Tuesday, 2 June 2009


Na Lilian Lugakingira, Bukoba

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeanza safari ndefu ya kumnadi Rais Jakaya Kikwete ili awe mgombea pekee katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, na tayari wilaya ya Bukoba Mjini imetoa hundi ya Sh1milioni za kulipia fomu yake ya kuwania nafasi hiyo.

Hundi hiyo ilitolewa jana na Umoja wa Vijana wa CCM wilaya ya Bukoba Mjini kwa maelezo kuwa umeridhishwa na uongozi wa Kikwete katika kutekeleza na kutimiza ilani ya CCM, na hivyo kuungana na jumuiya nyingine, vikundi na watu mbalimbali waliojitokeza kuanza kumkapenia Kikwete.

Hata hivyo, katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliiambia Mwananchi jana kuwa hajui kwa nini jumuiya hiyo ya vijana wa chama chake imefanya hivyo na kwamba atawatafuta ili kupata ukweli na sababu za kitendo hicho.

"Niano msimamo wa chama, lakini siwezi kusema kwa sababu sijajua wamefanya nini. Bila shaka wanayo sababu," alisema Makamba baada ya kuuliza maswali mengi kuhusu kitendo hicho cha UVCCM Bukoba.

Katika halfa iliyofanyika mjini hapa, mwenyekiti wa UVCCM wa Bukoba Mjini, Chifu Kalumuna alimkabidhi mwenyekiti wa CCM wilayani Bukoba Mjini, luteni mstaafu Ally Shamte hundi ya fedha za kuchukulia fomu hizo.

Katika hafla hiyo, Kalumuna pia alimkabidhi mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki hundi ya Sh 100,000 kwa ajili ya kuchukulia fomu za kuwania ubunge katika uchaguzi huo.

Akizungumzia sababu za kutoa fedha kwa Kikwete na Kagasheki kwa ajili ya kuchukulia fomu, katibu wa vijana wa Bukoba Mjini, Yusuph Kaliat alisema wamefanya hivyo kutokana na kuridhika na ufanisi katika utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Sisi kama vijana na nguzo ya taifa, tumeamua kutoa zawadi hiyo ili viongozi hao waendelee kuongoza, kila mmoja kwa nafasi aliyokuwa nayo,” alisema Kaliat katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa wa CCM na UVCCM, akiwemo Kagasheki.

Chifu Kalumuna alikabidhi hundi zote mbili kwa Balozi Kagasheki ambaye naye alimkabidhi Shamte.Hakuna maelezo yaliyotolewa kwa nini UVCCM wilaya ya Bukoba imeamua kutoa fedha hizo sasa, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya mchakato wa uteuzi za majina ya wagombea na kuanza kampeni.

Kwa kawaida, CCM ina kipindi chake cha kuanza kampeni za ndani kwa wagombea wa nafasi zote za kuanzia serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais, lakini muda rasmi unaoruhusiwa na Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kuanza kampeni ni miezi minne kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Uchaguzi mkuu utafanyika mwezi Agosti mwaka 2010.

Kitendo cha wilaya hiyo kutoa fedha kwa ajili ya kuchukulia fomu kinaelekea kuwa ni mkakati mpya wa kumnadi Kikwete pamoja na Kagasheki, ambaye hivi karibuni alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema hatawania kiti hicho tena.

Fedha hizo za jumuiya ya vijana ya Bukoba Mjini ni sehemu ya kampeni kadhaa ambazo zimekuwa zikionekana katika miezi ya karibuni kumpigia debe Kikwete, ambaye alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Hivi karibuni Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Manyara ulimpendekeza Kikwete kuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais katika chama chao cha CCM.Umoja huo ulitoa msimamo huo Mei 30 katika mkutano mkuu wa mkoa uliofanyika kata ya Magugu wilayani Babati ambako mgeni rasmi alikuwa katibu mkuu wa UWT, Hasna Sudi Mwilima.Risala ya akina mama hao iliyosomwa na katibu wa mkoa, Venosa Mjema ilisema wamenufaika zaidi na uongozi wa Rais Kikwete tangu alipoingia madarakani mwaka 2005.

Pia mkoa wa Rukwa ulionyesha kuridhishwa na uongozi wa Kikwete katika hafla ya kuchangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa shule za mkoa huo.Katika hafla hiyo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam na ambayo mgeni rasmi alikuwa Kikwete, kiasi cha Sh 1.4bilioni kilichangwa kwa fedha taslimu au ahadi.

Wanachama wengine wa CCM waliowahi kutoa kauli za kutaka Kikwete awe mgombea pekee wa chama hicho ni pamoja na makamu mstaafu wa rais, Samuel Malecela, mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Dodoma, Pancras Ndejembi na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Dar es Salaam, Mzee Hemed Mkali.

Baada ya wazee hao kutoa kauli hiyo mapema mwaka huu, Mbunge wa Sumve, John Shibuda alidai kwamba atachukua fomu kuwania urais mwaka 2010. Shibuda pia alikuwa miongoni mwa wana-CCM 11 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 2005.

Wengine ni makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, Malecela, waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof Mark Mwandosya, Balozi Patrick Chokara, Balozi Ali Karume, Dk Abdallah Kigoda, Dk William Shija, Dk Salim Ahmed Salim na Idd Simba.

Akionekana kunogesha kampeni za chini kwa chini hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Shinyanga, Rais Kikwete mwenyewe alisema haoni sababu kwa nini akina mama waliofaidika na mradi huo wamnyime kura mwakani.

Nasema, kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kupata usingizimimi sioni kwa nini akina mama walionufaika na mradi huu waninyime kura,” alisema Kikwete huku akishangiliwa na akina mama waliofika kwenye uzinduzi
huo.

CHANZO: Mwananchi
HABARI INAYOSHABIHIANA NA HII: UWT Wamteua Kikwete Kuwa Mgombea Pekee

PENGINE NI MUHIMU KUJIULIZA HAO UVCCM WILAYA YA BUKOBA MJINI WANA MRADI GANI WA KUWAWEZESHA KUWAKIRIMU "WAGOMBEA" HAO WATARAJIWA!PENGINE UTAULIZA KWANINI NI MUHIMU.WELL,NI RAHISI SANA KWA MAFISADI KUTUMIA COVER KAMA HIYO KUJIPENYEZA KWENYE ANGA ZA KITAIFA KWA MINAJILI YA KUFISADI NCHI BAADA YA UCHAGUZI HUO.

LAKINI CHA SEHEMU MUHIMU ZAIDI KATIKA HABARI HIYO HAPO JUU NI HIYO NUKUU NILIYOI-HIGHLIGHT KWA RANGI NYEKUNDU.IT SAYS IT ALL

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget