Serikali imeionya Taasisi ya HakiElimu kuacha kutumia matangazo yake katika vyombo vya habari, kueneza chuki miongoni mwa watoto na vijana nchini na badala yake ingetumia nafasi iliyonayo katika kuwafundisha utawala bora.
Aidha, imewatahadharisha wote wanaoanzisha taasisi za elimu kwa minajili ya kupata fedha bila kuchangia lolote katika sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na shule zinazotoza wazazi fedha nyingi ambazo hazilingani na mazingira na kiwango cha elimu kinachotolewa.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii katika ofisi za Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Lucy Nkya, alisema HakiElimu pamoja na kuonywa na kusimamishwa hivi karibuni kutokana na utendaji wake, bado imeendelea kutoa matangazo ambayo yanaeneza chuki kwa vijana.
“Hili tangazo tena linalorushwa hata televisheni ya TBC1 la watoto wa sekondari wanazungumzia EPA, wanafanyiwa hesabu na kisha wanaambiwa waseme hizi hela zingefanyia hili na lile, kumbukeni samaki mkunje angali mbichi, huku ni kueneza chuki kwa watoto hawa,” alisema Dk. Nkya.
Alisema taasisi hiyo ya HakiElimu inakosea kutumia matangazo hayo kwa upande mmoja tu wa kukosoa. “Mimi nimesomea saikolojia, huu mtindo wa kukosoa serikali kwa namna hii, kunawajengea vijana wetu chuki, badala ya kuwafundisha utawala bora, sasa watoto wanafikiri serikali yote ni mafisadi,” alisema.
Alisema kutokana na matangazo na vitendo hivyo kwa sasa, hata watoto wa baadhi ya viongozi wamelazimika kuhamishwa katika shule za kawaida na kupelekwa shule nyingine kwa vile wanaitwa watoto wa mafisadi na wenzao.
Aliitaka taasisi ya TEN/MET kufikisha ujumbe kwa HakiElimu kuwa wanayo nafasi nzuri kuelimisha jamii juu ya masuala ya sekta ya elimu na si kueneza chuki pekee, kwani serikali itafika mahala italazimika kutumia meno yake.
“Msiisingizie serikali haina demokrasia pindi itakapotumia meno yake, haitokuwa kibogoyo tena,” alionya. Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, alitaka kufahamu uwezo wa kiutendaji wa mtandao huo wa elimu kwa kuwa haujitangazi, kwani pamoja na yeye kuwa Waziri wa Elimu ndio anausikia.
Kwa upande wake, Mratibu wa TEN/MET, Joseph Kisanji, alikiri kuwa mtandao huo umejificha na kwamba wanajitahidi kwa sasa kuutangaza kwa kutumia mtindo wao bila kuiga HakiElimu.
Alisema awali wakati HakiElimu ilipokabiliwa na serikali, takribani asasi nyingi za elimu ziliwatetea ukiwamo mtandao huo. “Hata hivyo, kuna mipaka yake katika kutumia media (vyombo vya habari) kwani zina nguvu na tuliwaambia wenzetu juu ya hilo ila hatuna maamuzi, kazi yetu ni kushauri,” alisema.
Alisema kama suala la tangazo la EPA limeleta athari hadi kufikia watoto wa viongozi kuhamishwa shule ni jambo hatari, hivyo aliahidi kulifikisha katika Bodi ya Mtandao huo ili walijadili na kulifikisha kwa taasisi hiyo ya HakiElimu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TEN/MET, Antoine Gizenga, alisema watalivalia njuga suala la HakiElimu kwani mtandao wao unaitazama taasisi hiyo kama asasi inayosaidia kuibua yaliyojificha.
Mwaka jana, Ofisi ya Waziri Mkuu ilipiga marufuku machapisho na matangazo yanayotolewa na HakiElimu kupitia vyombo vya habari na kutishia kulichukulia hatua kali za kisheria iwapo itakiuka amri hiyo.
CHANZO: HabariLeo
0 comments:
Post a Comment