatizo ukitofautiana na kikwete utachezewa na rafu na chma kizima.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget