Picha kwa hisani ya LUKWANGULE
Albino anusurika kunyofolewa mkono (Majira Novemba 16,2008)
*Mnyofoaji alimrubuni kuwa anataka kumwoaNa Benedict Kaguo, TangaWIMBI la mauaji ya albino limechukua sura mpya mkoani Tanga baada ya Bibi Aisha Yusuph mwenye ulemavu huo kunusurika kuuawa kikatili.Imedaiwa Bibi Aisha alinusurika kuuawa na Bw. Mohamed Athuman baada ya kutaka kumkata mkono ili kwenda kuuza.Polisi mkoani hapa tayari imemkamata Bw. Athuman ambaye ni mkazi wa kijiji cha Dindira, Korogwe kwa tuhuma za kutaka kumuua Bi Aisha.Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Bw. Anthony Rutta, alisema mtuhumiwa huyo alitaka kutenda kosa hilo kwa kujifanya anataka kumchumbia Aisha.Tukio hilo lilitokea Novemba 13 mwaka huu saa 12 jioni katika kijiji chaDindira.Bw. Athuman amelazwa katika Hospitali ya wilaya Korogwe Magunga kutokana na kipigo cha wananchi wenye hasira baada ya kubainika kutaka kumuua albino huyo.Polisi Tanga inawashikilia watu wawili kuhusu tukio hilo ambao ni Bw. Eliaza Seif na Bw. Shaaban Ramadhan wote wakazi wa Dindira.Watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya upelelezi kukamilika.
Waua albino na kutoweka na miguu yake (Majira Julai 1,2008)
Na Mary Ng'oboko, MwanzaJESHI la Polisi mkoa wa Mwanza, linawatafuta watu wanne kwa tuhuma za kumkatakata na mapanga hadi kumuua albino na kutoweka na miguu yake.Akizungumza jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Khamis Bhai, alisema watu hao walifika nyumbani kwa albino huyo wakiwa na mapanga na wamevaa makoti meusi.Kamanda Bhai alimtaja marehemu kuwa ni Bw. Nyerere Ludaila (50) ambaye ni mkazi wa eneo la Usagara wilayani Misungwi mkoani hapa.Alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 2.30 usiku katika kijiji cha Nyaligwe, Usagara.Kamanda Bhai alisema inasemekana albino huyo alikuwa ni mganga wa kienyeji na kwamba wiki mbili kabla ya tukio, alikuwa na ugomvi na mtoto wake mkubwa uliosababishwa na mtoto huyo kudai urithi wa mali kutoka kwa baba yake, huku angali hai, lakini baba yake hakuwa tayari kutoa urithi huo."Baada ya tukio la mauaji, mtoto huyo wa albino ambaye hatujaweza kupata jina lake, alikimbia na hajaonekana nyumbani hadi sasa, nasi tunaendelea kumtafuta tukishirikiana na wananchi," alisema Kaimu Kamanda Bhai.Alisema hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo na kwamba polisi wanaendeleza juhudi za kuwatafuta wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Wafukua kaburi wakidhani la albino, watoweka na mifupa (Majira Agosti 6,2008)
Na Theonestina Juma, BukobaWATU wasiojulikana wamefukua kaburi la mtu waliyedhani ni albino aliyefariki dunia miaka 18 iliyopita na kutokomea na mifupa yake yote.Habari kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Bw. Henry Salewi, zilisema tukio hilo lilitokea Julai 30 mwaka huu usiku, katika kitongoji cha Igabilo kijiji cha Ihangiro kata ya Nshamba wilayani Muleba.Ilielezwa kuwa watu hao wasiojulikana walifukua kaburi la albino aliyejulikana kwa jina la Bibi Hilda Angelo (60) aliyefariki dunia Februari 6, 2001 kwa lengo la kuchukua mifupa yake inayoaminika kutumika kwa masuala ya kishirikina.Hata hivyo, inadaiwa kuwa watu hao hawakulenga kaburi la albino huyo kutokana na la mumewe Bw. Mkalimo Rufurani aliyefariki dunia mwaka 1990 kuwa karibu nalo.Ilielezwa kuwa makaburi ya wanandoa hao yalipangwa sehemu moja na hivyo watu hao walipofika walifukua kaburi la mume badala ya mke aliyekuwa albino na kuondoka na mifupa.Habari zaidi zilieleza kuwa watu wa familia hiyo walipoamka walikuta kaburi likiwa wazi huku mifupa yote ikiwa imechukuliwa na watu wasiojuliakana.Novemba 26 mwaka jana, katika kitongoji cha Nyakashenye kijiji na kata ya Rushwa, Muleba, watu wasiojulikana walifukua kaburi la Zeuria Yustance aliyefariki dunia Oktoba 29, 2006 wakati akijifungua na kuchukua masalia ya mifupa yake yote na kutokomea nayo.Hili ni tukio la pili kutokea wilayani humo ya watu wasiojulikana kufukua makaburi ya maalbino kwa lengo la kuchukua mifupa.Katika tukio lingine katika kijiji cha Nyambogo kata ya Ilememleza wilayani Chato, umeokotwa mwili wa mwanaume ukiwa umecharangwa mapanga na kisha kuteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana.Hata hivyo haijajulikana mtu huyo alikuwa akituhumiwa kwa kosa gani hadi kufikia hatua ya watu hao wasiojulikana kumteketeza kwa moto.Uchunguzi zaidi unafanywa na Jeshi la Polisi Wilayani humo ikiwa ni pamoja na kuwasaka watu waliojulikana katika mauaji hayo ya kikatili.
'Biashara ya viungo vya albino vigogo wanahusika' (Majira Oktoba 16,2008)
*Yahofiwa kuongezeka katika uchaguzi 2010Na Gladness MbomaSIRI nzito juu ya mauaji ya albino yanayoendelea kutokea sehemu mbalimbali nchini imefichuliwa kufuatia utafiti wa kina uliofanywa na albino wenyewe na sasa wameamua kukifikisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete.Kwa mujibu wa utafiti huo, imebainika kuwa watu wanaotumwa kukata viungo hivyo na kuua albino wanapewa fedha nyingi na vigogo ambao huvitumia kishirikina.Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania, Bw. Ernest Kumaya, wakati akizungumzia maandamano ya amani ya kupinga na kulaani mauaji yanayoendelea dhidi yao nchini."Tunaamini kabisa watu wanaonunua viungo hivi vya albino ni watu matajiri na wenye madaraka makubwa katika maeneo malimbali ikiwamo serikalini."Mtu maskini hana uwezo na hawezi kununua kiungo kimoja kinachouzwa sh. milioni 13 hadi 14 ni matajiri ndio wenye uwezo wa kununua," alisisitiza Bw. Kumaya akibainisha waliyoyagundua.Alisema kutokana na hali hiyo wana hofu kubwa katika uchaguzi mkuu wa 2010 viungo vyao vitazidi kuongezeka kwani kipindi hicho cha kuelekea uchaguzi mbalimbali nchini vitendo vya kishirikina pia huongezeka."Wakati huo kila kiongozi atataka kuhakikisha anashinda, hivyo kwa kuwa viungo vyetu ni biashara, vitendo vya kishirikina vya mauaji ya albino kwa ajili ya kuchukua viungo vyetu vitaendelea kutawala," alisema.Alisema katika uchunguzi wao wa Septemba mwaka huu albino waligundua pia kuwapo kwa kikundi cha watu wasiozidi 10 wakiwamo wanawake ambao wamekuwa wakifanya mauaji hayo.Bw. Kumaya alisema kikundi hicho ambacho kilikuwa kipo Kanda ya Ziwa hasa Mwanza kimehamia Bukoba na baadaye wanahofia kwamba kitahamia Dar es Salaam.Akigusia maandamano waliyopanga kuyafanya Oktoba 19 mwaka huu na Rais Kikwete kutarajiwa kuwa mgeni rasmi, Bw. Kumaya alisema msukumo uliowafanya waandae maandamano ni kutoona juhudi hasa za kumaliza tatizo la mauaji dhidi ya albino, ambapo yanazidi kuongezeka huku viongozi wakuu na watoa uamuzi wakiendelea kukaa kimya.Maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia kwenye viwanja vya Shule ya Walemavu ya Uhuru Mchanganyiko na kuishia viwanja vya Karimjee."Kutolipa kipaumbele suala la mauaji ya albino kitaifa, mfano vifo vinavyotokea katika migodi ya madini ya Mererani viliundiwa Tume na kushughulikiwa maafa hayo ni mambo yaliyotufanya tuandamane."Vifo vya watoto vilivyotokea wakati wa Sikukuu ya Idd mkoani Tabora, Serikali imetia mkono wake kwa kutoa pole kwa wafiwa yakiwamo mashirika kutoa rambirambi zao kuonesha kuguswa na janga hilo, lakini suala la mauaji ya albino nchini viongozi hawajaweza kuchukua hatua madhubuti zenye kuonesha mwelekeo," alidai.
NILIWAHI KUANDIKA MAKALA KATIKA GAZETI LA RAIA MWEMA KUHUSIANA NA SUALA HILI.UNAWEZA KUJIKUMBUSHA NILIYOJADILI HUMO KWA KUBONYEZA HAPA
0 comments:
Post a Comment