Wananchi wahoji Rais ametumia sheria gani kusamehe wahalifu?
Na Daniel Mjema,Dodoma
BAADHI ya watu nchini wakiwamo, wanasiasa na wabunge wa Bunge la Jamhuri wamepokea kwa hisia tofauti hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu suala la mafisadi wa fedha zaAkaunti ya Madeni ya nje katika Benki Kuu ya Tanzania ( EPA), huku baadhi wakisema hotuba hiyo imejaa porojo na kuongeza utata zaidi ambao umewakatisha tamaa Watanzania.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliunga mkono uamuzi huo wa Rais kuwasamehe wale waliorejesha fedha za EPA ingawa pia wapo wengine waliokataa kutoa maoni yao wakisema bado wanatafakari hotuba hiyo.
Mbunge wa Karatu, Dk Wilbroad Slaa(Chadema) ambaye pia ni Naibu Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni, aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa hotuba yake imethibitisha hana muda wa kusoma alama za nyakati na kwamba hata wasaidizi wake hawamsaidii.
Dk Slaa alisema matarajio ya watanzania walio wengi ni kwamba Rais angetaja majina ya watu au makampuni yaliyorejesha Sh69 Bilioni na kutoa ufafanuzi ya fedha zilizorejeshwa ni fedha taslimu au zinajumuisha nyumba na magari ya watuhumiwa ambao serikali ilitangaza kuyataifisha.
“Rais amefanya kosa lile lile alilolifanya alipohutubia Bunge kwa sababu tunataka kufahamu ni akina nani hawa waliorudisha fedha hiyo ni moja lakini pili hizi Bilioni 69 zilizorudishwa ni fedha taslimu au zinajumuisha mali wanazodai wamezitaifisha,”alihoji Dk.Slaa.
Dk Slaa aliongeza kusema; "Angetuambia hizo nyumba na magari ziko wapi na zina thamani gani kwa kweli Rais amezidisha utata zaidi kuliko kutoa majibu…binafsi naiona hotuba ya jana kama porojo za alinacha”.
Mbunge huyo alimtaka Rais Kikwete amwambie ni kifungu gani cha sheria kinachomruhusu kumsamehe mtuhumiwa wa kosa la jinai ambaye hajahukumiwa na mahakama akisema kinachoonekana Rais ana safiri zaidi nje ya nchi na wala hana washauri wazuri wa kumsaidia.
Alisema kama Rais angekuwa na wasaidizi makini asingeiongezea muda kamati ya mwanasheria mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika kuendelea kutafuna fedha za walipa kodi kuchunguza makampuni tisa kwa kuwa makampuni hayo yalishatangaza hakuna mtu wanayemdai Tanzania.
Hata hivyo Mbunge wa Nungwi, Ame Pandu Ame (CCM) alikataa kusema lolote kwa sasa akisema hilo ni jambo zito linalohitaji tafakuri ya hali ya juu huku Mbunge wa Same Mashariki,Anna Kilango Malecela(CCM) naye akisema kwa sasa bado anaitafakari hotuba hiyo ya Rais.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe(CHADEMA),alisema kitendo cha Rais kuwasamehe watuhumiwa wa EPA waliorejesha fedha kimewagawa watanzania kwamba watuhumiwa wakubwa wanatakiwa kurudisha walichokiiba bali wanyonge ndio wanatakiwa kufungwa.
“Watanzania wanachotaka ni kwamba warudishe wasirudishe fedha lazima washitakiwe lakini hiki alichokifanya Rais ni kibaya sana kwamba wezi wakubwa wanatakiwa kurudisha fedha lakini hawa wadogo wanafungwa magerezani…hii ni mbaya sana”alisema Kabwe.
Kabwe alisema msamaha wa Rais una taratibu zake na huwa unamhusu mtu ambaye tayari amehukumiwa na mahakama lakini alichokifanya Rais si sahihi na kusema angalau basi kamati ya Bunge ya mambo ya sheria ingearifiwa ili ijadili na kuridhia kuwasamehe watuhumiwa hao.
“Tusubiri DPP atasema nini lakini tangu mwanzo tulimshauri Rais kwamba wale wa Bilioni 90 wafikishwe mahakamani na wale wa Bilioni 42 uchunguzi wao uendelee na jana(juzi) kwa mara ya kwanza Rais ametofautisha makundi hayo mawili”alisema Kabwe.
Baadhi ya wabunge ambao hawakupenda majina yao yatajwe walipinga hatua ya Rais kuwasamehe waliorejesha fedha hizo wakisema uamuzi huo unakwenda kinyume na misingi ya utawala wa sheria ambao unatambua kuwepo kwa Mahakama katika kushughulikia wahalifu.
"Hata kama wamerejesha fedha hawa ni wezi wamegushi nyaraka wanasamehewaje? kama ni hivyo tuwaachie pia watoto wetu, ndugu zetu na wajomba zetu wanaoozea magerezani kwa kuiba kuku ni jambo la ajabu na limeleta sura mbaya sana kwa jamii,'' alidai Mbunge mmoja.
Mbunge mwingine wa viti maalumu kutoka CCM alisema alitegemea Rais angezingatia maneno ya Spika wa Bunge,Samwel Sitta aliyemtaka Rais kutowaonea huruma watuhumiwa wa EPA kwa kisingizio cha haki za Binadamu kwa sababu hicho ndicho wananchi wanachokitaka.
''Kama utakumbuka alipokuja hapa Bungeni Spika alimweleza waziwazi suala hili na maneno ya Spika ndio ambayo yaliwapa faraja sana wananchi kuliko yale ya Rais ambaye alionekana kama anaogopa kitu fulani kuhusu hawa mafisadi,” alidai Mbunge huyo.
Mbunge wa Mkwajuni, Mzee Ngwali Zubeir(CCM) alisema binafsi haoni tatizo kwa Rais kuwasamehe watuhumiwa hao kwani walipewa muda wa kujirekebisha na kufanya hivyo lakini akasema anaunga mkono kufikishwa mahakamani kwa wale ambao hawajarejesha fedha hizo.
“Nafahamu wapo wananchi ambao hawajafurahishwa na uamuzi huu wa Rais lakini wapo pia wanaona ni uamuzi wa busara nafikiri ni sahihi kuwasamehe wale waliorejesha kwa sababu walipewa muda wa kujisahihisha na wakafanya hivyo”alisema Mbunge huyo.
Masanja James mmoja kati ya wanafunzi wa chuo kikiu cha SAUT Mwanza amesema kuwa katika hotuba ya Rais amejitahidi katika kuzungumzia matatizo mengine kama yale ya mauji ya Albino, na OIC.
Alisema kuwa kulingana na utata wa sula la OIC hoja ni kuanzisha mjadala kama ambavyo rais ameeleza lakini kueleza masikitiko yake kuhusiana na suala la EPA ambalo alisema kuwa Rais bado ameonekana kuwa hatambui anachokijibu kwa wananchi.
''Amezungumza vizuri sana haya masuala mengine, lakini katika suala la EPA hapa hakutoa maelezo ya kuridhisha, kama Rais wa nchi anaweza kueleza kuwa amekuwa akipokea taarifa vipande vipande?
Kubwa ni kwamba, bado Rais hajaeleza wezi hao watashughulikiwa vipi na serikali yake kwa wizi huo, kwa mtazamo wangu ameonesha kuidhinisha wizi kwa waliolipa kurejesha kwa vile hajatwambia hatua ambayo watachukuliwa,” alieleza James.
Alisema kwa kauli ya rais katika hotuba yake wizi wa fedha za umma umeruhusiwa kwa wale wote wataofanikiwa kuiba, isipokuwa kwa wale ambao watashindwa kurejesha wao hatua zitachukuliwa.
James alieleza kuwa hali hiyo itakuza wizi katika sekta mbalimbali serikali kwa vile inaacha somo kuwa kila anayeiba vizuri akirudisha hakuna kuchukulia hatua kama ilivyo kwa wizi wa mabilioni ya EPA.
Mwajabu Bakari alisema kuwa katika hotuba ya Rais Kikwete ameghazabishwa na kuona jinsi serikali isivyo sikiliza kilio cha wananchi kutaka walioiba na kurejesha fedha za EPA wachukuliwe hatua na kusema kuwa jambo hili litalifikisha taifa mahari pabaya.
?Naye Salim Said anaripoti kuwa Mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema, amesikitishwa na kusononeshwa sana na hotuba ya Rais Jakaya kwa kuamua kufanya kazi isiyomuhusu.
''Nimesononeshwa, nimesikitishwa na nimekasirishwa sana na hotuba ya Rais, kwa kuwasemehe watu waliofanya jinai kabla ya mahakama kufanya kazi yake. Rais anaweza kusamehe, lakini hadi mahakama ifanye kazi yake. Huu ni ufunjifu wa Sheria za nchi,'' alisema Prof. Lipumba.
Alifafanua kuwa, utawala wa Kikwete ni utawala mbovu uliokosa muelekeo na unaongeza ufisadi ndani ya nchi, kwa kukosa nguvu ya kuwashughulikia mafisadi wa EPA.
''Hatuna utawala kabisa, tumekosa uongozi nchini. Hizi fedha zilituimika katika kumuingiza madarakani na ndio mana leo anakosa nguvu ya kuwashughulikia wezi hao,'' alilalamika Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba aliwataka Watanzania kujipanga na kujiandaa kwa ajili ya kuing’oa serikali ya CCM madarakani, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kabla nchi haijayoyoma.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislaam Tanzania, sheikh Ramadhan Sanze alisema, ni mfano mbaya sana kwa mamlaka ya kirais nchini kufagilia sheria kutumikia siasa jambo ambalo ni hatari kwa mamlaka nyengine za chini.
Alisema, inaonekana kuna siri nzito katika suala la wizi wa fedha za EPA kwa kuwa kuchukua fedha kinyume na taratibu ni kosa la jinai lakini rais amelichukulia kama la madai.
''Tatizo si kurudisha fedha, hapa tunataka kukomesha huu mchezo mchafu, kwa sababu kuchukua fedha visivyo ni kosa la jinai. Kwa mpango huu wa rais Kikwete kufagilia Sheria kutumikia siasa, basi watu wataendelea kukwepa sheria kwa mlango wa siasa kila siku,'' alitahadhariasha Sheikh Sanze.
Sheikh Sanze alifafanua kwamba, pamoja na juhudi kubwa anazofanya rais Kikwete katika suala la EPA, bado maslahi ya kisheria na utawala bora yamekiukwa.
''Jambo hili litawafanya Watanzania waanze kuhoji ni jinsi gani nguvu na mamlaka ya rais yananavyoshindwa kufanya kazi ya kuwashughulikia mafisadi. Jambo ambalo linatutia wasiwasi mkubwa juu ya mamlaka na nguvu hiyo,'' alisema Sheikh Sanze.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment