Picha (for illustrative purpose only) kwa hisani ya MWANAKIJIJI.
MAPIGANO ya koo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, yameingia katika sura mpya baada ya kubainika watu wanaodaiwa kuwa askari wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutumia silaha, sare za Jeshi hilo na mbinu mbalimbali ili kuhakikisha koo wanazotoka zinashinda.
Baada ya kugundulika kwa matumizi hayo ya vifaa vya JWTZ, Polisi mkoa wa Mara imeanzisha operesheni kali na limewafanikiwa kukamata bunduki tatu, risasi 56 na sare mbalimbali za Jeshi, ambazo zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya watu katika mapigano ya koo za Wairegi na Wanyabasi wilayani Tarime.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Bw. Deusdedit Kato, alisema jana kuwa silaha hizo ndizo zilizotumika katika mapigano hayo juzi na kuua watu wawili kwa risasi.
Alisema ingawa bado haijathibitishwa kuwa wamiliki wa silaha hizo kinyume cha sheria ni askari wastaafu wa JWTZ, lakini kuna ukweli huo kutokana na taarifa za awali na wamekuwa pia wakiendesha mafunzo kwa vijana hili kumudu mapambano hayo ya koo.
Alisema katika operesheni hiyo inayoendeshwa na Polisi, limeweza kukamata bunduki mbili aina ya shotgun namba 979256 na 85084 na risasi 56 zinazomilikiwa kinyume cha sheria nyumbani kwa Bw. Samwel Range wa kijiji cha Magoto ambaye alikimbia kabla ya kukamatwa.
Kamanda Kato alisema katika upekuzi huo, pia polisi walikamata sare za JWTZ kama vile half sack (2), kit bags (6), suruali za JWTZ (2), suruali za JKT (2) na shati aina ya kombati moja ya JWTZ ambazo zimekuwa zikitumiwa katika mapigano ya koo na matukio mengine ya uhalifu.
Alisema katika upekuzi mwingine uliofanyika nyumbani kwa Bw. Samwel Magabe, askari hao wa Polisi walikamata bunduki nyingine aina ya shotgun 978862 CAR 151 ambayo pia inasadikiwa kutumika katika mapigano ya koo hizo mbili katika kata ya Nyamwaga.
Kamanda Kato ambaye pia ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) wa Mara, alisema pia viongozi wawili wa kijiji cha Magoto wamekatwa baada ya kudaiwa kuchochea mapigano hayo ya koo.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Bw. Gabriel Matiku, ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho na Bw. Charles Chacha, Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho na hivi sasa wanahojiwa na Polisi Tarime kabla ya kufikishwa mahakamani.
“Vita hii ya koo katika wilaya ya Tarime, kwa kweli inatuumiza vichwa kwani baadhi ya viongozi pia wanahusika, sasa lazima tufanye uchunguzi na hatutashindwa kuwachukulia hatua viongozi wote wanaodaiwa kuwa wachochezi,” alisema Kamanda Kato.
Katika mapigano hayo ambayo kwa sasa yameanza kudhibitiwa na polisi waliosambazwa katika vijiji vya Nyamwaga na Magoto, watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na kutajwa kuwa ni Bw. Girasi Marwa na Bw. Samwel Chacha wote wakazi wa Nyamwaga kutoka koo ya Wairegi.
Wilaya ya Tarime imekumbwa na vita vya koo kwa muda sasa na watu kadhaa kuuawa kwa mishale, kukatwa mapanga, kuchomwa moto na wengine kupigwa risasi, huku mali na nyumba zikiteketezwa kwa moto kwa kuhusisha koo za Wakira, Waanchari na Warechoka katika kata za Susuni na Sirari, wakati mapigano kama hayo pia yamekuwa yakiibuka katika kata ya Bumera kwa kuhusisha koo za Wahunyaga na Wamera.
Chanzo kikuu cha mapigano hayo kimekuwa kikitajwa kuwa ni wizi wa mifugo, mipaka ya ardhi na kilimo cha bangi.
CHANZO:Majira
MAUAJI YA DHIDI YA ALBINO YAMESHINDWA KUDHIBITIWA,NA HAKUNA ANAEWAJIBIKA.MAPIGANO YA KOO HUKO TARIME YAMEKUWA YAKIENDELEA KWA MUDA MREFU SASA NA ENEO HILO LIMEGEUKA MITHILI YA ENEO LISILOTAWALIKA LA MPAKA KATI YA PAKISTAN NA AFGHANISTAN.AGAIN,HAKUNA ANAYEWAJIBIKA KUTOKANA NA MAPIGANO HAYO HUKO TARIME.NA KAMA KAWAIDA YETU,TUNASUBIRI MOTO UWE NJE YA UWEZO WA ZIMAMOTO NDIO TUANZE KUUZIMA KWA MIKONO.
0 comments:
Post a Comment