Friday, 6 May 2011


Nilipofika hapa Uingereza kwa mara ya kwanza,takriban muongo mmoja uliopita,nilishangazwa na jinsi wengi wa watu hawa waliotuletea dini huko nyumbani wakiwa hawana habari kabisa na dini.Ilinishangaza kuona baadhi ya majengo yaliyokuwa yakitumika kama nyumba za ibada huko nyuma yakiwa yamegeuzwa klabu za usiku au baa.

Kwa ujumla,idadi kubwa ya wanaohudhuria makanisani kwa hapa ni raia wa kigeni au wale wenye asili ya nje ya nchi hii.Hata hivyo,kuna idadi ya wastani ya Waingereza wanaojitambulisha kama wenye imani ya kidini japo haimaanishi kuwa wanakwenda makanisani.

Pamoja na kuzorota kwa dini miongoni mwa wengi,kwa kiasi kikubwa wananchi hapa wana uadilifu mkubwa hususan katika kutoa huduma.Unajua,kibarua sio suala la mshahara tu bali pia kujali yule unayemhudumia.Kadhalika,kutoa au kupokea rushwa sio tu suala la kukosekana kwa sheria madhubuti bali pia ni suala la kiroho,namna nafsi inavyomsuta mtu kutoa,kudai au kupokea rushwa.

Binafsi nadhani dini ya kweli ni upendo.Na hata katika Biblia Takatifu tunafundishwa kuwa ni vigumu mtu kumpenda Mungu ambaye hamuoni ilhali anamchukia jirani yake anayemwona kila mara.

Japo ni muhimu kuhudhuria nyumba za ibada,lakini binafsi naona ni bora kuwa mtu asiyekwenda kanisani au msikitini lakini anaishi katika namna anayompendeza Mungu (na wanadamu wenzie) kuliko hao wasiokosekana makanisani au misikitini lakini ndio wanaodumisha uzinzi,ufisadi,unafiki,na kila aina ya baya.Hapa simaanishi kuwa kila aendaye kanisani au msikitini hafanyi anayopaswa kufanya,bali napigia mstari umuhimu wa matendo mema.

Kwa hapa Uingereza kumekuwa na mfumuko mkubwa wa makanisa "mapya" (new Christian movements).Makanisa haya yanazidi kupata waumini wengi na kukua aidha kwa sababu madhehebu makuu (Katoliki,Waluteri,Waanglika,nk) yameshindwa kukidhi matarajio ya waumini hao wanaokimbilia makanisa mapya,au kwa upande mwingine ni ukweli kuwa licha ya majukumu ya kiroho,makanisa hayo ambayo waumini wake wengi ni wageni (hususan Waafrika) yamekuwa kama sehemu ya watu wanaotoka eneo moja kujumuika.Mnaijeria akienda kanisa la Kinaijeria anajikuta kama yupo nyumbani,na hivyo hivyo kwa Mtanzania akienda kanisa linaloendesha ibada kwa kiswahili.

Lakini,baadhi ya makanisa hayo yamekuwa yakishutumiwa kuwa ni miradi ya kitapeli ya wajanja flani.Kwa mfano,kituo cha runinga cha Channel 4 kiliwahi kuonyesha documentary ya namna baadhi ya makanisa ya Waafrika jijini London yalivyokuwa yakisababisha kuvunjika kwa ndoa (kwa mfano pale mchungaji anapomwambia mume kuwa mkewe ana majini) na hata kupelekea vifo,hususan vya watoto wadogo wanaotuhumiwa kuwa wana majini.Kibaya zaidi,baadhi ya maaskofu wa makanisa hayo walidiriki kudanganya mabinti kuwa matatizo waliyokuwa nayo yalihitaji maombi maalumu nyakati za usiku,na hatimaye mabinti hao wakaishi kufanyiwa tendo la ndoa.

Utafiti mdogo tuliofanya mie na wanafunzi wenzangu Faith Msina,Latifa Almasi (Queen Latifa) na Baraka Msemwa,mwaka 1999 (kama sehemu ya kozi ya Mwaka wa Tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Sosholojia ya Dini) ulionyesha matokeo kwamba wengi wa watu wanaoamua kujiunga na "madhehebu mapya" ni pamoja na wale wenye matatizo ya kibinadamu ambayo "dini kuu" zimeshindwa kuyatatua.Tulifanya utafiti wetu kwenye Kanisa "la Kakobe" (Full Gospel Bible Fellowship),Mwenge jijini Dar,na asilimia kubwa ya wahojiwa walikiri kuwa kilichowavutia kujiunga na kanisa hilo ni "miujiza" mbalimbali,kwa mfano kwenye uponyaji,ajira,nk.

Lakini jambo la kusikitisha ni tabia inayozidi kushamiri ya matapeli kuanzisha makanisa kama ajira.Hawa ni wajanja wanaofahamu fika kuwa masuala ya imani hayahitaji udadisi,na laiti tapeli husika akifanikiwa kutangaza "miujiza yake",basi muda si mrefu kijikanisa chake kitageuka hekalu kubwa la "maombezi na miujiza".Simaanishi kuwa wote wanaoanzisha makanisa ni matapeli,lakini ni ukweli usiopingika kuwa kuna matapeli kadhaa wanaotumia jina la Bwana kutapeli waumini wenye mahitaji ya kimwili na kiroho.

Ni kwa mantiki hiyo basi,siafikiani na msimamo wa baadhi ya wachunga kondoo wanaopinga dhamira ya serikali kukagua mapato na matumizi yao.Pengine ni kukosa ufahamu tu,uamuzi wa serikali kutotoza kodi au kutoangalia mapato na matumizi ya taasisi za dini ni suala la upendeleo (privilege) zaidi kuliko stahili.Kama waumini wa taasisi hizo za kidini wanawajibika kwa mamlaka za mapato,kwanini isiwe kwa viongozi wa dini na/au taasisi zao?

Je wachunga kondoo hao wa Bwana wanahofia nini kuhusu dhamira hiyo nzuri ya serikali?Ieleweke kuwa kama wana kipato juu ya kiwango cha msamaha wa kodi basi ni lazima walipe kodi.Lakini hata kama suala hapa si ulipaji wa kodi,ni muhimu kwa mamlaka za mapato kufahamu mapato na matumizi ya taasisi hizo kama ilivyo kwa taasisi nyingine za umma na za binafsi.Dini si kigezo cha kutofuata sheria,na hata Maandiko Matakatifu yanakumbusha kuwa "ya Musa apewe Musa,na ya Kaizari apewe Kaizari",or something like that.

Enewei,soma habari husika hapa chini

Maaskofu wapinga serikali kudai taarifa za mapato

na Betty Kangonga

BAADHI ya makanisa ya Kipentekoste yamesema si haki kwa serikali kudai taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za makanisa wakati yenyewe haitoi hata ruzuku kwa taasisi hizo za dini.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mchungaji wa Kanisa la Maombezi la Ubungo Kibangu (GRC), maarufu kama Mzee wa Upako, Anthony Lusekelo, wakati wa hafla ya chakula cha usiku kwa wachungaji 100 wa makanisa ya Kipentekoste.

“Huu ni uonevu usio na mfano, wachungaji lazima tusimame imara kuhakikisha tunatetea haki zetu, tena tunatakiwa kuacha woga. Kwa nini serikali inahitaji mapato na matumizi wakati hawajui fedha hiyo tunapopata? Tunahitaji serikali ijenge heshima na kazi inayofanywa na viongozi wa dini ndani ya nchi,” alieleza.

CHANZO:Tanzania Daima

1 comment:

  1. Hapa umeniacha hoi. Ningekubaliana na hoja yako iwapo serikali hii ingetuhakikishia kwamba kwanza imefanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya watu wa aina ya "mzee wa vijisenti" ambao wanatamba kuweka bilioni za madafu mabenki ya nje kwa madai kuwa wamezipata kwa kufanya biashara - biashara isiyokuwa na kampuni iliyosajiliwa wala leseni. Tokea mzee wa vijisenti alipotangaza kuwa ni mfanyabiashara hatujawahi kusikia TRA wanatueleza iwapo biashara hiyo inalipa kodi.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget