Wasaidizi wana nafuu kuliko rais?Ansbert NgurumoBAADHI yetu hatujaelewa ari, nguvu na kasi ya Rais Jakaya Kikwete. Nina hakika naye ameiimba, lakini hajaielewa barabara.Kaulimbiu hii iliyoasisiwa na kina Samuel Sitta mwaka 2005, ilitumika kumtafutia urais mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya.Waliomjua vema uwezo na udhaifu wake walidokeza mapema kwamba maisha ya Watanzania chini ya CCM ya Kikwete yangedorora na kuwa magumu zaidi - kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.Baadaye, sisi na baadhi ya watani wa CCM tuliifupisha kaulimbiu hiyo, tukaiita ANGUKA. Ni kweli! Miaka mitano baadaye, wameangukia pua.CCM imeanguka. Rais Kikwete ameanguka. Mtandao wake umeanguka. Na kwa bahati mbaya, hata serikali yake imeanguka, ikaishia kuwa serikali kopa-kopa – hata mishahara ya watumishi – licha ya kodi kubwa tunazolipa.Kuanguka huku, ndiko kumekuwa chanzo cha kura chache za mgombea urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kuanguka huku ndiko kumekuwa kichocheo cha vilio vya wananchi dhidi ya ufisadi. Kuanguka huku ndiko kumesababisha hata usanii mpya wa CCM wa ‘kujivua gamba.’Kuanguka huku ndiko kumemkosanisha Rais Kikwete na maswahiba wake wa siku nyingi. Kuanguka huku ndiko kumemfanya Rais Kikwete aogope maandamano ya wananchi yanayoratibiwa na CHADEMA hata akalialia kwamba “wanataka kuniondoa kabla ya wakati.”Kuanguka huku ndiko kumemwondoa Yusuf Makamba katika ukatibu mkuu wa CCM, yeye na sekretariati na Kamati Kuu. Kuanguka huku ndiko kumerutubisha na kukuza fitina na vita ya makundi ndani ya CCM.Kuanguka huku ndiko kumewafanya Watanzania kuikataa CCM waziwazi kuliko wakati wote katika historia, na ndiko kumemwingiza Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM) katika migogoro mipya ndani ya makundi ya CCM na kumwandalia anguko lake huko tunakokwenda, hasa baada ya Rais Kikwete kuondoka madarakani.Anguko hili la ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya limewagusa wananchi wenyewe. Sasa wanakabiliwa na ukali wa maisha usiofanana kabisa na ahadi kemkemu walizopewa na CCM mwaka 2005 na 2010.Bahati mbaya waliosababisha anguko hili, bado wanajitapa kwamba wameleta maendeleo. Vipofu!Na kwa sababu ya upofu huu, wanakosa mikakati mipya ya kujikwamua. Wanarudiarudia yale yale yaliyoshindwa kuwanusuru miaka mitano iliyopita.Kwa mfano, mwaka 2006 mwanzoni, Rais Kikwete aliingia na mbinu ya kutembelea wizara moja moja, kutoa maelekezo na kupiga picha na watumishi wa wizara hizo. Ilikuwa propaganda na mapambo ya magazeti na televisheni.Baadaye, aliwaita mawaziri na watumishi waandamizi wa serikali (mara mbili) katika semina elekezi kwenye Hoteli ya kifahari, Ngurdoto, Arusha.Leo tunapotazama nyuma, ni nani anaweza kujivunia semina elekezi za Ngurdoto?Lakini watu wasiojifunza hawafichiki. Mwaka jana, rais yule yule akagombea kwa kaulimbiu ya ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi. Yaani, hawa jamaa hawakuridhika na ’anguko jipya’ la 2006. Waliona hilo halitoshi, wakatuandaa “kuanguka zaidi” mwaka 2010!Haikumwongezea kura mgombea wao. Haikuvuta hisia za vijana wala kina mama. Ili kupata watu wa kuhutubia ilibidi CCM itumie pesa nyingi kuchapisha na kugawa sare, kuwagawia watu na kuwapakia kwenye magari kuwapeleka kwenye mikutano ya mbali.Haikuwaunganisha watawala wawe na sauti moja, hata baada ya kurejea madarakani. Haikuwasaidia kupata hekima ya kumaliza matatizo ya muda mrefu, kama ukosefu wa umeme ambao umezungumzwa tena na tena bila ufumbuzi.Sasa kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, watawala wamerudi tena katika semina elekezi, chini ya mwelekezaji yule yule.Walidhani zile zilishindikana kwa sababu zilifanyika Arusha. Sasa wamekimbilia Dodoma. Kwa wiki nzima, serikali iko Dodoma, imelala; inakula posho. Kazi zinakwama.Rais naye, badala ya kuwaelekeza kwa hekima na ustadi, “akawananga” wasaidizi wake hadharani, kana kwamba huwa hapati fursa ya kukutana nao – wakati amekuwa akikutana nao kila mwezi katika vikao vya Baraza la Mawaziri. Ndio hao aliowatembelea na kuwasema wizarani kwao miezi miwili iliyopita, hata akawaamuru wengine waache ubabe.Alitaka kuonewa huruma. Alitaka kuwashitaki kwa wananchi – waonekane wabaya, awe mzuri.Rais anawasema mawaziri wake kama watoto wadogo wanaohangaika kuelewa kitu kidogo anachowafundisha. Anawaonyesha wananchi kwamba ana mawaziri mizigo, mbumbumbu – ambao kazi pekee wanayofanya ni “kumwangusha” rais.Anataka turudi kwenye propaganda za kijinga walizoimba miaka mitano iliyopita, kwamba rais pekee ndiye anachapa kazi, bali mawaziri wake wanamwangusha.Anawaambia mawaziri wake kuwa kama hawawezi kazi “waondoke,” kana kwamba hajui uwezo wao, hajui waliingiaje, wakati ndiye aliyewateua na ndiye ana mamlaka ya kuwaondoa.Anataka “watoke” waende kwa wananchi kufafanua mafanikio ya serikali yake. Haamini kwamba wananchi wana uwezo wa kuona mazuri na mabaya ya serikali – bila kusubiri taarifa za mawaziri.Haoni kwamba serikali inayofilisika na kulazimika kukopa hata mishahara ya watumishi wake, inahitaji kubana matumizi na kupunguza ziara na posho nono za viongozi hao waandamizi.Lakini pia, tunapowatazama watu wenyewe aliokuwa anawapa somo, tunabaki kujiuliza: Rais amepata wapi hekima hii ya kudhani ana uelewa mpana kuliko mawaziri wake?Amesomea wapi huko wasikojua wao, alikopata hicho cha kuwafunda? Tunapowatazama baadhi yao tunagundua kwamba kama rais angekuwa na busara ya kujifunza kutokana na miaka mitano iliyopita, asingewaita mawaziri kuwafunda, bali angewaita ili wakae kama timu, awaombe ushauri, awasikilize, wampe mang’amuzi yao na mipango mkakati; naye baada ya kuwasikiliza na kuongeza maono yake, awapangie kazi na kuwadai matokeo baada ya muda kadhaa.Au basi angeunda kikosi kazi cha wasomi waliokubuhu kutoka taasisi mbalimbali zinazoheshimika, akawakutanisha na wasaidizi wake, wote pamoja wakavuna maarifa ya ziada katika kuboresha kazi zao na kukosoa kasoro za huko nyuma.Angejenga mazingira ya kuambizana ukweli, naye akaambiwa kasoro zake; hasa kwamba serikali imekosa mipango mkakati mbadala na hata hiyo iliyopo imekosa msimamizi makini.Kitendo cha rais kulialia mbele ya wateule wake na wananchi kupitia vyombo vya habari si ishara ya ushupavu anaostahili kuwa nao kiongozi mkuu wa nchi.Ndiyo! Tuliona wameinama na kushika tama alipokuwa anafoka. Lakini ana uhakika gani kwamba walikubaliana naye? Ana uhakika gani kwamba walimwona shujaa?Na kwa kiongozi ambaye ameongoza nchi kwa miaka mitano kwa hotuba na matamko yasiyotekelezeka, anadhani mawaziri wake watamwamini na kumheshimu baada ya kufokewa hadharani Dodoma?Labda, watamshukuru kwa kuwatengenezea mazingira ya kula posho za safari. Lakini naamini mawaziri wenyewe wanajua fika kwamba hawana sababu ya kusafiri hadi vijijini kila mara, maana huko kuna watendaji wa ngazi za chini wanaopaswa kusimamia kazi na kuleta taarifa kwa ngazi za juu.Sasa kama rais anaagiza mawaziri waende wenyewe vijijini, hao watendaji wa mikoani, wilayani na vijijini kwenyewe watafanya kazi gani?Hivi waziri aliyekaa katika wizara ile ile kwa miaka mitatu au zaidi, ana kitu gani cha kujifunza kwa rais aliyekaa madarakani kwa miaka mitano bila maono na mafanikio yanayoshikika?Rais Kikwete ana mfano gani wa utendaji uliotukuka anaoweza kuutumia kuwasuta mawaziri wake? Aliacha urithi gani katika wizara alizowahi kuongoza kabla hajawa rais?Ni nani anayejua matatizo, changamoto, na suluhisho la matatizo yake, kati ya waziri aliye kwenye wizara hiyo hiyo, na rais “anayeishi kwenye ndege?”Baadhi yetu tunajua kwamba mkwamo mkubwa wa kiutendaji unatokana na madaraka makubwa ya rais, nidhamu ya woga ya wasaidizi wake na utovu wa uzalendo wa baadhi yao.Zipo taarifa kwamba siku hizi wasaidizi wa rais wameamua kumwambia yale anayotaka kusikia, kwa sababu anawafokea hovyo hovyo wanapomweleza asiyotaka, au wanapompa mapendekezo magumu.Wanadai rais hataki kuambiwa asichotaka; nao hawako tayari kupoteza kazi zao.Kwa mantiki hii, haiwezekani kwamba baadhi ya wasaidizi wa rais wana nafuu kuliko yeye? Kwanini tusiamini, basi, kwamba rais ndiye anawaangusha wasaidizi wake?
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment