Saturday, 28 May 2011



Ilikuwa dakika,masaa,siku,wiki,mwezi,miezi,mwaka na sasa ni mwaka wa tatu tangu mama yangu mpendwa Adelina Mapango alipotuacha na majonzi ambayo kamwe hayatafutika.

Mara ya mwisho kuonana na mama akiwa hai ni mwaka 2005 nilipokwenda nyumbani kwa ajili ya fieldwork yangu.Novemba mwaka huo,ndoa ya Baba Mzee Philemon Chahali na Mama ilitimiza miaka 50,yaani nusu karne.Niliwarekodi kwenye video na kila ninapojaribu kuangalia mkanda huo naishia kububujikwa na machozi.Bila kujua kuwa ananiachia wosia,mama alisisitiza sana kuhusu upendo.Aliniambia kuwa nikiwa mcha Mungu nitaweza kuwapenda watu wote.Alinisisitiza kumtanguliza Mungu katika kila nifanyalo.Alininiambia pia kuwa zawadi kubwa nitakayoweza kumpa yeye na mumewe ni kufanikiwa katika masomo na maisha yangu kwa ujumla,kuwatunza wazazi na ndugu zangu,kwathamini marafiki na jamaa zangu,kuheshimu kazi na pindi nikioa,nimpe upendo mke wangu na watoto kama ambavyo yeye na baba walivyonipenda.

Mama alikuwa na upendo usioelezeka.Nakumbuka nikiwa mdogo huko Kigoma timu ya Pan Africa ilifanya ziara huko.Wakati huo,binamu yangu Gordian Mapango alikuwa bado anacheza mpira (kama winga machachari wa Pan Africa).Basi Gordian alikuja kututembelea nyumbani akiwa na rafiki zake marehemu Ibrahimu Kiswabi na mchezaji mwingine jina limenitoka.Walipoingia tu ndani mama akakaa chini na kumpakata Gordian kama mwanae mchanga vile.Japo nilikuwa mdogo lakini bado nakumbuka jinsi marehemu Kiswabi na yule mchzaji mwingine walivyoguswa na upendo wa mama kwa mtoto wa kaka yake (Gordian).

Kwa vile mwaka 2005 nilikaa Tanzania kwa takriban miezi sita hivi,nilikuwa nikienda nyumbani Ifakara mara kwa mara,kila nilipopata fursa nje ya fieldwork yangu.Kila nilipokuwa hapo nyumbani mama alisisitiza kunichemshia maji ya kuoga,kunifulia na kunitunza kama mtoto mchanga.Mama,upendo ulionipa nitaendelea kuukumbuka hadi naungana nawe huko uliko.

Nilimeshahudhuria misiba mbalimbali lakini kufiwa na mzazi ni kitu kisichoelezeka.Nakumbuka nilikuwa Kinondoni Mtaa wa Isisi pamoja na binamu yangu Gordian na marafiki wengine,na majira ya saa 4.30 usiku nikapigiwa simu kutoka Ifakara (maana wakati huo nilikuwa Dar kwa muda).Ile kupokea tu nikamsikia sista (wa kanisani) aliyekuwa mmoja ya masista waliokuwa wanamsaidia sista mwenzao (mdogo wangu) Sr Maria-Solana kumuuguza mama.Huku akilia,sista huyo akaniambia "Kaka Evarist,mama hatunaye".Nikamuuliza "unamaanisha nini?"Akaendela kusema "mama hatunaye,ametutoka".Nikawa kama nimepigwa ganzi vile.Yani ilinichukua kama nusu saa hivi,baada ya kuondoka Kinondoni na kurejea Sinza (nilipokuwa nimefikia)
 kupata fahamu kuwa hatimaye mama yangu mpendwa Adelina Mapango amefariki.

Niliongea na mama mara ya mwisho mwezi Februari 2008.Nilipiga simu nilipopata taarifa kuwa mama mkubwa (dada yake mama) alikuwa amefariki.Japo hali ya mama wakati huo haikuwa nzuri sana,alisistiza kuwa lazima aende kumzika dada yake.Nikamsihi mama kuwa kwa hali aliyonayo,na kwa jinsi alivyompenda dada yake,ni vema asiende msibani.Kumbe siku hiyo ndio nilikuwa naongea nae kwa mara ya mwisho.Siku chache baadaye akapata stroke na akapoteza fahamu.Wiki chache baadaye nikaenda Tanzania kumuuguza lakini kwa bahati mbaya hadi anafariki hakuweza kufumbua mdomo kuongea nami.

Kinachonitia uchungu hadi leo ni ukweli kwamba siku nilipomtembelea hospitalini Muhimbili baada ya kufika Dar alitoa kama tabasamu hivi.Hata baadhi ya manesi na ndugu waliokuwa wanamuuguza wakasema inaelekea mama amefurahi mwanae nimekwenda kumuuguza.Niliendelea kuwa na matumaini kuwa ipo siku atapata fahamu na hatimaye kurejea kwenye hali yake ya kawaida.Kwa bahati mbaya haikutokea hivyo hadi anafariki.
Kwa kweli bado nina uchungu mkubwa sana.Kuzidisha machungu hayo ni ndoto za mara kwa mara ambapo mama namuona mama.Pengine ni kwa vile namuwaza sana,au pengine ni kwa vile alifariki bila kuniambia chochote.Majonzi niliyonayo moyoni hayaelezeki.

Kuna tatizo jingine.Wakati mama anafariki,baba alikuwa amemzidi kama miaka 10 hivi.Ikumbukwe pia kuwa walikuwa kwenye ndoa kwa miaka 53 wakati mama anafariki.Sasa baba hadi leo hii anaendelea kuona kama yeye ndiye alistahili kutangulia kabla ya mkewe kwa vile alikuwa amemzidi umri.Baba na marehemu mama walikuwa zaidi ya mke na mume.Walikuwa best friends.Baba yangu si mzungumzaji sana,na muda mwingi aliutumia nyumbani na mkewe.Kifo cha mama kinamtesa sana baba na kila ninapoongea nae anakumbushia uchungu alionao.

Kuna tatizo jingine pia.Wadogo zangu wa mwisho ni mapacha.Baba na mama walijaliwa kuwapata mapacha hawa wakati umri umeshawatupa mkono.Kwahiyo,Kulwa na Doto wamekuwa kama wajukuu kwa baba na mama.Kwa wadogo zangu hawa,mama alikuwa ni za zaidi ya mzazi wao.Alikuwa ni mwalimu wao (akiwafundisha kupika,sala,nk),alikuwa kama bibi yao (walikuwa wanapenda sana kumtania na yeye alipenda kuwatania pia),alikuwa ni rafiki yao mkubwa kwa vile madogo hao walikuwa wanamwongopa baba,kwahiyo siri zao,habari zao na kila kitu chao walikuwa wanashea na marehemu mama.Kwa ndugu zangu hawa,kifo cha mama ni pigo kubwa sana sana.

Naweza kuandika kitabu kizima kuelezea tukio hili la kusikitisha kupita kiasi.Lakini yote ni mipango ya Mungu.Nakumbuka katika misa ya kabla ya mazishi ya mama,padre alijaribu kutuliwaza kwa kutuambia kwamba "sote tulimpenda Adelina lakini Baba yake aliyepo Mbinguni amemependa zaidi na hivyo ameamua kumchukua mwanae".

Basi,mama mpendwa,leo tunaadhimisha mwaka wa tatu tangu utuache.Pengo lako haliwezi kuzibika.Tunakukumbuka kila siku.Upendo wako,tabasamu lako la muda wote na huruma uliyokuwa nayo ni vitu tunavyoendela kuvienzi.Mafundisho uliyotupa ndio mwongozo wetu wa kila siku.

PUMZIKO LA MILELE AKUPE BWANA NA MWANGA WA MILELE AKUANGAZIE,UPUMZIKE KWA AMANI.AMINA


5 comments:

  1. Pole sana kaka Chahali sote ni wapitaji hapa dunia,Mungu awatie nguvu na Uvumilivu katika maisha yenu,Mshikamane na kupendana ndiyo nguzo yenu, nami nakuongezea hapo katika upendo,Tuungane katika neno hili ambalo nililisambaza kama ujumbe na msisitizo kwa wana wa Coventry Christian Swahili Fellowship, Soma 1 Wakorintho:13:1-13.Pamoja kaka katika kumuenzi mama Chahali.

    ReplyDelete
  2. Mpiganaji Evarist Chahali: Poleni sana na mola awafariji.

    ReplyDelete
  3. Pole sana kaka yangu Chahali. Umenigusa sana na kunikumbusha hisia ambazo na mimi ninazo juu ya mpendwa marehemu yangu. Yeye tarehe 16 mwezi June, anatimiza miaka miwili tangu atutoke. Hakika mama yako alikuwa na upekee, alikuwa mzazi hasa!Kikubwa ni kundelea kuyaishi aliyokuwa akikuasa, na kuendelea kusambaza upendo wake aliokuwa nao kwako kwa watu wengine. Hivi ndiyo mama na Muumba wetu watakavyozidi kufurahi na kukukirimia mafanikio. Tunamkumbuka mama Adelina Mapango sote kaka Chahali

    ReplyDelete
  4. Mpiganaji Chahali: Mola awafariji.

    ReplyDelete
  5. Pole sana Evarist, Hii ndio njia yetu sote, japo kuna watu hawaamini kwa sababu ya anasa za dunia hii.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget