Thursday, 25 June 2009


Hili ndio "BUNGE LENYE MENO"!Juzijuzi mbunge mmoja wa CCM kaomba Mungu alilaani Baraza la Mawaziri kwa kushindwa kutimiza majukumu yake.Mwingine kadai serikali ina ugonjwa na inahitaji maombezi (na kwa kawaida magonjwa yanayohitaji maombezi ni yale yasiyotibika kama vile ukimwi,nk).Jana mbunge mwingine wa chama hicho tawala amewafananisha mawaziri na mbwa.Na pengine moja ya mambo yatakayokumbukwa zaidi katika historia ya bunge letu tukufu ni jinsi kikao hiki cha bajeti kinavyoonekana "mwiba mkali" kwa mawaziri,at least according to walio mahiri katika kuripoti pasipo kusoma kati ya mistari (reading between the lines).

Sina maneno ya huruma kwa baadhi ya wabunge hawa wa CCM.Ni wanafiki wanaohangaika kutumia vizuri nafasi hizi za mwisho mwisho kujitengenezea mazingira ya kurejea bungeni hapo mwakani.Lakini ili haki itendeke,ni vema kuwatofautisha wanafiki hawa kwa makundi.Kuna kundi la wabunge waliojitokeza mapema (kabla hata ya joto la uchaguzi wa mwakani halijaanza kupanda) kukemea ufisadi na vitendo vingine vinavyokwaza maendeleo ya taifa letu.Sio siri kwamba wabunge kama Selelii,Kimaro,Killango,Mwambalaswa,Mwakyembe na wengineo wamejitokeza kuwa sauti adimu ndani ya CCM dhidi ya ufisadi.Na tunafahamu vituko wanavyofanyiwa na watu walewale wanaopaswa kuwaunga mkono.

Kundi la pili ni la wababaishaji walio njia panda; upande mmoja hawana nia ya dhati ya kupambana na ufisadi au pengine ni sehemu ya mfumo unaodumisha ufisadi,upande mwingine wanafahamu fika kwamba miongoni mwa ajenda za uchaguzi mkuu ujao ni ufisadi na namna wawakilishi wetu walivyoshiriki katika mapambano dhidi ya ufisadi.

Pia kuna makundi mengine mawili: la kwanza linajumuisha wababaishaji wanaokwenda bungeni kwa vile tu ndio mahala pao pa kuchuma shs 7,000,000/= za mshahara kiulaini.Hawachangii hoja,hawaongei lolote japo si mabubu,wapo wapo tu.Kuwepo au kutokuwepo kwao bungeni hakutambuliki kwa vile wanaongeza tu idadi ya wabunge.Kundi la pili ni la watetezi wa ufisadi.Hawa ni wepesi wa kuomba mwongozo wa Spika kila maslahi yao au ya wadau wenzao wa ufisadi yanapoguswa.Nadhani mmesikia "Dokta" Mzindakaya alivyotumia Maandiko Matakatifu kutetea ufisadi .Ila hawa wanaocheza na vitabu vya Mungu,nadhani ndio wanaostahili kulaaniwa zaidi kwani wamevigeuza kama manifesto za usanii wao wa kisiasa!

Uzuru wa makundi haya mawili ya mwisho-la tatu na la nne-ni kwamba angalau yanajumuisha wabunge tunaofahamu wanaposimamia.Aidha ni wazembe na mabubu wasioongea (aidha kwa aibu ya kuongea,au "heri mie sijasema",au uzembe tu) au ni watetezi wa mafisadi.Hawa si wanafiki as such kwa vile wameji-identify kwetu kuwa ni viumbe wa namna gani.

Tofauti kati ya makundi hayo ni ndogo mno contrary to inavyosomeka na kusikika kwenye vyombo vya habari.Hapa nataka kuzungumzia makundi mawili ya mwanzo-la kwanza na la pili.Hawa wote ni wana CCM,na kwa namna yoyote ile hawawezi kujitenganisha na matatizo yanayosababishwa na chama hicho tawala.Na hili si la kufikirika kwa sababu tayari wengi wa wabunge wa kundi la kwanza wamekuwa wakikumbana na kadhia mbalimbali kutokana na msimamo wao dhidi ya ufisadi,na guess what,kadhi hizo ni kutoka kwa wenzao ndani ya CCM.

Mawaziri wanaolaaniwa na kufikia hatua ya kuitwa mbwa wanatoka CCM pia.Hii sio vita ya wenyewe kwa wenyewe kama inavyoweza kutafsiriwa kiuzembe.Huu ni unafiki,period.CCM isingefika hapo ilipo laiti "wapambanaji hawa" wangekuwa na mkakati wa dhati wa kuleta mabadiliko ya kweli.Wanachofanya muda huu ni cha kibinafsi zaidi kuliko kitaifa.Wanaweza kurudi bungeni hapo mwakani baada ya wapiga kura wao "kuzugika" na CVs za wawakilishi wao tangu 2005 hadi 2010.Kurudi kwao bungeni kutapelekea CCM kuendelea kuwa yenye wabunge wengi bungeni,na hivyo kupelekea kuendelea kwa haya tunayopigia kelele kila siku.

Siamini kama kuna mkakati kwa Selelii na wenzake kuleta mageuzi ndani ya CCM.So far,kelele zao hazijasaidia kukitenganisha chama hicho na ufisadi,implying that kelele zao zimebaki kuwa kelele tu.Wana options mbili: waendelee kupiga kelele lakini wabaki kuwa sehemu ya chama kinachohusishwa na ufisadi au wajondoe ndani ya chama hicho na hivyo kubainisha kuwa kuwa kwao ndani ya CCM ilikuwa ni sehemu tu ya maisha yao ya kisiasa lakini cha muhimu zaidi kwao ni Tanzania na ustawi wa Tanzania.Yes,si lazima kuwa mbunge wa CCM ili kupata fursa ya kupigania maslahi ya taifa.Mifano hai ipo;Dkt Slaa,Zitto Kabwe,nk sio wabunge wa CCM,lakini sote tunafahamu michango yao katika kupambana na ufisadi.

Unafiki wa wabunge hao wa CCM unasababishwa na kitu kimoja kisicho na msingi: UBINAFSI WA KISIASA.Ni hivi,kwa CCM,umoja na mshikamano ndani ya chama hicho ni muhimu zaidi kuliko umoja na mshikamano wa taifa.Na hilo ni matokeo ya chama hicho kuamini kwamba ni chenyewe tu kinachoweza kudumisha mshikamano na umoja wetu.Kwa lugha nyingine,kimebinafsisha uwezo,dhamira,jitihada na nguvu za Watanzania zaidi ya milioni 35 ambao si wanachama wa chama hicho (takwimu za karibuni zinaonyesha idadi ya wanachama wa CCM ni takriban milioni 4 tu).Japo ni kweli kwamba chama hicho kimetoa uongozi uliosaidia kudumu kwa amani na mshikamano huo,Watanzania wenyewe ndio waliofanya kazi ya msingi zaidi kufanikisha hilo.Upendo na upole wetu (ambao mara nyingi umeishia kutumiwa vibaya na wanasiasa walafi) ndio sababu kuu ya kwanini tumeendelea kubaki kisiwa cha amani (kwa maana ya kutokuwa vitani).

Ni ubinafsi wa kisiasa unaopelekea CCM kuweka mbele maslahi ya kisiasa badala ya maslahi ya taifa.Sote tumeshuhudia mara kadhaa wabunge wa chama hicho tawala wakiitisha vikao "vya kuwekana sawa" kila zinapojiri hoja nzito bungeni.Kuwekana sawa kwa maslahi ya nani?Hivi cha muhimu ni hoja ipite tu au ipite ili ilete mabadiliko chanya kwa wananchi?

Lakini ili upate mfano sahihi zaidi kuhusu ubinafsi wa wabunge hawa ni pale Dkt Slaa alipotamka bayana kwamba mishahara ya wabunge ni mikubwa mno kulinganisha na hali halisi ya uchumi wetu.Kwa umoja wao (huku wakipata sapoti kutoka kwa wabinafsi wengine waliojificha kwenye vyama vya upinzani) walimzomea Dkt Slaa na kumzongazonga kana kwamba kawatukana.Hivi ina maana wabunge hawa wanaotuzuga kuwa wanatetea maslahi yetu hawaelewi kuwa wakati wao wanazawadiwa takriban shilingi 7,000,000/= mwezi (wastani wa shilingi laki 230,000/= kwa siku sawa na takriban shs 10,000/= kwa saa) takriban Watanzania 36,000,000 wanaoishi kwa chini ya shilingi 3000/= kwa siku?

Hadi kufikia tamati yake na mabiloni kadhaa kutumika,kikao hiki cha bajeti kitashuhudia kila aina ya vituko kutoka kwa wanafiki hawa.Ukidhani hizo dua dhidi ya mawaziri na "matusi" ya kuwaita mbwa ndio hatua kali kabisa,subiri usikie "makombora" zaidi.Na kama kawaida ya vyombo vyetu vya habari,kurasa zitapambwa na maneno mazito kama "Bunge moto juu","Wabunge wachachamaa",na ubabaishaji mwingine kama huo.Lakini pamoja na yote hayo,makadirio ya wizara za mawaziri wanaoombewa dua mbaya na kuitwa mbwa yatapitishwa na wabunge haohao wanaotuzuga kuwa "wana hasira na mawaziri".

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget