WALIMU wa Mkoa wa Dar es Salaam jana walimshambulia kwa kumrushia mawe, chupa za maji, viti na meza, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania nchini (CWT), Gratian Mukoba, kwa madai kuwa amewasaliti kwa kukubali kuahirisha mgomo wao, uliotarajiwa kuanza leo nchi nzima.
Tafrani hiyo ambayo inazidi kuliingiza taifa katika sura mpya ya migomo ya wafanyakazi nchini, ilitokea jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee wakati walimu hao walipokutana kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mwisho ya mgomo wao waliodai kuwa usingekuwa na kikomo, wenye lengo la kuishinikiza serikali iwalipe malimbikizo yao, yanayofikia zaidi ya sh bilioni 16.
Kikao hicho kilianza majira ya saa nne asubuhi na kuhudhuriwa na maelfu ya walimu kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na wawakilishi wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza.
Mwanzoni mwa kikao hicho kilichovunjika kutokana na vurugu hizo, walimu walikuwa watulivu kwenye viti vyao, kusikiliza kauli za viongozi wao, hasa Mukoba aliyekuwa akizungumzia hatima ya mgomo huo.
Ilipofika majira ya saa 6:20 mchana, Mukoba alishika kipaza sauti na kuanza kutoa tamko la chama hicho kwa nchi nzima kwamba mgomo wao ambao ulipangwa kuanza leo, umeahirishwa.
Huku baadhi ya walimu wakianza kunyanyuka kwenye vitu vyao na kutoa kelele za miguno iliyosikika kila kona, Mukoba alisema CWT imelazimika kuahirisha mgomo huo baada ya kushauriana na Mwanasheria wao, Gabriel Mnyele, aliyewataka waahirishe ili wapate nafasi ya kukata rufaa kupinga amri ya Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi, iliyozuia mgomo huo usifanyike leo.
“Kwa tamko hili ninalolisoma hapa mbele yenu, mgomo unaahirishwa kwa nchi nzima, hadi mwanasheria wetu atakapotujibu baadaye kutokana na zuio la mahakama lililotolewa jana (juzi),” alisema Mukoba.
Mara baada ya kutoa kauli, huku akiendelea kusoma maazimio mengine, ghafla umati wa walimu ulisimama kutoka kwenye viti vyao na kuvamia meza kuu, huku baadhi wakiipindua na kusababisha viongozi wa CWT kumwagikiwa maji yaliyokuwa juu za meza yao.
Kama hiyo haitoshi, baadhi ya walimu walianza kurusha chupa za maji na viti kwenye meza kuu, kwa lengo la kuwapiga viongozi wao, hasa Mukoba, aliyeonekana kushambuliwa zaidi.
Tafrani hiyo ilidumu kwa takriban dakika 35 ndani ya ukumbi huo uliokuwa na kelele nyingi za kuzomea, huku maofisa usalama wakilazimika kufanya kazi ya ziada kumwokoa Mukoba na viongozi wenzake, waliotaharuki kutokana na kushambuliwa huko.
Vita ya kurusha makopo, chupa za maji na viti iliposhika kasi, Mukoba na wenzake waliamua kukimbilia kwenye moja ya kona za ukumbi huo kujisalimisha, lakini hali hiyo haikuwasaidia, kwani walizidi kushambuliwa kwa kurushiwa vitu kama vibaka.
Tukio hilo lililoonekana kama filamu, mbali ya kuwapo kwa mashambulizi ya kurusha vitu, pia baadhi ya walimu walitoa lugha chafu kuwatukana viongozi hao na kuwataka wajiuzulu mara moja kwa madai kuwa wamewasaliti.
“Leo hatuwaachii, ama zenu ama zetu, walimu tumeonewa, tumedhalilishwa na kuibiwa vya kutosha na wewe Mukoba funga mdomo wako hapo mbele, tena katisha kusoma hilo tamko lako la kilaghai…sasa leo tutakufunza adabu kwa kukucharaza bakora ili ukome tabia hii ya usaliti.
“Kama ulikuwa unajua unakuja kutusomea hilo tamko la kipuuzi, kwanini usingeenda kwenye vyombo vya habari ukautangazie umma, kuliko kutuita hapa ukumbini kuja kutueleza ujinga kama huu…sasa leo utatujua sisi ni nani,” walisikika baadhi ya walimu wakitoa kauli hiyo.
Wakati vurugu hizo zikiendelea, majira ya saa 7:20 mchana makachero wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shirogile, Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa kipolisi Ilala, Mkumbo na makachero zaidi ya 20, wakiwa na gari tatu aina ya Land Rover ‘Defender’, walifika eneo hilo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Makachero hao, walifanikiwa kuwatorosha viongozi hao kupitia mlango wa nyuma, huku baadhi ya walimu, nao wakitoka nje, kuangalia mlango uliolengwa kutumika kumtoa Mukoba na wenzake.
Wakiwa wanajipanga kumtorosha Mukoba kupitia mlango wa nyuma na kutaka kumwingiza kwenye gari la Polisi badala ya ‘Shangingi’ alilokuja nalo, walimu walibaini hali hiyo na kuamua kusogea karibu na gari hilo bila kuogopa vitisho vya polisi waliokuwa wakifyatua risasi hewani, kuwatawanya.
Wakati huo walimu wengi walikuwa wameshatoka ndani ya ukumbi kwenda kujipanga kandokando mwa barabara ya kwenda Shule ya Msingi Olympio, kwa lengo la kutaka kuendeleza mashambulizi.
Bila kuogopa risasi, wengine wakiwa na mawe mkononi, walilisogelea gari hilo la Polisi lenye namba za usajili T 220 AMV, huku wakiwakebei polisi kuwa nao wana njaa kama walimu na mishahara yao ni midogo, hivyo hawapaswi kuwazuia.
Ilipofika majira ya saa 7:30, polisi walilazimika kumtoa Mukoba na baadhi ya viongozi wa CWT chini ya ulinzi kwa ajili ya kuwapandisha kwenye gari hilo, lakini walimu nao walivyoona hali hiyo, walirusha mawe na jiwe moja lilimpata Mukoba sehemu ya tumbo na kusababisha aanguke kabla ya kusimama tena na kukimbilia ndani ya ‘Defender’ ya polisi.
Baada ya kuingizwa ndani ya gari hilo, polisi walirusha risasi hewani kabla ya dereva kuliondoa kwa kasi ili kuwatawanya walimu hao ambao walikuwa wakiendelea kulirushia mawe gari hilo.
Baada ya gari hilo kuondoka, hasira za walimu hao ziliishia kwenye kuimba nyimbo za kumsifu Mwalimu Nyerere.
Moja ya nyimbo hizo ni pamoja na ule unaotumika kwenye migomo mingi ya wafanyakazi nchini, ambao wao waliongezea vionjo kwa kusema: “Kama siyo juhudi zako Nyerere; Kikwete, Maghembe, Ghasia wangetoka wapi!”
Pia waliimba wimbo unaodai kuwa CCM ni chama cha mafisadi, huku wakikisifia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuonyesha alama ya vidole viwili juu, inayotumiwa na chama hicho kusalimiana.
“CHADEMA, CHADEMA, CHADEMA oyeee! Sasa inatulazimu tufanye mapinduzi kama waliyofanya wenzetu wa Tarime kwa kuing’oa serikali ya CCM madarakani kwani inatukandamiza wanyonge na kukumbatia mafisadi,” walisikika wakisema baadhi ya walimu hao.
Hata baada ya Mukoba kuondolewa katika sehemu hiyo na kuliacha gari lake ambalo lilitolewa upepo na walimu hao, bado walimu hao walifunga barabara kuzuia magari yote yaliyokuwa yakipita eneo hilo huku, magari ya kifahari yakipigiwa kelele kuwa ni ya kifisadi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya walimu hao walisema licha ya kuwepo kwa amri ya mahakama kuzuia mgomo huo leo, wataendesha mgomo baridi, kwa kwenda kwenye shule zao, kujiandikisha kwenye vitabu vya mahudhurio, kisha kurejea majumbani mwao.
“Viongozi wa serikali wanajifanya wajanja, sasa sisi ndio walimu, na sisi ndio tunawafundisha watoto mashuleni, tutawafundisha uongo na mzazi mwenye uwezo ni vyema akampeleka mtoto wake shule binafsi,” alisema Mwalimu Lidyia Mhina.
Ilipofika majira ya saa 8:30 mchana, baada ya hali kuwa shwari, walimu walikusanyika nje ya ukumbi huo na Mwalimu Maulid Ng’umbe aliwatangazia walimu hao kuwa kuanzia sasa, CWT haina viongozi.
Juzi, Jaji William Mandia, wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, aliamuru CWT kusitisha mgomo mara moja, kwa kuwa unaweza kuharibu mfumo wa elimu, hasa wanafunzi wa kidato cha nne, ambao wapo katika mitihani.
Mgomo huo ulitarajiwa kuanza leo baada ya CWT kutoa notisi ya siku 60 ambayo imemalizika jana. Walimu wote nchini wanaidai serikali zaidi ya sh bilioni 16, zikiwa na fedha za malimbikizo ya mishahara, likizo na kupandishwa madaraja.
0 comments:
Post a Comment