Tuesday, 23 June 2009


Na Ramadhan Semtawa, Dodoma

SERIKALI imesisitiza kuwa haiwezi kuruhusu suala la kampuni ya Buhemba Goldmine (Meremeta), kujadiliwa hadharani kwa kuwa inahusu mambo ya usalama wa taifa, lakini ikaeleza kuwa suala la ukaguzi wa Mwananchi Gold linasubiri wakati mwafaka kwa kuwa kwa sasa inafilisiwa.

Kauli hiyo ilitolewa Bungeni jana na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari wakati akijibu swali la mbunge wa Karatu, Dk Willbrod Slaa, aliyetaka kujua sababu za kampuni hizo kutokaguliwa.

Kauli hiyo pia imetolewa siku moja baada ya kuripotiwa kwa taarifa kuwa, Bunge limemwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kuyakagua mashirika hayo tata yanayohusishwa na upotevu wa mabilioni ya fedha za walipakodi.

Swali hilo lilitakiwa kujibiwa Ijumaa iliyopita, lakini Spika Samuel Sitta aliliahirisha hadi jana.

Akitoa majibu ya serikali, Waziri Sumari alisema msimamo kuhusu Kampuni ya Meremeta ulishawekwa bayana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa kikao cha Bunge cha mwaka jana aliposema kuwa, suala hilo haliwezi kujadiliwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kwa sababu linahusu usalama wa nchi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema yuko tayari kusulubiwa kuliko kuizungumzia Meremeta kwa kuwa inahusu usalama wa taifa.

Waziri Sumari alirejea kauli hiyo ya Pinda akitaka iheshimiwe na kwamba asingeweza kueleza chochote kuhusu Meremeta na badala yake angetoa majibu ya Kampuni ya Mwananchi Gold peke yake.

Hatua hiyo ya serikali kutangaza uamuzi huo inaonekana kwenda kinyume na Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2008 inayompa CAG, ambaye anawajibika kwa Bunge, mamlaka ya kufanya ukaguzi bila ya kuagizwa.

Sumari pia alisema: “Makampuni mengine yote yenye uhusiano na Maremeta kama alivyosema mheshimiwa waziri mkuu hayatajadiliwa hadharani na serikali haioni sababu ya kufanya ukaguzi."

Baada ya majibu hayo, Dk Slaa alisimama tena kuulizwa swali la nyongeza na kudai kuwa hakuwa amejibiwa chochote na wakati akiendelea kuuliza kuhusu Meremeta, Spika Sitta alisimama na kumzima.

“Mheshimiwa Dk Slaa, suala la Meremeta linahusu jeshi. Tulikaa kwenye Kamati ya Uongozi tukakubaliana kwamba suala hili lisizungumzwe hadharani. Waziri Mkuu alishalisema; nafikiri na wewe ulikuwepo, kwa hiyo sitakuruhusu kuuliza chochote kuhusu Meremeta. Uliza makampuni hayo mengine ya Mwananchi Tangold," alisema Spika Sitta na kuipa serikali ahueni.Lakini Dk Slaa akajibu na kusema: “Siulizi Jeshi, nauliza wizi.” Lakini Sumari akamjibu kwa kusema: "Na wewe pia (Dk Slaa) tafuta hoja nyingine..."

Taarifa zinadai kuwa, Meremeta ni kampuni ambayo ilianzishwa ikimilikiwa kwa asilimia 50/50 baina ya serikali na kampuni ya Trinnex na kuna tuhuma kuwa Benki Kuu (BoT) ililipa zaidi ya Sh155 bilioni kupitia benki moja ya kigeni bila ya kufuata taratibu, kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi ya CAG ya kipindi kinachoishia Juni 30, 2006.

Kuhusu Mwananchi Gold, Sumari, alisema kwa sasa iko katika mchakato wa kufilisiwa.Hata hivyo, alisema ni mapema mno kuzungumzia mchakato huo, bali alitaka wabunge, akiwemo Dk Slaa kuvuta subira na muda mwafaka utakapofika wataelezwa.

Mwishoni mwa wiki, CAG aliiambia Mwananchi kuwa amepata barua kutoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma inayomtaka azikague kampuni hizo tata, lakini akasema bado hajapanga ataanza lini kuzikagua.

Barua hiyo yenye kumbukumbu BC.50/155/06/98 inamtaka CAG afanye ukaguzi maalumu ili kubaini thamani ya mtaji na hisa za serikali katika makampuni hayo tata na pia aieleze kamati sababu za kampuni hizo kutokaguliwa.

Awali, Dk Slaa alimuuliza Waziri wa Fedha na Uchumi ni sababu gani za msingi zilizofanya kuchukua muda mrefu kuanza ukaguzi kwa kampuni hizo hata pale tuhuma hizo zilizopigiwa kelele na jamii na hata kamati mbalimbali zilizoundwa kuchunguza tuhuma hizo.

Katika swali hilo namba 76, Dk Slaa alisema kwa kuwa katika hotuba ya waziri mkuu kivuli kwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), aliyoitoa bungeni Juni, 2007, alieleza juu ya ubadhirifu mkubwa uliofanywa kwa kutumia makampuni ya Meremeta na Tangold.

Dk Slaa alifafanua kwamba ubadhirifu huo ulibainika kwenye Makampuni ya Mwananchi na Deep Green Finance Co, ambao kiasi kinachodaiwa kufanyiwa ufisadi ni zaidi ya Sh215 bilioni.

Alihoji: “Ni lini kampuni hizo zitafanyiwa ukaguzi maalumu kama ilivyofanyika kwa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ili kubaini ubadhirifu huo uliohusisha uhamisho wa fedha kutoka Benki Kuu (BoT) na vyombo vya umma kupitia NBC Corporate Branch DSM na Ned Bank ya Afrika Kusini.

Akizungumzia majibu hayo ya serikali, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe alisema serikali imepotoka.Zitto alisema CAG anawajibika kwa bunge na si serikali kwa kuwa ndiyo inayokaguliwa. "Serikali ndiyo inakaguliwa na CAG, huyo waziri kakosea kusema serikali haijaamua kufanya ukaguzi huo," alifafanua Zitto.

Zitto aliongeza kuwa kauli hiyo ya waziri ni sawa na kutangaza kujiingiza katika mgogoro na bunge kwa kuwa CAG anafanya kazi kwa niaba ya bunge.Utata mkubwa uliopo Meremeta ambayo inamiliki mgodi wa dhahabu wa Buhemba, pamoja na tuhuma za ufisadi ni utata wa wanahisa.Wakati serikali ikisema kampuni hiyo inahusu masuala ya ulinzi na usalama wa nchi, ndani yake kuna wanahisa ambao ni kampuni ya Uingereza ya British Law Associate.


CHANZO: Mwananchi

Related Posts:


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget