Sunday, 14 June 2009


Majuzi,Watanzania wametahadharishwa kuhusu athari za mdodoro wa uchumi wa dunia na madhara yake kwa nchi yetu.Kadhalika,bajeti ya mwaka ujao wa fedha imeandaliwa kwa kuzingatia tahadhari hiyo huku kukitangazwa mpango wa kuchochea uchumi (economic stimulus plan).

Hata hivyo,kama nilivyojadili HAPA,uwezekano wa bajeti na stimulus plan hiyo kufanikiwa,sambamba na umuhimu wa tahadhari iliyotolewa,utategemea zaidi hatua kali na za makusudi dhidi ya ufisadi na mafisadi.Yayumkinika kubashiri kwamba pamoja na imani kwamba mipango hiyo inalenga kulinusuru taifa,wanaufaika wakubwa wanweza kuwa mafisadi wanaojua vema namna ya kubuni mikakati ya ulaji huku wakiwa hawana hofu ya kuchukuliwa hatua yoyote kutokana na siasa za kulindana na kishkaji.

Hebu soma kwanza habari ifuatayo,kisha tujadili kidogo mwishoni.

Wingu zito fedha za EPA
• Chegeni: Zimekwenda kusikojulikana

na Mwandishi Wetu

UTATA umegubika mahali zilipo na matumizi ya fedha zilizorejeshwa na kampuni zilizoshiriki katika wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akilihutubia Bunge mjini Dodoma Agosti mwaka jana, alibainisha fedha hizo zilizorejeshwa na baadhi ya kampuni si mali ya serikali lakini zitawekwa kwenye akaunti maalumu kabla ya kupelekwa katika Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kufungua dirisha dogo la kuwakopesha wakulima wakati nchi ikielekea katika mchakato wa kuanzisha Benki ya Kilimo.

Ingawa Rais Kikwete na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kwa nyakati tofauti walieleza kuwapo kwa fedha hizo katika akaunti maalumu, taarifa ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata zinasema hadi sasa fedha hizo hazijaingia katika Benki ya TIB, licha ya kuwapo kwa taarifa kuwa fedha hizo zimetumika kununulia mbolea iliyotolewa kwa mfumo wa vocha kwa baadhi ya wakulima hapa nchini.

Chanzo kimoja cha habari kilichomo ndani ya TIB kimedai fedha hizo wamekuwa wakizisikia kupitia katika vyombo mbalimbali vya habari kutoka kwa wanasiasa, ambao wamekuwa wakijinadi kuwa fedha hizo zitatumika kunyanyua kilimo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa hadi sasa dirisha la kilimo lililosemwa bado halijaanza kufanya kazi iliyotarajiwa, ingawa maneno ya watu mbalimbali yamekuwa yakibainisha kuanza kazi kwake ambako kungetarajiwa kuwasaidia wakulima kupata mikopo ya muda mrefu, baada ya kuikosa fursa hiyo kwa kipindi kirefu kutokana na kutokopeshwa na taasisi za fedha za hapa nchini.

“Haya mambo huwa tunayasoma, kuyasikia na kuyaona kwenye hivyo vyombo vyenu vya habari, lakini kwenye makaratasi hali ni tofauti, sasa sijui niseme siasa inatawala au muda bado haujafika,” kilisema chanzo hicho.

Tanzania Daima Jumapili, ilifanya juhudi za kumtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Peter Noni, ambaye ameteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete, lakini Ofisa Mwanadamizi wa Mambo ya Uhusiano wa benki hiyo,Catherine Magambo, alisema mkurugenzi wake hawezi kutoa ufafanuzi hivi sasa, kwa kuwa ameanza kazi siku si nyingi na ni busara akapewa wiki moja ili aweze kujipanga.

Catherine, alipotakiwa kueleza kama ana taarifa zozote za kutokuwapo kwa fedha zilizoahidiwa na rais kupelekwa katika benki hiyo, alisema anachokifahamu ni kile kilichoelezwa wakati fulani na Mkurugenzi aliyestaafu, William Mlaki, kuwa hawajapokea fedha hizo na kama kungekuwa na mabadiliko vyombo vya habari vingejua kama walivyofanya hapo awali.

“Nyinyi Tanzania Daima Jumapili, habari kama hii unayoniuliza au unayotaka mkurugenzi wangu akujibu, najuakwamba hakuna kitu ambacho kimebadilika lakini kama mnataka habari zaidi msubiri mkurugenzi mpya azoee ofisi kwa muda wa wiki, halafu ndipo uje kumuuliza maswali yako,” alisema Magambo.

Pia alibainisha kuwa hajaona mabadiliko yoyote juu ya ahadi iliyotolewa pia na Rais Kikwete ya kutoa kiasi cha sh bilioni 15 kwa ajili ya kuendeleza benki hiyo ili iweze kutoa mikopo kwa wakulima.

“Jamani maswali yenu mbona yamezidi, si nimewaambia hakuna mabadiliko na hayo maswali yenu msubirini mkuu? Mbona mnanibana kwa mambo nisiyo na uwezo wa kutoa majibu? Kwani kila ofisi ina utaratibu wake,” alisema Magambo.

Wakati fedha hizo zikionekana kugubikwa na utata, baadhi ya watu wamekuwa wakiiona hatua ya serikali kutangaza kurejeshwa kwa fedha hizo ni kiini macho au zimetumika katika matumizi mengine badala ya kupelekwa katika kilimo kama ilivyoahidiwa, kwa kuwa viwanda vingi vya mbolea kwa mwaka huuvimejikuta vikishindwa kujiendesha baada ya kuzalisha bidhaa hiyo na kukosa wanunuaji.

Dhana hiyo inachagizwa na baadhi ya wakulima ambao wamekuwa wakilalamikia kutokupata mbolea hiyo, licha ya serikali kutangaza kutenga fungula fedha kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kukuza kilimo na kuleta mapinduzi ya kijani.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na wanasiasa mbalimbali wa hapa nchini walikuwa wakihusisha wizi huo wa fedha na mkakati maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwaagiza baadhi ya makada wake na wanachama wakwapue fedha hizo kwa ajili ya matumizi ya kampeni za uchaguzimkuu wa mwaka 2005 uliokiwezesha chama hicho kuibuka na ushindi wa ‘kishindo.’

Hisia hizo zilipata nguvu baada ya kuwapo tetesi kuwa kampuni iliyochota kiasi cha sh bilioni 40 ya Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, inadaiwa kumilikiwa na baadhi ya vigogo wa chama hicho, jambo lililochangia ugumu wa kukamatwa kwa wamiliki wa kampuni hiyo ambayo inaaminika ndiyo iliyosuka mpango wa uchotaji wa fedha hizo.

Tuhuma hizo mara kadhaa zimekuwa zikikanushwa na viongozi waandamizi wa chama hicho, akiwamo Katibu Mkuu wake, YusufMakamba, ambaye aliweka bayana kuwa CCM haijamtuma mwanachama wake afanye wizi huo na kama kuna mwanachama amehusika na wizi huo apewe lawama hizo binafsi na si chama.

Naye Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, katikati ya wiki alinukuliwa na vyombo vya habari mjini Dodoma akisema kuwa fedha za EPA zinaonekana kwenda sehemu zisizoonekana kirahisi kwa wananchi, ingekuwabusara kama zingetumika katika ujenzi wa barabara ambayo ingepewa jina la EPA, ili kila
mwananchi aweze kuamini kinachosemwa na viongozi wa serikali.

Alisema mazingira ya fedha hizo tangu awali yalionyesha utata, hivyo ingekuwa busara hata matumizi yake yakafanyika bila kuwapo kwa usiri, ili kuondoa fikra potofu kuwa hakuna fedha iliyorejeshwa.

“Hizi fedha za EPA mimi nafikiri zingetumika kujengea barabara na tukaziita barabara za EPA, ili yeyote anayetaka kuzusha lake ashindwe kufanya hivyo au tumuonyeshe vithibitisho,” alisema Chegeni.

Alisema sekta ya kilimo ni pana na hata fedha zinazotumbukizwa huko ni lazima ziandaliwe mipango mizuri na mapema ili ziweze kufikia walengwa na zilete tija inayotakiwa kuliko inavyoonekana sasa ambapo serikali inasema imetoa mbolea ya ruzuku kwa wingi, lakini wakulima wanalalamika kutoipata mbolea hiyo kwa kiwango kinachohitajika.

Wizi wa fedha za EPA ulibainika baada ya Kampuni ya ukaguzi ya kimatifa ya Ernst &Young kubaini wizi wa sh bilioni 133, ambapo baada ya uchunguzi huo, Rais Kikwete aliamua kumfukuza kazi aliyekuwa Gavana wa benki hiyo, marehemu Daudi Ballali na kuagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi kwa maofisa wa benki hiyo ili kufikishwa mbele ya vyombo vyasheria.


CHANZO: Tanzania Daima.

Katika mazingira kama haya,itakuwa kosa kweli kuyamkinisha kwamba hiyo stimulus plan inaweza kuishia kutengeneza dili ya kuifanya EPA ionekane "cha mtoto"?

Halafu,habari hiyo hapo juu ina kitu kingine cha ziada,nacho ni kuhusu PETER NONI.Huyu jamaa anahusishwa kwa karibu na skandali la EPA.Awali wasiwasi wangu ulikuwa kwenye kuteuliwa kwake kuwa Mkurugenzi wa TIB.Kilichonifumbua macho katika habari hii ni ukweli kwamba marejesho ya fedha za EPA yalipangwa kupelekwa TIB.You see the connection?NONI anahusishwa na ishu ya EPA kwa wadhifa aliokuwa nao BoT.Sasa anapokwenda TIB ambako tunaambiwa ndiko zitakapopelekwa marejesho ya fedha za EPA ni mithili ya "kula denge" kuelekea lilipo fungu hilo.

Ndio Tanzania yetu hiyo!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget