UTITIRI WA AHADI ZA KIKWETE NI KAMA UTAMU WA PIPI HIZO ANAZOMPATIA MTOTO HUYO PICHANI.PIPI NI TAMU KADRI INAVYOYEYUKA MDOMONI LAKINI SIO TU HAIDUMU BALI HAIONDOI NJAA. |
Hebu soma kwanza nukuu hii hapa chini kisha utaelewa kwanini nimeweka kichwa cha habari hicho hapo juu
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya kazi kubwa itakayofanywa na serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kumsaidia mkulima wa Tanzania aweze kulima kwa kutumia trekta badala ya jembe la mkono.
Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kata ya Lyabukande, jimbo la Solwa wilayani Shinyanga katika moja ya mikutano yake ya kampeni iliyofanyika jana.
“Katika miaka mitano ijayo iwapo mtatupa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, tumepanga kumsaidia mkulima ili aweze kuboresha kilimo chake kwa kumwezesha kulima kwa trekta badala ya jembe la mkono alilolizoea enzi na enzi,” alieleza Rais Kikwete.
Alisema iwapo mkulima atasaidiwa katika kilimo chake, ataweza kujikomboa kutokana na umasikini na kumuwezesha kuwa na maisha bora kama ambavyo sera ya CCM inavyoelekeza.
CHANZO: Majira
Sio siri,inaudhi,inakera na inachukiza.Hivi huyu Jakaya Kikwete siye aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2005 hadi leo hii?Ofkozi,jibu ni ndiyo.Sasa hizi habari za kusema atamsaidia mkulima kuondokana na jembe la mkono kwanini ziwe leo na sio mwaka 2005 au 2006 au 2007 au 2008 au 2009 au hata mapema mwaka huu?
Kwa kweli kama kuna Watanzania bado wanajishauri kuhusu wampigie au wamnyime kura Kikwete basi utitiri wa ahadi anazoendelea kutoa,huku nyingi zikiwa ni marejeo ya alizotoa wakati wa kampeni zake za mwaka 2005 ni sababu moja kati ya maelfu ya sababu ya kustaafisha urais kwa kumyima kura.Tena huyu hapaswi kushindwa kwa tofauti ya kura chache bali stahili yake ni kile kiitwacho anguko la pua.
Hakuna maelezo mengine zaidi ya kuamini kuwa Kikwete anawafanya Watanzania ni wapumbavu maana vinginevyo asingediriki kuongea upuuzi kama huu wa kuahidi kuwakomboa wakulima eti akipewa miaka mingine mitano ilhali hii anayomaliza ameitumia zaidi kuzurura huko nje ya nchi.Na kwa angalizo tu,huyu mtu amezowea sana kusafiri,sasa kwa vile amelazimika kukaa nchini kwa zaidi ya miezi miwili sasa basi wapiga kura mkirogwa tu kumrejesha atafanya utalii wake kwa hasira,perhaps on weekly basis badala ya monthly basis kama tulivyozowea.
Badala ya kuwaomba msamaha wakulima kwa kuwapuuza kwa muda wote aliokuwa madarakani yeye anakuja na hadithi mpya kuwa anadhamiria kuwatoa kwenye kilimo cha jembe la mkono.Hayo matrekta hewa yatanunuliwa kwa fedha zipi ilhali priority ya serikali yake ni ununuzi wa magari ya kifahari na samani za bei mbaya kwa watawala?
Na wakulima wakishapatiwa matrekta,je ziada ya mazao yao itauzwa wapi ilhali vyama vya ushirika vimeendelea kuwa taasisi maalum za kuwafisadi wakulima?Kama kweli alikuwa na nia ya kuona mkulima anaondokana na jembe la mkono kwanini basi zile fedha "zilizorejeshwa" na mafisadi wa EPA hazikutumiwa kwa dhamira hiyo?Lakini kwa kuonyesha kuwa anawazuga tu wakulima,alipotangaza "stimulus package" ya kisanii,waliopewa kipaumbele ni wafanyabiashara huku wakulima wakisahaulika.
Naomba nisiandike zaidi.Kikwete ni mbabaishaji na hana jipya.Haihitaji majini ya Sheikh Yahya kufahamu kuwa ahadi alizokwishatoa hadi sasa zinahitaji awe rais wa maisha ili atekeleze japo nusu ya ahadi hizo.Haiwezekani kutoa ahadi kila kukicha ilhali kuna lundo la ahadi zinazosubiri utekelezaji.
Chonde chonde Watanzania,kumbukeni kuwa kama Kikwete ameweza kufanya masihara katika awamu yake ya kwanza huku akijua fika kuwa mwishoni mwa awamu hiyo angesimama tena majukwaani kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena,pata picha awamu yake ya pili ambapo hatohitaji tena kura itakuwaje!Tafakari maneno haya kwa makini sana kwa sababu pindi mtu huyu akirejea Ikulu basi sote tumeliwa.Kidogo kilichobaki kitakombwa na kukwanguliwa kabisa.Na kwa namna ufisadi ulivyoshamiri katika awamu yake ya kwanza basi yayumkinika kubashiri kuwa pindi akichaguliwa tena (God forbid) basi si ajabu Watanzania kushtukia nchi yetu imeshauzwa na hatuna pa kwenda.
Bahati nzuri,katika uchaguzi wa mwaka huu hatuna tena tatizo lililokuwa likitukwaza hata kufikiria mbadala wa CCM.Zama hizo tulikuwa tunasema "sasa tusipoichagua CCM tukichague chama gani ilhali vyama vyenyewe ni bora ya hiyo CCM".Mwaka huu Mungu amesikiliza kilio chetu na kutupatia ufumbuzi mapemaaa.Tumeletewa Dokta Wilbroad Slaa,mwanasiasa ambaye kwa hakika amejidhihirisha bayana kuwa ana uchungu wa dhati kwa Tanzania na Watanzania.
TANZANIA BILA UFISADI INAWEZEKANA.TANZANIA BILA MAFISADI WANAOLINDWA NA KUPIGIWA KAMPENI NA KIKWETE INAWEZEKANA PIA.MPE KURA YAKO DOKTA SLAA NA MPATIE WABUNGE WA KUTOSHA WA KUUNDA SERIKALI NDOGO YA UFANISI NA YA UKOMBOZI WA MTANZANIA.