Friday, 21 November 2008


Asema viongozi wanakumbatia matajiri, nchi inahitaji maadili mapya ya viongozi

Na Ramadhan Semtawa

WAZIRI MKUU mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ameonya kuwa iwapo hali ilivyo sasa nchini ikiachiwa iendelee kama ilivyo, amani, umoja na utulivu vitatoweka.

Kauli ya Jaji Warioba ambaye anaheshimika kutokana na maono yake ya mara kwa mara kuhusu mwelekeo wa nchi, imekuja wakati nchi inakabiliwa na tatizo la ufisadi na migomo kutoka kwa makundi mbalimbali ya jamii.

Huku akichambua nchi ilikotoka, ilipo na inakoelekea, Jaji Warioba alionya jijini Dar es Salaam jana kwamba, hakuna tena sera ya kujitegemea bali msingi wa maendeleo ni fedha, huku utu ukitoweka kwa kasi kubwa na kwamba, hali hiyo imeibuka zaidi baada ya kuvunjwa Azimio la Arusha visiwani Zanzibar mwaka 1990.

Jaji Warioba alisema kuvunjwa kwa Azimio la Arusha kumeivuruga nchi na kutaka ifanyike tathimini ya kuunda azimio jipya ambalo litaweka miiko ya uongozi, kwani sasa nchi iko katika hali ngumu.

Akionyesha jinsi mfumo wa uongozi wa nchi ulivyovurugika baada ya kuvunjwa azimio hilo la mwaka 1967 na kuundwa Azimio la Zanzibar, alisema viongozi badala ya kuangalia wananchi wa kawaida, huamua kukumbatia matajiri na wafadhili ili waendelee kuwepo madarakani.

"Hata ukiangalia huo mfumo wa uwakilishi wa uwiano, badala ya watu kukaa na kujadili namna bora ya kufanikisha mfumo huo, kinachoonekana ni watu kutaka kuzidi kukaa katika madaraka wakifikiri majimbo ni yao," alionya.

Waziri Mkuu huyo mstaafu, alisema mbali ya kukumbatia matajiri, lakini hata maisha ya baadhi ya viongozi wa sasa na watumishi wa umma yako juu yakilinganishwa na viongozi wa zamani ambao walifanya kazi chini ya misingi na miiko ya uongozi ikiwemo ya Azimio la Arusha.

Huku akionyesha msisitizo wa hilo, Jaji Warioba ambaye alizungumza mbele ya viongozi wa vyama 17 vya siasa nchini na wawakilishi wa serikali kutoka Idara ya Utawala Bora Ikulu, katika kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia (TCD), alimtolea mfano mzee Rashid Kawawa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 15 kutoka mwaka 1962 hadi 1977, lakini maisha yake ni ya kawaida.

"Mzee Kawawa alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 15, kutoka 1962 hadi 1977, tena Waziri Mkuu Mtendaji mwenye madaraka kweli si kama Waziri Mkuu wa sasa hivi, lakini hebu nenda katafute mali zake, kaangalie nyumba yake ya Madale ni ya kawaida tu, utajiuliza hivi yale ni maisha ya mtu aliyekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 15?" alihoji na kuongeza:

"Leo hii nyumba za serikali zilizouzwa kwetu sisi viongozi, zimekarabatiwa na zinapendeza kweli, wengine wamezivunja na kujenga upya, angalia haya maisha, hata tupige kelele za ufisadi bado haya ni matokeo madogo, tuko katika hali ngumu sana."

Akichambua kipengele kimoja baada ya kingine katika Azimio la Arusha na athari zake kwa sasa baada ya kuvunjwa, alisema wakati siku za nyuma ilikuwa ni mwiko watumishi wa umma kuwa na mishahara miwili, leo hii baadhi yao wanapokea mishahara zaidi ya mmoja na pia ilikuwa ni mwiko kwa watumishi kuwa wakurugenzi au kuwa na hisa, leo wapo wanaomiliki makampuni.

Kwa msisitizo, alisema watu wanapata mishahara miwili, wapo baadhi ya watendaji serikalini wakiwemo mawaziri hawaendi kufungua semina kama hazina maslahi ya posho kubwa.

Alisema posho hizo wakati mwingine ni kubwa kuliko mishahara na kibaya zaidi ni kwamba, haikatwi kodi kama inavyofanyika katika mshahara.

Licha ya kumulika baadhi ya viongozi walio katika utumishi wa umma, Jaji Warioba alisema hata baadhi ya wabunge hupenda kuhudhuria semina ambazo zina posho huku wakilalamikia maslahi duni wakijilinganisha na wenzao wa Kenya.

"Wakati mwingine hata baadhi ya wabunge hutaka kwenda sehemu zenye posho, pia hulalamikia maslahi duni, ni kweli mkijiangalia na wenzenu wa Kenya wao wako juu sana, lakini nanyi msiangalie wale angalieni watu wa chini," alisisitiza.

Huku akiangalia zaidi athari za kuvunjwa azimio hilo kwa nchi, alisema sasa wakati kipindi cha nyuma uongozi wa nchi ulikuwa ni kwa wakulima na wafanyakazi, leo hii hakuna tena nafasi kwa watu wa kada hiyo kushika nafasi.

Alisema hata mfanyakazi au mkulima awe na uwezo mkubwa kiasi gani bado ni nadra kuweza kupata nafasi ya kuongoza kutokana na kuwepo tabaka la wafanyabiashara wenye pesa, ambalo limewatenga na kuwafanya duni watu wa chini.

Jaji Warioba alisema ni kujidanganya kufikiri kunaweza kuwepo Sheria ya Maadili, akitoa mfano kwamba Azimio la Arusha halikuwa sheria, lakini watu waliheshimu na ambao walishindwa kutii walijiondoa wenyewe kabla ya kufikishwa mahakamani.

Alisema sasa hivi maisha ya tabaka la chini yanazidi kuwa magumu hasa kwa wafanyakazi katika sekta ya umma kuwa na mishahara midogo, lakini wakubwa wakizidi kujiongezea posho na mishahara huku tabaka hilo la chini likiona, kitu alichoonya kwamba ni cha hatari.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema uamuzi wa kuandaa kongamano lenye mada hiyo linalenga kukumbusha maadili katika utumishi wa umma.

Profesa Lipumba ambaye ni msomi mwenye kuheshimika katika taaluma ya uchumi, alisema utumishi wa umma unapaswa kuegemea katika msingi wa kuangalia maslahi ya umma.

"Tumeamua kuangalia hili ili kukumbusha maadili katika utumishi wa umma, hali ni mbaya na nchi inaweza kuvurugika kama hali itakwenda kama ilivyo sasa," alionya.

Profesa Lipumba alisisitiza kwamba, kama matabaka yataendelea kwa watumishi wa chini kuishi kwa mishahara midogo huku viongozi wa juu wakijiongezea posho na mishahara mikubwa, hali itakuwa mbaya.

Kongamano hilo ambalo linamalizika leo, pamoja na mambo mengine limejikita katika kujadili maadili katika utumishi wa umma na namna bora ya kupata viongozi wa dola.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget