Watendaji wa Ifakara wametakiwa kuangalia uwezekano wa kuzungumza na uongozi wa Kanisa Katoliki juu ya ughali wa tiba unaotolewa katika Hospitali yao ya Mtakatifu Francis. Rai hiyo imetolewa na Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa upokeaji taarifa ya wilaya, mkutano uliofanyika Ikulu Ndogo ya Ifakara juzi.
Kauli hiyo ilitokana na rai ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapo ambao walitoa kilio cha tiba ghali katika hospitali hiyo na kutaka serikali iingilie kati. Hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki inadaiwa kutoa huduma kwa bei ghali baada ya wafadhili wake wakubwa wa Uswisi kujiondoa na kuingia Wataliano.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya, Evaristo Ndikilo akichangia hoja ya afya, alisema kwamba kwa upande wao walikuwa wakifikiri kupandisha hadhi kituo chao cha afya kukifanya kuwa hospitali. Hoja hiyo pia ilizungumzwa na Mbunge wa Ulanga Mashariki, Celina Kombani juu ya kuwapo kwa haja ya kupandisha kituo hicho, na kueleza mchakato umeshaanza. Kombani pia ni Waziri wa Tamisemi.
Mwenyekiti wa Halmadhauri ya Ifakara, Hassan Goagoa, alisema ughali wa hospitali hiyo ambayo inatumika pia na mikoa mingine na shughuli za utafiti, kunatokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na ingawa walishauriwa kuomba udhamini zaidi wa serikali kwa kuongeza idadi ya vitanda, hali imebaki kwao kama kitendawili. Hospitali ya Ifakara tayari ina vitanda vingi kwa hadhi yake ya kuwa hospitali teule ya rufaa. Rais aliendelea na ziara yake ya Mkoa wa Morogoro ambapo jana alitarajia kuzuru Wilaya ya Kilosa.
CHANZO: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment