KAMPUNI iliyopewa jukumu la kusimamia na kutunza mali za lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (RAHCO), imeanza kukatakata injini 27 na mabehewa 19 ili yauzwe kama chuma chakavu.
Mabehewa hayo na injini zake yanadaiwa yalikuwa na hali nzuri, lakini mwekezaji akayakataa wakati anachukua shirika kwa maelezo kuwa hayamfai.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya mwekezaji Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kudai kuwa, mabehewa hayo yalikuwa yamechakaa zaidi na hayawezi kutumiwa tena, huku Rahco ikidai kuwa yalikuwa yanafaa kuendelea kutumika.
Tayari zabuni ya kupata makampuni ya kununua vyuma hivyo chakavu imeshafanyika na washindi kupatikana.
Makampuni ambayo yameshinda zabuni yameshaanza kukata mabehewa hayo na injini katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tabora na Kigoma.
Mwananchi Jumapili wiki hii ilishuhudia baadhi ya mafundi wa kampuni iliyoshinda zabuni wakikata mabehewa yaliyopo katika Stesheni ya Dar es Salaam.
Meneja Uhusiano wa RAHCO, Musita John aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa, wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kushindwa kuzifanyia kazi injini hizo na mabehewa.
Alisema kuwa endapo injini hizo na mabehewa zingefanyiwa ukarabati mdogo zingeendelea kuisaidia kampuni hiyo kupunguza matatizo ya usafiri lakini mwekezaji hakuzikubali.
John alisema wakati mwekezaji anachukua shirika hilo alikuta jumla ya injini 116 na 92 kati yake zilikuwa zinafanya kazi, lakini yeye aliamua kuchukuwa 79 tu na zingine akazikataa kwa madai kwamba hazimfai.
Alisema mbali na injini hizo, pia alikuta jumla ya mabehewa ya abiria 164, yaliyokuwa yanafanya kazi ni 125, lakini yeye aliamua kuchukuwa mabehewa 106 tu na 19 yaliyobaki aliyakataa.
John alifafanua kwamba baada ya mwekezaji huyo kumaliza tathimini ya mali za TRC alizokuta kabla hajaanza kazi waliamua kuziweka katika madaraja mbalimbali, ambapo daraja (A) lilikuwa ni mabehewa na injini yaliyokuwa yanafanya kazi.
Alisema Daraja (B) lilikuwa ni la mabehewa na injini zilizokuwa zinahitaji matengenezo madogo, ingawa yalikuwa bado yanaendelea na kazi ya kusafirisha abiria na mizigo wakati daraja (C) ni yale ambayo alikuta yameondolewa kazini, baada ya kuharibika na kupelekwa kwenye karakana ili yafanyiwe ukarabati, lakini pia aliyakataa kwa madai kwamba hayamfai.
Aliongeza kuwa kulikuwa na daraja (D) ambalo lilihusisha injini na mabehewa yaliyoharibika, yasiyofaa kutumika na daraja E ni yale ambayo yalishakaguliwa na kubainika kwamba, yalishafikia katika kiwango cha vyuma chakavu.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya TRL, zinaeleza kwamba mbali na injini na mabehewa hayo, mali zingine ambazo mwekezaji huyo alizikataa ni vifaa vya ofisini ambavyo hivi sasa pia viko katika orodha ya vitu vinavyouzwa na RAHCO kama vyuma chakavu.
Wakati RAHCO ikiendelea kukatakata injini hizo na mabehewa TRL hivi sasa inadaiwa kuwa katika hali mbaya kutokana na baadhi ya injini zake aina ya ‘73 class’ zilizokodishwa kutoka India kuwa na uwezo mdogo wa kuvuta mzigo, kiasi kwamba wanalazimika kuziunganisha mbili ndipo ziweze kuvuta mzigo ambao ungevutwa na injini moja aina ‘88 class’ za Tanzania alizozikataa.
Meneja Uhusiano wa TRL, Midlajy Maez alipotakiwa kutoa ufafanuzi wake kuhusiana na suala hilo alisema wanaotakiwa kulizunguzia ni RAHCO.
CHANZO:Mwananchi
HIVI KWANINI TUNAENDELEA KUWANG'ANG'ANIA HAWA WABABAISHAJI WA KIDOSI?JIBU JEPESI NI KWAMBA WALIOWAKARIBISHA NI WABABISHAJI WENZAO,SO SIO RAHISI KWAO KUONA UBABAISHAJI ULIOPO.TUNA WAZIRI,NAIBU WAZIRI,KATIBU MKUU,NAIBU KATIKA MKUU,MKURUGENZI,NK,NK,NK WOTE KATIKA WIZARA HUSIKA.HAWA WANALIPWA MSHAHARA NA MARUPURUPU MENGINE KUTOKA KWA WALIPA KODI WA TANZANIA LAKINI SIJUI WANASHINDWA NINI KUCHUKUA HATUA STAHILI DHIDI YA USANII HUU ULIOPEWA JINA LA UWEKEZAJI.MWEKEZAJI GANI AMBAYE ILI ALIPE MSHAHARA KWA WAAJIRIWA WAKE NI LAZIMA APEWE TAFU NA SERIKALI?
KAMA KAWAIDA,JAMAA WATAHARIBU RELI WEE MPAKA IWE TOO MUCH THEN WATAINGIA MITINI,AU MZEMBE FLANI ATAKURUPUKA USINGIZINI NA KUDAI IUNDWE TUME YA UCHUNGUZI (ISOMEKE TUME YA KULA FEDHA ZA VIKAO) LAKINI WAKATI HUO HUDUMA YA RELI YA KATI ITAKUWA IMEKUFA KABISA.CALL IT MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA AS WE ARE APPROACHING 2009!
0 comments:
Post a Comment