Saturday, 6 December 2008


UTATA wa zilipo fedha zilizorejeshwa na kampuni zilizoiba fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), umeendelea kuigubika nchi, baada ya kubainika kuwa fedha hizo hazijaingizwa kwenye mfuko ulioelekezwa na Rais Jakaya Kikwete wakati akilihutubia Bunge, Agosti 21 mwaka huu.

Fedha hizo ambazo ni zaidi ya sh bilioni 70, zilitakiwa ziende Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), ambapo zingefunguliwa dirisha maalumu, lenye jukumu la kutoa mikopo kwa wakulima ambao kwa miaka mingi wamekosa fursa hiyo.

Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumapili, umebaini kuwa fedha hizo zimehifadhiwa katika akaunti maalumu ambayo mpaka hivi sasa maelezo yake bado yamegubikwa na utata, kwa sababu kila ofisa wa Wizara ya Fedha na Uchumi aliyeulizwa juu ya akaunti hiyo, ameshindwa kutoa jibu linaloeleweka.

Tangu awali baadhi ya watu walionyesha wasiwasi wao kuhusu urejeshaji wa fedha hizo kama ni kweli zimerejeshwa au ilikuwa mbinu ya kisiasa ya serikali kutaka kuzima joto la wananchi, wapinzani na wahisani waliotaka fedha hizo zirejeshwe na watuhumiwa wafikishwe katika mikono ya sheria.

Watu hao waliweka wazi msimamo wao kuwa fedha hizo hazikurejeshwa bali ilikuwa ni janja ya serikali ili waweze kupata misaada kutoka kwa wafadhili ambao awali walitishia kutochangia bajeti ya serikali mpaka majibu sahihi na hatua za wizi wa EPA zichukuliwe.

Shinikizo hilo inadaiwa ndilo lililomfanya Rais Jakaya Kikwete kuamua kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali, pamoja na kuunda timu ya uchunguzi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, baada ya mkaguzi wa nje, Ernst & Young, kuthibitisha kuwapo kwa wizi katika akaunti hiyo, unaofikia kiasi cha sh bilioni 133.

Mkurugenzi wa Benki ya Rasilimali (TIB), William Mlaki, hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari kuwa fedha hizo hadi sasa hawajazipokea.

Alisema inawezekana serikali inajiandaa kuwapelekea fedha hizo ambazo Rais Jakaya Kikwete alishaweka wazi dhamira ya serikali yake kuzipeleka TIB ili ziwasaidie wakulima.

“Mpaka sasa fedha za EPA, bado hazijaingia kwetu na si jukumu letu kuulizia fedha hizo zitakuja lini, kazi yetu ni kuzipokea na kuratibu zoezi la utoaji mikopo kwa wakulima,” alikaririwa Mlaki.

Kauli hiyo ya Mlaki, inazidisha utata kuhusu ukweli wa urejeshaji wa fedha za EPA ambazo uchotwaji wake unahusishwa na matumizi ya uchaguzi mkuu uliopita.

Inadaiwa kuwa mbinu za kuchota fedha hizo, zilifanywa na viongozi wa juu wa Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kushirikiana na mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu nchini ili zikisaidie Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu uliopita.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, tena kwa nyakati tofauti, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba na Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha, Amos Makala, wamekanusha chama chao kuhusishwa na wizi huo.

Mfanyabiashara huyo ndiye anayeaminika alikuwa mmiliki halali wa Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyochota sh bilioni 40, lakini hadi hivi sasa hajafikishwa mahakamani au kutajwa mbele ya umma.

Kutotajwa kwa mfanyabiashara huyo kunatokana na ukweli kuwa ndiye anayejua siri yote ya Kagoda na viongozi waliomuagiza kuzichota fedha hizo na hata matumizi yake pamoja na kujua nani kapata kiasi gani na kwa kazi gani.

Kwa hali ilivyo, Kagoda ndiyo kampuni inayoonekana kuitikisa nchi kama wamiliki wake watatajwa na kufikishwa mahakamani, kwani hawatakubali kushitakiwa peke yao bila kuwataja viongozi waliowatuma kufanya wizi huo.

Hali hiyo ndiyo iliyomfanya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji, kutoa ufafanuzi kwa umma kuwa fedha zilizochotwa zilitumika kwa mambo ya usalama na si ufisadi kama ambavyo baadhi ya wanasiasa, akiwemo Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, walivyokuwa wakisema.

Msumari wa moto juu ya utata wa urejeshwaji wa fedha za EPA na ufisadi hivi karibuni ulishindiliwa na mfanyabiashara maarufu nchini na mwachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jafar Sabodo, ambaye alisema serikali inafanya mchezo wa kuigiza na haina nia thabiti ya kutatua matatizo ya rushwa.

Sabodo ambaye ni rafiki wa karibu wa marehemu Mwalimu Nyerere na mfadhili wa mfuko wa taasisi ya Mwalimu Nyerere na CCM, alifikia hatua ya kusema yuko tayari kukisaidia chama chochote cha upinzani katika uchaguzi ujao, kuiangusha CCM madarakani, kwa madai kuwa imeshindwa kuondoa tatizo la rushwa nchini.

Wachambuzi wa masula ya siasa wanadai kupandishwa mahakamani kwa mawaziri wawili ya serikali iliyopita Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona ((Nishati na Madini), ni mpango wa kuwasahaulisha wananchi juu ya mwenendo wa kesi ya EPA, hasa kuendelea kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa wengine.

Mpango huo uliasisiwa kutokana na joto la wananchi kutaka wamiliki wa Kampuni ya Kagoda inayohusishwa na wafanyabiashara, wanasiasa maarufu na wakongwe nchini, kuzidi kushika kasi kiasi cha kumfanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuweka bayana kuwa joto hilo likizidi, wamiliki wake watajulikana.

Wadadisi hao wanaendelea kubainisha kuwa mpango huo kwa kiasi fulani, umefanikiwa, kwani watu walihamisha macho na masikio yao kutoka EPA na kuhamia kwa Yona na Mramba, ambao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salam kwa kosa la kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya sh bilioni 11.7, kwa kutoa misamaha ya kodi kiholela katika sekta ya madini.

Wakati wingu zito likiwa limetanda kuhusu mahali zilipo fedha za EPA, kuna tetesi kwamba fedha hizo ndizo zilizotumika kulipa madai ya walimu ambao miezi miwili iliyopita walitishia kugoma nchi nzima kushinikiza kulipwa fedha zao za malimbikizo zinazofikia sh bilioni 16.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget