Tuesday, 24 May 2011

Askari wa Kikosi cha Kuzuwia Ghasia (FFU) wakiwa tayari kuvunja haki za binadamu nchini Tanzania.Picha hii haihusiani na habari ifuatayo.

Tanzania yetu inaelekea wapi?Tangu lini kupiga picha jeneza imekuwa kosa linalopelekea polisi kukamata waandishi wa habari waliopiga picha majeneza?

Kwa kweli Jeshi la Polisi linafanya kila jitihada kuhakikisha amani na utulivu vinaondoka nchini.Jeshi hilo limekuwa likiendeshwa kibabe pasipo kujali haki za binadamu.Inachukiza kuona polisi wanakurupuka kumkamata mtu yeyote yule wanapojisikia lakini wanakuwa wagumu kuchukua hatua dhidi ya wabaka uchumi wanaotenda uhalifumkubwa kwa taifa kuliko raia wema hao wasio na hatia.

Kadhalika,jeshi hilo limekuwa halina heshima yoyote kwa wanasiasa na wanachama wa vyama vya upinzani ambapo polisi wanawakamata ovyo ovyo.Wito wa tovuti hii ni kwa wanaokamatwa kufungua kesi za madai wanapoachiwa bila kufunguliwa mashtaka.Tkuwaacha wahuni hawa waliokabidhiwa jukumu la usalama kwa raia lakini badala yake wanapelekea adha kwa raia wasio na hatia tutaishia kujilaumu huko mbeleni.Violence begets violence,wananchi watafika mahala wakaamua liwalo  na liwe na hao polisi waonevu hawatakuwa salama.

Ubabe sio ufumbuzi wa matatizo kwani kama tumeshuhudia tawala kadhaa za kibabe zikiondoka madarakani pale wananchi wanapoamua kuwa imetosha,enough is enough.Soma habari ifuatayo na utaelewa ninacholalamikia hapa

Polisi wadaiwa kupora maiti Tarime 
Tuesday, 24 May 2011 22:44

WADAIWA KUVAMIA MOCHWARI USIKU,
WABUNGE CHADEMA WATUPWA RUMANDE
Waandishi Wetu
POLISI Kanda Maalumu ya Tarime, wanadaiwa kuvamia chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Mara kuchukua maiti za watu wanne waliouawa katika tukio la uvamizi wa Mgodi wa Nyamongo na kuziweka chini ya ulinzi.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa tukio hilo lilikwenda sambamba na kukamatwa kwa watu 12 wakiwemo wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Waliokamatwa katika tukio hilo ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko. Wengine ni kada wa Chadema, Waitara Mwita na wakazi wengine sita wa Tarime ambao majina yao hayakupatikana mara moja.

Chanzo kimoja cha habari kilisema jana kwamba watu hao walikamatwa majira ya saa 3:23 juzi usiku baada ya polisi kupiga mabomu ya machozi eneo la chumba cha kuhifadhia maiti kuwatawanya watu waliojitokeza kuzuia polisi kuchukua miili ya marehemu usiku huo.

Taarifa zilisema kuwa mbali na watu hao kukamatwa juzi, jana majira ya saa 4:30 asubuhi waandishi wa habari watatu; Anthony Mayunga (Mwananchi), Beldina Nyakeke (The Citizen) na Anna Mroso (Nipashe), walikamatwa.

Waandishi hao walikamatwa jana na mbunge huyo wa viti maalumu wa Chadema katika Kijiji cha Nyakunguru na kuhojiwa kwa muda katika Kituo cha Polisi Nyamwaga kabla ya kupelekwa kwa Kamanda wa Operesheni Maalumu, Paul Chagonja. Waliachiwa kwa kujidhamini wenyewe saa 9:30 jioni.

Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema alipotafutwa kuzungumzia suala hilo simu yake ya mkononi ilipokewa na msaidizi wake ambaye alisema anayeweza kulitolea ufafanuzi ni msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso.

Senso alipotafutwa naye alisema hawezi kulizungumzia akimtupia mpira Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime, Constantine Massawe.

Hata hivyo, Massawe alikanusha madai hayo ya kupora maiti akisema kwamba walipata taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu kwamba kuna baadhi ya watu waliokuwa wakiwazuia kuchukua miili ya ndugu zao.

"Jana baada ya kufanyika uchunguzi kama walivyotaka, miili yote ilikuwa chini ya familia. Sasa uamuzi wa kuzika ulikuwa juu yao, lakini majira ya saa mbili usiku tulipata taarifa kuwa kuna watu wako mochwari wamezuia ndugu wanaotaka kuzika wasichukue miili ya jamaa zao," alisema Kamanda Massawe na kuongeza:

"Tulipofika tulikuta wapo watu wanane, wanne walikuwa ni wakazi wa Singida na wengine wanne wakiwa ni wakazi wa Tarime. Tuliwakamata na kusimamia ulinzi wa ndugu waliotaka kuchukua miili ya jamaa zao wakachukua."

Alisema baada ya miili hiyo kuchukuliwa, polisi ililitoa msaada wa kuwasafirishia ndugu hao hadi majumbani kwao na walikuwa wanaishusha kadri walivyokuwa wameambiwa na ndugu hao.

‘Sasa asubuhi hii (jana), tumeelezwa kuwa kuna kundi la watu wengine lilikuwa likipita nyumba hadi nyumba kuwahamasisha wafiwa kutokubali kuzika maiti za ndugu zao baada ya kufuatilia tuliwakamata na hawa waandishi wakiwa wanapiga picha jeneza," alisema Kamanda Massawe.

Awali, Katibu wa Chadema Tarime Mjini, Paschal Warioba alidai kuwa polisi walipora maiti hizo na kwamba viongozi wa chama chake walikamatwa juzi usiku majira ya saa nne.

"Lissu yuko 'lockup' (rumande) hapa Nyamongo, walikuwa wakifuatilia maiti za watu waliouawa katika vurugu mgodini ili leo (jana) ziende kuzikwa, lakini kabla ya kufanikisha zoezi hilo jana (juzi), polisi walizipora maiti hizo kwa kuwadanganya baadhi ya ndugu kwa kuwapa fedha ili waende kuzizika," alisema.

Warioba alidai kuwa baadhi ya maiti tayari wamezikwa, lakini wengine wameonekana katika maeneo karibu na walipokuwa wakiishi.

Juzi alasiri, maiti hao walifanyiwa uchunguzi wa mwisho tayari kwa ajili ya maandalizi ya mazishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika jana chini ya uratibu wa Chadema kabla ya vurugu kubwa kuibuka katika chumba cha maiti baada ya polisi kufika na kukuta umati wa watu uliokuwa tayari umekusanyika kuanzia saa 1:30 jioni ili kuchukua miili hiyo kwa ajili ya mazishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo.

Hata hivyo, Chadema kinadai kwamba baadhi ya ndugu wa wafiwa waliona maofisa wa polisi wakinunua majeneza manne na kuyapakia katika gari lao kabla ya kufika hospitali hapo kuchukua miili hiyo.

Kutokana na taarifa hiyo, Lissu, Waitara na makada wengine wa Chadema wakiwa na wananchi wengine waliamua kufika katika eneo la mochwari na muda mfupi baadaye, idadi ya watu iliongezeka kwa lengo la kuzuia Polisi kubeba miili hiyo.

"Wakati tukio hilo hapo mochwari polisi walifika majira ya saa mbili usiku na kukuta timu kubwa ya watu ambao walikuwa wamejitolea kulinda maiti hao wasichukuliwe," alisema mkazi wa Tarime aliyejitambilisha kwa jina la Mwita Nyankaira na kuongeza:

"Walianza (polisi) kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya watu na ndipo walipowakamata kina Lissu na wengine. Sisi tulifanikiwa kukimbia."

Alisema baada ya polisi kuwasambaratisha wananchi, walirudi hospitalini hapo na kuchukua maiti hao na kuanza kuwapeleka usiku huohuo kwenye familia za wafiwa.

Habari zimeeleza maiti ya Chawali Bhoke ilipelekwa katika Kijiji cha Bonchugu, wilayani Serengeti na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mwikwabe Makena alisema kulikuwa na vurugu kubwa jana asubuhi kijijini hapo baada ya polisi kuwalazimisha ndugu kupokea mwili huo kwa ajili ya kuuzika.

"Kumekuwa na vurugu kubwa iliyoambatana na polisi kurusha mabomu ya machozi," alisema mwenyekiti huyo.

Maiti nyingine ilipelekwa katika Kijiji cha Nyakunguru, Kata ya Kibasuka. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamanche kilichoko kwenye kijiji hicho, Isaack Marara alisema jana saa 12:00 asubuhi, alifuatwa na mkazi wa eneo hilo, Kisabo Ghati na kumweleza kuwa kuna jeneza limewekwa barabarani lakini hawajui kuna nini ndani yake.

"Watu walishtuka sana kwani hawajawahi kuona tukio hilo. Baba mdogo wa marehemu Emmanuel Magige, Ambrose Nyabwanya alidai kuwa saa 6:00 usiku wa juzi, magari mawili ya polisi yalisimama na kushusha jeneza mita 200 kutoka nyumbani kwao kisha magari hayo yakaondoa haraka.”

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Mwanasheria na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando alisema kitendo cha polisi kuchukua kinguvu miili ya watu hao wanne kwa lengo la kwenda kuizika ni kinyume na walivyokubaliana.

Marando alisema walikubaliana na polisi pamoja na ndugu wa marehemu Jumapili iliyopita kwamba shughuli za mazishi zifanyike leo katika Uwanja wa Sabasaba.

“Chadema siyo kama tumeshikilia kidedea msiba huu. Tunafanya hivi kwa kuwa waliouawa ni makada wa Chadema na hiyo ndiyo siasa."

Ripoti ya uchunguzi wa miili yawekwa hadharani

Uchunguzi wa miili ya maiti wanne waliopigwa risasi na askari polisi katika Mgodi wa African Barrick North Mara uliofanywa na daktari bingwa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Makatta imebaini kuwa marehemu wote walipigwa risasi maeneo ambayo hayakulenga kujeruhi, bali kuua.

Uchunguzi huo uliochukua saa 4:27 ulianza saa 5.20 asubuhi hadi saa 9.47 alasiri. Upande wa familia za wafiwa ulisimamiwa na Dk Greyson Nyakarungu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Tarime na askari wawili. Taarifa hiyo itakabidhiwa kwa hospitali

Dk Nyakarungu alisema Emmanuel Magige mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari namba za PM1/5/2011 (TGH), alipigwa risasi katika nyonga ya kushoto ambako kulikuwa na tundu la duara llilokuwa na upana wa sentimita 0.5 ilipoingilia na sentimita 2.5 ilipotokea.

“Mishipa ya damu iliharibiwa, kibofu cha mkojo, mishipa ya fahamu, mfupa wa nyonga ulisagika, damu ikavia ndani ya tumbo, lakini chini ya mgongo karibu na risasi ilipotokea kulikuwa na tundu linaloonyesha kuwa alichomwa na kitu chenye ncha kali kama singa ya bunduki,” alisema na kuongeza:

“Tumebishana sana kwa hilo wenzangu wakidai huenda aliangukia kitu kikamchoma, ikumbukwe kuwa alipigwa kwa nyuma akikimbia hivyo asingeweza kuanguka chali zaidi ya kifudifudi,” alisema.

Kuhusu Chacha Ngoka mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari PM 2/5/11 (TGH), uchunguzi ulibaini kuwa alipigwa risasi mgongoni karibu na kiuno na kutokea katikati ya mbavu chini ya titi, tundu la kuingilia likiwa ni sentimita za duara 0.3 na ukubwa wa tundu pa kutokea ikiwa ni sentimita tano.

Mishipa mikubwa ya damu iliharibiwa, ini likasagwasagwa, damu iligandia kwenye mfumo wa upumuaji hali ambayo inadhihirisha kuwa alipumua kwa nguvu, damu ilikwisha mwilini na kuwa alipigiwa risasi kwa mbali.

Alisema marehemu Bhoke mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari PM/3/5/11(TGH) alipigwa risasi ya kichwani karibu na sikio na kidonda chake pakuingilia ni sentimita za duara 0.2 ,pa kutokea sentimita tano za duara kwenye paji la uso hivyo kuharibu ubongo, fuvu na mifupa yote kubomolewa.

Kuhusu uchunguzi wa Mwikwabe Marwa Mwita mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari PM/4/11 (TGH) alisema alipigwa risasi karibu na nyonga na kuacha tundu la sentimita za duara 3,5 na risasi haikutoka nje na kuharibu mifupa yote ya nyonga, misuli ikawa imeharibiwa na kipande cha risasi kilikutwa katikati ya misuli (PSOAS), damu ikiwa imevia tumboni.

“Kilichoonekana hapo ni kuwa walipigwa risasi kwa mbali tena kwa nyuma maana wote zimeingilia kwa nyuma na maeneo waliyopigwa risasi ni yale ya kuua si kuwapunguza nguvu kama walikuwa wamegoma kusalimu amri,” alisema daktari huyo.

Kuzuiwa kwa maziko ya pamoja

Awali, Chadema kilipanga kuendesha ibada ya maziko katika Uwanja wa Sabasaba leo kuanzia saa 2:00 asubuhi kabla ya kupelekwa katika vijiji vyao kwa ajili ya mazishi ya kifamilia.

Lissu alisema juzi usiku kuwa licha ya kukubaliana na wanafamilia na Kamishina wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, jeshi la polisi lilibatilisha kibali hicho baadaye.

"Tumekuwa katika maandalizi ya mazishi hayo tangu jana jioni. Hata hivyo, jioni hii tumeletewa barua ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Tarime kututaarifu kwamba haturuhusiwi tena kuwaaga marehemu wetu kama ilivyokubaliwa jana," alieleza Lissu.


Waandishi waeleza walivyokamatwa

Baadhi ya waandishi waliokamatwa katika sakata hilo walieleza kuwa walikuwa kazini kutekeleza majukumu yao.

Mmoja wa waandishi waliokamatwa, alisema baada ya kusikia taarifa juzi usiku juu ya polisi kupiga mabomu na kuchukua miili ya marehemu aliamua kuingia kazini kufuatilia tukio hilo.

“Tulipofika hapo kijijini tulikuta pia kuna mbunge wa viti maalum wa Chadema, sasa wakati tukiwa tunamhoji, polisi wakafika na kutukamata wakieleza kuwa tumekuwa tukichochea ndugu wasizike miili ya marehemu," alisema

Alisema kitendo cha polisi kuwahoji jana kuanzia saa 5:10 asubuhi hadi saa 6:20 mchana kimewafanya washindwe kuwajibika ipasavyo jambo ambalo linapaswa kulaaniwa na wadau wote wa habari.

“Tulihojiwa hapa kwa zaidi ya saa moja na ilipofika saa 6:20 mchana walituambia tusubiri maelekezo kutoka kwa kamanda wa polisi…" alisema.

Mei 16, mwaka huu polisi wilayani Tarime iliwaua kwa kuwapiga risasi watu wanne kati ya zaidi ya watu 1,000 waliovamia mgodi wa Nyamongo wilayani humo kwa lengo la kupora mchanga wa dhahabu.

Tukio hilo lililotokea katika Kijiji cha Matongo, lilizua msuguano baina ya polisi, Chadema na wananchi wa eneo hilo ambao juzi waligoma kuzika miili ya marehemu hao na kukataa rambirambi ya polisi.

Habari hii imeandaliwa na Antony Mayunga, Tarime,
Frederick Katulanda, Mwanza na Fidelis Butahe Dar


CHANZO: Mwananchi

2 comments:

  1. SALAM"" MIMI BADO SIJAPATA PICHA ,LOL. SASA HAYO MAGENEZA YALIKUWA YA NANI NA WAPI ? NA JE HAO WAANDISHI WAPIGA PICHA WALIKUWA NA LENGO GANI ? NI LAZIMA HAPA PANA NAMNA,SIYO BURE WATU WAENDE KUPIGA PICHA MAGENEZA NA KUZUILIWA,,,MPAKA KUKAMATWA NA POLICE...

    ReplyDelete
  2. Yaani it is just sad? Kutupa miili ya watu njiani. Ni inane tu but watanzania winging wanajifanya kukaa Linus kwa vile ni kwa jirani ngoja siku moto uwake. Na kwetu hatuna mafuta tutakatana mpaka tuishe. Sipendi wanamaker siasa lakini napenda chadema inavyosaigia kuonyesha watu kutambua haki zao. Wengi hawajui sheria za nchi wala haki zao.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget