Saturday, 27 June 2009


Kifo!

Yaani,licha ya kumaanisha mwisho wa safari ya uhai wa binadamu,kifo huambatana na matukio ya ajabu kabisa ambayo pengine yangepelekea tifu laiti marehemu angeweza kuyasemea.Nikupe mfano hai.Kabla ya kukutana na mauti,marehemu mama yangu aliugua kwa takriban miaka mitatu.Japo kwenye mambo ya imani za kidini tunaambiwa uzima na uhai ni mipango ya Mungu,mara kadhaa mikono ya binadamu wenzetu huhusika kuharibu au kutokomeza kabisa uhai wa binadamu wenzao.Maelezo ya kitabibu yalitufahamisha kuwa marehemu mama alifariki kutokana na sehemu kubwa ya ubongo wake kuathiriwa na mishtuko ya moyo (strokes) miwili aliyopata wakati wa uhai wake.

Mshtuko wa kwanza ulichangiwa na kitendo cha mtu wa karibu na marehemu.Alimfanyia tendo ambalo lilimwacha marehemu akisononeka hadi anaingia kaburini.Ni hadithi ndefu,na kwa vile pengine hapa si mahala mwafaka kuweka kila jambo wazi,nachoweza kukielezea ni namna mhusika huyo (alomtenda ubaya mama hadi akaishia kupata mshtuko wa kwanza wa moyo) "alivyojibaraguza" wakati wa mazishi ya mama Juni 2,2008.

Kuna takriban nyakati tatu hivi katika msiba ambazo kwa hakika zinatia uchungu usioelezeka.Kwangu,kwanza ilikuwa ni wakati wa taarifa kuwa "mama yako amefariki".Kwanza unaona kama ni utani,kisha inakuwa kama ndoto,lakini pindi akili inapofunguka na kugundua si utani wala ndoto,hapo ni bwawa la machozi,sambamba na mayowe ya kilio,na wengine huishia kumfuata wanayemlilia (kifo kinazaa kifo kingine).Pili ni wakati wa kuona maiti,aidha mortuary au wakati wa kuaga maiti kabla ya mazishi.Yaani hapo kumbukumbu zote za uhai wa marehemu zinakurejea.Tatu ni wakati wa kutumbukiza jeneza kaburini na kisha kufukia kaburi.Maneno "wewe xxx (jina la marehemu) mavumbini ulitoka,na mavumbini utarejea" (kwa sie Wakristo) ni machungu na yanaumiza mno!

Nirejee kwenye matukio ya siku ya mazishi ambayo laiti marehemu angeweza kusema lolote muda huo...!Tukiwa makaburini,yule kiumbe niliyemtaja awali kuwa alimtendea mama kitu kibaya kilichopelekea stroke alikuwa ameshikiliwa na watu wawili wakimdhibiti asijitumbukize kaburini!Yaani ungedhani ndio mtu mwenye uchungu mkuuuubwa kuliko hata sie wengine tuliokuwa tunajitahidi kujikaza japo kwa shida.Kwa sekunde kadhaa nilibaki nimeduwaa nikishangaa usanii wa mnafiki huyo.Huyu ni mtu aliyemchukia marehemu mama hadi siku anafariki,sasa iweje leo apandwe na uchungu kiasi cha kutaka kuingia na mama yangu kaburini?Laiti ningekuwa na bastola muda huo pengine saa hizi ningekuwa jela!

Hilo ni tukio la kweli.Ukitaka kushuhudia unafiki wa daraja la kwanza,nenda msibani.Sio kila chozi linalotiririka na yowe linalopigwa ni matendo ya dhati.Kuna wanaolia kutimiza wajibu na wengine "kuua soo".Utamliliaje mtu ulokuwa unamchukia wakati wa uhai wake?How come mauti yawe na thamani zaidi ya uhai?Au hayo yanafanyika kwa vile marehemu hawezi kuamka na kumsuta mtu?

Twende kwenye kifo cha Michael Jackson.Moja ya mambo yatakayokumbukwa zaidi kuhusu msanii huyu ni kipaji chake cha muziki kilichopelekea kupachika "cheo" cha mfalme wa pop duniani.Lakini ni jambo lisilofichika kwamba kwa miaka kadhaa kabla ya kifo chake hapo juzi,Michael alikuwa maarufu zaidi kwa vituko kuliko muziki wake.

Marehemu huwa hasemwi vibaya,na hiyo ni sehemu ya unafiki wa wanadamu wengi.Yayumkinika kusema kwamba Michael,kabla ya kesi ya udhalilishaji wa watoto,aliwapa kisogo watu weusi.Alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kutafuta "uzungu" (kuwa mtu mweupe zaidi ya rangi ya mwili).Alipokumbwa na kesi hiyo,sapoti kubwa haikutoka kwa Weupe wenzake" bali Weusi ambao walifumbia macho dharau ya mfalme huyo wa pop dhidi ya asili yake.

Wapo wanaoona kifo cha msanii huyo mahiri kilikuwa kikijijenga kadri siku zinavyokwenda mbele.Hauhitaji kuwa mtaalam wa mwili wa binadamu kugundua kuwa transformation ya Michael kutoka mtu mweusi kuwa mweupe zaidi ya weupe wa kawaida ingeweza kuhatarisha afya yake.
Kulikuwa na tetesi kuwa alikuwa na kansa ya ngozi,just like tetesi kwamba kuna wakati pua yake "iling'oka"!Ukichanganya na vituko kama kumning'iniza mwanae katika dirisha la chumba kilicho juu ghorofani,kuficha sura yake na masks za ajabu ajabu,nk ni dhahiri kuwa alikuwa anajitengenezea njia ya mkato ya kumrejea Muumba.


Hata hivyo,ni muhimu kutambua kuwa kuna watu waliomfikisha Michael hapo alipofia.Inaelezwa kuwa mwanamuziki huyo alikuwa mhanga wa manyanyaso dhidi ya watoto yaliyokuwa yakifanywa na baba yake mzazi.Japo mzee huyo,Joe Jackson, alionekana kuwa bega kwa bega na mwanae wakati wa kesi yake (Michael) lakini hiyo haikusaidia kukwepa hisia za baadhi ya wachambuzi wa tabia waliokuwa wakimtuhumu kuwa ndio chanzo cha "kuharibika" kwa mwanae.

Yote katika yote,kwa vile wengi wetu tumemfahamu Michael kutokana na kipaji chake cha muziki,huku tukielezwa kwamba huenda kifo chake kimetokana na overdose ya painkillers alizokuwa akitumia ili arejee jukwaani kutuburudisha,ni dhahiri kwamba historia itamtendea haki ya kuendelea kumheshimu kama MFALME WA POP!Na katika hilo,kuna kila dalili kwamba atarejea kwenye chati za muziki duniani kutokana na kupanda kwa mauzo ya albamu zake kama sehemu ya kumbukumbu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget