Serikali imewataka wanafunzi wote wa vyuo vya elimu ya juu nchini kuingia madarasani mara moja ifikapo saa moja asubuhi leo. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe alisema sera ya uchangiaji huduma za jamii ikiwamo elimu, halikwepeki katika mazingira haya ya kiuchumi.
“Sera yoyote ile haiwezi kubadilishwa mara moja bila ya majadiliano ya kina yanahusisha wadau wote,” alisisitiza Profesa Maghembe, katika kujibu madai ya wanafunzi hao wanaopinga sera ya uchangiaji elimu ya juu hasa suala la mikopo wakitaka kulipwa asilimia 100.
Waziri huyo wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alisema matatizo yote ya kiutendaji katika utekelezaji wa sera ya elimu yatatafutiwa ufumbuzi. “Itaundwa kamati itakayowashirikisha wadau wote mkiwamo wanafunzi,” alisema Profesa Maghembe, ingawa hakufafanua hatua zitakazochukuliwa endapo wanafunzi watakataa kutii agizo hilo la kurejea madarasani leo.
Akiahirisha Bunge mjini Dodoma Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hivi sasa serikali inabeba gharama za kuchangia elimu ya juu, na haitawezekana kutoa mikopo kwa asilimia 100. “Kwa hali ya kawaida, hii mikopo ilitakiwa ilipiwe riba kwa wanafunzi, lakini kwa sasa serikali inabeba mzigo huo.
Hatuna uchaguzi mwingine, bali kuendelea kuchangia gharama za elimu ili wanafunzi wengi zaidi wapate elimu ya juu,” alisema Pinda bungeni na kuongeza: “Napenda nirudie kusema kwamba serikali wakati wote itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafunzi wanapata kile wanachostahili kujiendeleza kielimu.
Naomba nitamke kuwa wanafunzi wale wanaotaka wanafunzi wote kupewa mikopo asilimia 100 haiwezekani.” Awali, jana wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani wameendelea kusisitiza kuendelea na mgomo leo baada ya Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutotokea chuoni hapo.
Akihutubia wanafunzi waliokusanyika kwa shauku katika Ukumbi wa Nkrumah kusubiri tamko la serikali, Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO), Anthony Machibya alidai amepata taarifa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu pamoja na wasaidizi wake waliitwa Ikulu na Rais kwenda kujadili matatizo yao.
“Profesa Mukandala ameondoka kimya kimya na wasaidizi wake wameenda Ikulu kujadili mgomo wetu, nimepigiwa simu na Karani wake, kwa hiyo tusikate tamaa tuendelee na msimamo wetu mpaka tuone hatima yetu,” alisema Machibya na kuongeza kuwa mgomo utaendelea kama kawaida hawatarudi nyuma. Aidha, magari matatu yakiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), yalikuwa yakirandaranda katika maeneo ya chuo hicho tangu juzi na jana kuhakikisha usalama wa mali na watu unakuwapo.
CHANZO: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment