Serikali imesema itakuwa tayari kununua mitambo ya Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd endapo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), litaishauri kufanya hivyo. Dowans Tanzania Ltd jana ilitangaza rasmi zabuni ya kuuza mitambo yake ya kuzalisha umeme ikiwa ni miezi mitatu baada ya serikali kukatisha mkataba wake na Tanesco.Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliiambia HabariLeo jana kuwa kimsingi serikali haitakuwa na tatizo na mitambo hiyo endapo wataalamu wa Tanesco watashauri hivyo. “Tanesco ndiyo wataalamu wetu, tutawauliza wakisema tununue tutanunua, lakini kwa kufuata taratibu na sheria za manunuzi ya mitambo hiyo,” aliongeza Ngeleja.Endapo serikali au Tanesco watanunua mitambo hiyo, itasaidia kupunguza uwezekano wa kutokea mgawo wa umeme mara mitambo mingine ikipata hitilafu. Mwezi uliopita, Tanesco ililazimika kutangaza mgawo wa umeme baada ya mashine moja ya Kampuni ya Songas yenye uwezo wa kuzalisha megawati 40 kuharibika.Hata hivyo, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud alisema jana kuwa shirika hilo halijaamua kama watanunua au la. Alisema watatoa taarifa uamuzi ukifikiwa. Dowans Tanzania Limited ilirithi mkataba wa kuiuzia umeme wa megawati 120 Tanesco kutoka kwa Kampuni ya Richmond Development LLC ambayo baadaye iligundulika kuwa ni kampuni hewa.Serikali ilifikia uamuzi wa kusitisha mkataba huo Agosti mosi mwaka huu baada ya kuridhika kuwa mkataba huo haukuwa halali wala haukuwa na nguvu kisheria. Tangazo lililotolewa jana na kampuni hiyo lilimtaka mtu yeyote, taasisi, kampuni itakayotaka kununua mitambo hiyo ipange bei inayoona inaweza kutoa kuipata mitambo hiyo.
CHANZO: HabariLeo
0 comments:
Post a Comment