*Wajipanga kuanika siri zote hadharani
*Vocha za malipo kwa CCM kuanikwa
*Kapt. Chiligati awakana, naye awatisha
*Asisitiza hakuna kikao kilichowatuma
Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya watuhumiwa wa ufisadi kwenye Akaunti ya EPA iliyokuwa Benki Kuu (BoT) sasa wameamua kuitisha Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, uchunguzi wa Majira umebaini.
Kitisho hicho kimekuja kufuatia baadhi yao kukamwatwa na kufunguliwa kesi mbalimbali za jinai huku ikionekana kuwa wao walikuwa mawakala tu katika kupitisha fedha hizo na vigogo husika wakiwa nje.
Chanzo chetu kilicho karibu na baadhi ya watuhumiwa hao kilieleza kuwa kukamatwa, kufunguliwa mashitaka kumewadhalilisha sana baadhi yao huku wakiumia zaidi kwa kusota rumande, kwenye gereza la Keko na wale wanawake wakiweka Gereza la Wanawake Segerea.
"Jamaa ameumia sana rohoni, hata kuhangaikia dhamana alisita mwanzo baada ya kuona kwa nini ahangaike kutoa mali zake, wakati alikuwa wakala tu," kilisema chanzo chetu kilicho karibu ni mmoja wa watuhumiwa waliokwisha funguliwa kesi na akasota sana kwenye gereza la Keko.
Ingawa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikikana mara kadhaa kuhusika kunufaika na fedha hizo katika chaguzi mbalimbali, duru za uchunguzi, zinawakariri baadhi ya watuhumiwa hao wakilalamika 'kutolewa kafara.'
Ndugu mwingine wa mtuhumiwa ambaye ameshafanikiwa kwa kiasi kikubwa kulikwepa sakata la EPA, ingawa taarifa za kiuchunguzi bado zinaamini huenda akaburutwa naye kortini, aligusia kuwa kwa sababu yeye alitumiwa tu, ameandaa faili la utetezi ambalo pamoja na nyaraka nyingine, limeheheni kile alichokitaja kuwa vocha za malipo kwenda kwa baadhi ya vigogo wa CCM.
"Hapa ndipo Serikali itakapoumbuka. Kila kitu kipo. Hajakamatwa bado, ameshahojiwa na kubanwa katika shughuli zake, anasubiri tu afikishwe kortini atoe vielelezo vyake, yeye si fisadi, aliombwa asaidie shughuli halali akafanya hivyo, kwa namna anavyojiheshimu, asingeweza kusaidia akakubali wizi," kilisema chanzo chetu kilicholiona faili hilo la utetezi.
Wakati watuhumiwa hao wa EPA wakijipa 'kujiondoa katika ukafara,' Mwandishi Wetu Eckland Mwaffisi anaripoti kuwa uongozi wa juu wa CCM, umeendelea kusisitiza kuwa hawahusiki na ufisadi wa EPA.
Akitoa tamko kwa niaba ya Chama chake Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Bw. John Chilligati, alisema CCM haikuhusika na wizi huo kama ilivyodhibitishwa na ripoti ya kamati ya wanasheria.
Alisema pamoja na madai yanayotolewa na viongozi wa vyama vya upinzani, pasipo kuthibitisha madai hayo, CCM haikuchukua fedha hizo wala haikumtuma mwanachama wake au mkereketwa yoyote kwenda kuchukua fedha hizo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Bw. Chilligati alisema pamoja na orodha ya watuhumiwa wa EPA kuhusisha majina ya wanachama wa CCM ama Wakereketwa, Chama hakijahusika kumtuma bali ni kitendo cha mtu binafsi.
Hadi sasa miongoni mwa waliokamatwa kwa tuhuma za wizi wa fedha za EPA wanaohusishwa na ukaribu na vigogo wa CCM au kuwa makada ni Bw. Rajabu Maranda na mfanyabiashara, Bw. Jeetu Patel.
"Kwenye ukweli, uongo hujitenga, madai yote ya kuihusisha CCM na ufisadi wa EPA ni uongo wenye nia ya kukivunjia heshima chama chetu machoni mwa jamii pamoja na hila za kuchafua jina la chama zinazofanywa na wapinzani ambazo kamwe, hazitafanikiwa," alisema Bw. Chilligati.
Kutokana na hali hiyo, Bw. Chilligati aliongeza kuwa, baadhi ya wanachama wanaokiuka maadili hayo, isichukuliwe kwamba wanatumwa na vikao vya chama bali ni vitendo vyao binafsi na watachukuliwa hatua za kisheria na vyombo vya dola kama ilivyo kwa wahalifu wengine.
Alisema CCM, inapongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hatua alizozichukua katika kushughulikia sakata hilo.
Hadi wiki inayoanza leo, ambapo zipo tetesi za watuhumiwa zaidi kuanza kufikishwa kortini huku Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), Bw. Eliezer Feleshi akikiri kuwa bado kuna mafaili yanapitiwa, idadi ya watuhumiwa waliokwishafikishwa kortini ni 20.
Baadhi ya makampuni ambayo yameshafikishwa mahakamani ni pamoja na Money Planners, Kiloloma & Brothers, Njake Hotel, Rashhas, Mibare Farm, Changanyikeni, Bencon International, Kernel, Malta Mining, Navy Cut Tobacco na BC Grassel & Company.
Makampuni yanayosubiriwa kwa hamu na wananchi katika Mahakama ya Kisutu ni pamoja na kampuni ya Kagoda ambayo inadaiwa kuchota fedha nyingi kulikoni kampuni nyingine.
CHANZO: Majira
jamani kutoka kwa BALALI hadi kwa washtakiwa akina Esther Komu kuna maafisa wangapi wameachwa? eeeh basi bwana mi sijui ila maswali magumu lukuki
ReplyDelete