MVUTANO mkali uliibuka jana katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa NEC- CCM kuhusu mwenendo wa baadhi ya wabunge wa chama katika mambo mbalimbali yaliyolihusu taifa na chama hicho. Tanzania Daima Jumapili imedokezwa.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho vililieleza gazeti hili kuwa mvutano huo uliibuka baada ya baadhi ya wajumbe wa kikao hicho ambao si wabunge kuwashangaa wenzao ambao wamekuwa wakiibua hoja zenye mwelekeo wa kuishambulia serikali na wale wanaoendeleza hoja zenye mwelekeo wa kuchochea udini.
Habari hizo zilieleza kuwa wajumbe wa kikao ambao si wabunge walionyesha dhahiri kuchukizwa na hatua ya baadhi ya wajumbe ambao ni wabunge ya kuanza kuwachimba viongozi wa kitaifa wa chama hicho kwamba inahatarisha umoja wa chama hicho.
Sambamba na taarifa za kuwepo mjadala mkali kuhusu hoja hizo, taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa wakakti Bunge likisubiri hatua zitakazochukuliwa na serikali dhidi ya gazeti lake la Habari Leo, baada ya kufichua njama za kundi dogo la wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kusuka zengwe la kumpinga hadharani Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kuhusu hatua alizozichukua dhidi ya wezi wa EPA, chama hicho kimeanzisha uchunguzi wa kuwabaini wabunge waliodaiwa kuhusika katika mpango huo.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya chama hicho, vimedokeza zaidi kuwa hatua hiyo ina nia ya kutaka kuthibitisha kilichoandikwa na gazeti hilo la serikali kama ni kweli au ni uongo na uchochezi, kama ilivyodaiwa juzi bungeni na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka.
Sendeka, mmoja wa wabunge machachari ndani ya CCM, juzi akitumia kanuni ya Bunge namba 68, alieleza masikitiko yake kuhusu habari iliyoandikwa katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la Habari Leo kuwa ilikuwa ya uchochezi na kuitaka serikali ichukue hatua kama ilizochukua kwa gazeti la MwanaHalisi, ambalo limefungiwa miezi mitatu, kwa madai ya kuchapisha habari ya uchochezi kuhusu kuwepo mpango wa kumng’oa madarakani Rais Kikwete, ifikapo mwaka 2010.
Habari iliyochapishwa na Habari Leo ilieleza kuwa kuna kundi la wabunge ambalo kwa makusudi lilikusudia kuwasilisha hoja hiyo bungeni, lakini mkakati huo ulizimwa na habari iliyochapishwa na gazeti hilo kabla ya kundi hilo kuwasilisha linachokiamini kuwa Rais Kikwete hajachukua hatua stahiki katika kulishughulikia suala la wezi wa EPA.
“CCM imeshitushwa na hoja hiyo kuletwa bungeni, kuomba serikali ichukue hatua dhidi ya gazeti la Habari Leo wakati taarifa hiyo inaelezwa na walioitoa kuwa ni kweli tupu. Sasa chama kimeamua kufanya uchuguzi ili kije na majina ya wabunge waliokuwa na mpango huo na mahala walipoendeshea vikao hivyo ili kuuthibitishia ulimwengu kwamba habari hiyo ni sahihi na kwamba kuna wabunge waliopanga kumdhalilisha rais,” kilisema chanzo chetu hicho cha habari.
Juzi Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Serikali ya Daily News na Habari Leo, Isaac Mruma, alikaririwa akieleza kuwa habari iliyoandikwa na gazeti analolisimamia ni sahihi na ya kweli.
“Kwanza napenda kusema kuwa tuna uhakika na tulichokiandika kuwa ni kweli, kwani chanzo chetu cha habari ni cha kuaminika,” alisema Mruma.
Alipoulizwa ni kwanini walichapisha habari hiyo upande mmoja bila kupata maelezo ya upande wa pili, yaani bungeni au kwa wabunge waliotuhumiwa, Mruma alisema taarifa hiyo waliipata usiku, hivyo walishindwa kuwatafuta wahusika, licha ya kwamba waliwajua kupitia chanzo chao cha habari.
Alisema kutokana na hali hiyo, waliamua kuyaondoa majina ya wabunge wote waliokuwa wakitajwa kuhusika katika mpango huo wa kumpinga Rais Kikwete, kuhusu namna alivyoeleza jinsi suala la EPA litakavyoshughulikiwa, wakati akilihutubia taifa hivi karibuni.
Mruma aliwataka wabunge kutambua kwamba gazeti la Habari Leo ni chombo cha serikali na lina dhamana ya kuchukua tahadhari kwa kuandika jambo lolote linaloonekana kwa namna moja ama nyingine kujaribu kuiyumbisha serikali au rais aliye madarakani.
Habari zaidi kutoka mjini hapa ambapo kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kinaendelea, zilieleza kuwa huenda suala la habari hiyo likaibua mjadala mzito katika kikao cha NEC kinachoendelea leo mjini hapa.
Akiwasilisha maelezo yake juzi bungeni, Sendeka alisema habari hiyo iliyokuwa na kichwa kisemacho ‘Kundi la wabunge CCM lasuka zengwe la EPA, ilikuwa na lengo la kuleta mtafaruku na uchochezi kati ya wabunge wa CCM na serikali.
Hoja ya Sendeka iliungwa mkono na Spika Samuel Sitta, ambaye alieleza kushangazwa kwake na habari hiyo kutoa maelekezo kwa serikali kufuatilia suala hilo na kupelekewa taarifa.
Kwa upande wake serikali, ilisema tayari ilishaanza kulishughulikia suala hilo kwa kuwahoji wahusika.
0 comments:
Post a Comment