Monday, 27 October 2008


CCM haihusiki na OIC-Msekwa

27 Oct 2008
By Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeukana mpango wa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) na kusema kwa hilo vyombo vya habari na maaskofu wanakionea. 

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, alisema suala la kujiunga na OIC limo mikononi mwa Serikali na CCM haihusiki. 

``Mbona mnanionea jamani, kwa kweli kuniuliza juu ya jambo hili mnatuonea. Suala la kujiunga na OIC sio la CCM na wala aliyesema maneno hayo sio mimi wala kiongozi wa Chama,`` alisema. 

Pamoja na Msekwa kuukana mpango huo, lakini maamuzi makubwa yanayohusu nchi hayawezi kuamuliwa na serikali bila chama tawala kutoa baraka zake. 

Hata hivyo, Msekwa alisema hawezi kuingia kwa undani kujibu kauli iliyotolewa na maaskofu 58 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwamba watauangalia upya uhusiano wao na Serikali pamoja na Chama tawala, iwapo mipango wa kuiingiza nchi katika jumuiya hiyo pamoja na kuruhusu kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi itaendelea. 

Alisema hawezi kuamini kwamba ni kweli maaskofu walitoa kauli hiyo, kwa vile katika mkutano huo yeye hakualikwa na wala hakuhudhuria. 

Alipoulizwa kwamba Serikali inaweza kuchukua uamuzi mkubwa kama huo (wa kujiunga na OIC) bila kupata baraka ya Chama tawala, Msekwa alizungumza kwa hasira huku akilalamika kwamba maswali hayo yana lengo la kumuonea. 

Hivi aliyetoa kauli ya OIC ni mtendaji wa Serikali au mtendaji wa CCM? alihoji na kuongeza: Unataka ufafanuzi juu ya uhalali au ubaya wa hicho unachouliza, tafadhali muoneni huyo huyo aliyesema, Chama hakihusiki, mbona mnaendelea kunisakama kwa jambo nisilolijua. 

Msekwa alisema anaamini Serikali ina majibu mazuri na yenye uhakika kwa vile haiwezi kufanya jambo ambalo halina maslahi. 

Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Kamillius Membe, aliwaambia waandishi wa habari kuwa suala la kujiunga na OIC halina madhara kwa taifa. 

Kauli hiyo iliamsha wasikwasi wa maaskofu ambao licha ya kukemea kauli ya Membe na kumtaka ajiuzulu, pia walisema kitendo hicho ni uvunjaji wa Katiba ya nchi na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa. 

Hata hivyo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilipinga kauli ya maaskofu kwa kupitia kwa Kaimu Mufti, Sheikh Suleiman Gorogosi, kuwa inalengo la kupotosha. 

Wakati huo huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeunga mkono mpango wa Serikali ya Muungano wa Tanzania wa kutaka kujiunga na OIC kwa kuwa itasaidia juhudi za kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wake. 

Tamko hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alipokuwa akizungumza mjini Zanzibar baada ya kujitokeza kwa tofauti kati ya taasisi za kidini dhidi ya uamuzi wa Serikali ya Muungano. 

``Zanzibar tunaunga mkono uamuzi wa Serikali ya Muungano wa kufikiria Tanzania kujiunga na OIC kwa vile suala hilo halihusiani na mambo ya dini na litanufaisha jamii katika ustawi wa maendeleo, alisema Hamza. 

Alisema ndio maana Zanzibar imekuwa ikitetea kila mara Tanzania ijiunge na Jumuiya hiyo kwa vile misaada na mikopo inayotolewa na OIC ikiwemo miradi ya elimu na huduma za kijamii itanufaisha Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za imani ya dini. 

Alisema kuna mataifa mengi yaliyojiunga na Jumuiya hiyo licha ya nchi hizo kuwa na waumini wachache wa dini ya kiislamu na kuzitolea mfano nchi hizo kuwa ni Uganda na Msumbiji ambazo tayari zimeshanufaika na mfuko wa maendeleo wa OIC katika sekta za elimu, afya na viwanda. 

Akizungumiza suala laMahakama ya kadhi,, Waziri Hamza alisema wananchi waondoe hofu kwa vile mahakama hiyo si jambo geni kutokana na mfumo huo kuwepo visiwani Zanzibar bila ya kuathiri madhehebu mengine ya dini. 

Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi, amesema kunahitajika meza ya mazungumzo itakayokutanisha makundi yote ya Watanzania kujadili masuala mazito yanayowakabili kama kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na la kujiunga na OIC. 

Akizunguza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mvungi alisema malumbano yaliyozuka hivi karibuni, na ambayo bado yanaendelea yanaonyesha dalili mbaya kwa mustakabali wa kitaifa. 

Alisema matatizo yaliyopo nchini, yanasababishwa na mambo mengine, lakini lililokubwa zaidi ni ile tabia ambayo imejengeka nchini kwamba hakuna anayetaka kumsikiliza mwenzake. 

``Hoja kama OIC au Mahakama ya Kadhi zinatakiwa zijadiliwe kwa lugha ya utaifa, pande zote zinazohusika zikutane, zikae pamoja na zijadiliane kwa maslahi ya kitaifa, tuache pembeni dini zetu, kabila zetu na koo zetu,`` alisema na kuongeza ``Katika mambo mazito kama yanayoendelea nchini lazima utaifa utangulizwe mbele, vinginevyo tutaishia kulumbana na kugombana lakini hatutapata jawabu la matatizo yetu, alisema. 

SOURCE:Nipashe

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget