Wednesday, 15 October 2008

Maaskofu: Mafisadi wataiangusha CCM
 
2008-10-15 10:43:17 
Na Simon Mhina

Viongozi wa dini nchini wamesema tofauti na wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo mafisadi walikuwa wanawaogopa viongozi, sasa imekuwa kinyume chake kwani viongozi ndio wanawaogopa. 

Kadhalika, viongozi hao walionya kama mafisadi wataendelea kuwa marafiki wa watawala, ni wazi kuwa wananchi watakiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani katika chaguzi zijazo. 

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti kwa lengo la kutoa maoni ya hali ya kisiasa, uchumi na vita dhidi ya rushwa tangu Nyerere afariki dunia miaka tisa iliyopita, viongozi hao walisema kama angekuwepo mafisadi wote nchini wangekuwa rumande. 

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa alisema jinsi viongozi wanavyoasi taratibu miiko ya uongozi ya Mwalimu Nyerere, ndivyo CCM inavyozidi kumomonyoka taratibu, lakini kwa kasi ya ajabu mithili ya barafu lililoanikwa juani. 

Alisema Nyerere alikuwa jasiri kukemea maovu, wizi, rushwa na ufisadi, lakini viongozi wa sasa wanahofu kufanya hivyo. 

Alisema hatua ya CCM kukubali kukumbatia mafisadi inakifanya chama hicho kujitengenezea njia ya kujiangamiza siku za usoni. 

Alisema miiko ya uadilifu na ujasiri wa kupamba na uovu huo, aliokuwa nao Nyerere ndio ulioipa CCM umaarufu na kuaminiwa na Watanzania. 

``Kwa hiyo wakienda kinyume imani hiyo itatoweka mara moja, kwa mfano nataka niwaulize hawa wanaochanganya biashara na siasa. 

Hivi Nyerere yeye alikuwa mbumbumbu kiasi kwamba hakujua faida za kuanzisha kampuni. Hivi Nyerere alikuwa hajui utamu wa kujilimbikizia pesa ndani na nje ya nchi?`` alihoji. 

Akitoa maoni yake kuhusu maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu yaliyofanyika nchini kote jana, Askofu Mkuu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, alisema kinachomtofautisha Mwalimu Nyerere na viongozi wa sasa ni matendo. 

Alisema Nyerere siku zote aliishi sawa sawa na yale aliyokuwa anayahubiri. 

``Nyerere alikuwa sawa kabisa na mwinjilisti anayehubiri injili, mhubiri yeyote lazima matendo yake yawe kielelezo. 

Huwezi kuhubiri kuacha ulevi wakati wewe mwenyewe ni mlevi. Ndio maana unakuta viongozi wetu wanakemea ufisadi kwa mtindo wa rasharasha kwa vile wengi wao wana sehemu katika huo ufisadi,`` alisema. 

Askofu Kakobe alisema hivi sasa ni wazi kwamba tangu Mwalimu afariki, ni vigumu kukemea ufisadi ukiwa ndani ya CCM. 

Alisema njia pekee ya kuifanya CCM iendelee kuwepo sio dola wala propaganda, bali ni viongozi wake kuishi sawa na maisha ya Nyerere, vinginevyo chama hicho kitabomolewa na wananchi. 

``Ndio maana hadi leo Nyerere anaheshimika na thamani yake inaongezeka kila mwaka, ni kwa sababu aliishi sawa sawa na yale anayosema, alipambana na aina zozote za dhuluma na rushwa,`` alisema Kakobe. 

Alipoulizwa mafisadi wataiangusha CCM kwa mtindo upi, Askofu huyo alisema hatua ya CCM kukubali pesa iwe kigezo cha mtu kukubaliwa awe kiongozi, ni njia rahisi watakayoitumia mafisadi kuidondosha. 

``Enzi za Mwalimu pesa hazikuwa kigezo cha kupata uongozi, hivi sasa pesa ndicho kigezo,`` alisema na kuongeza: ``Kwa vile mafisadi wanajua pesa ndicho kigezo cha kupata uongozi, wameshaanza kuchangishana kwa ajili ya 2010. Kibaya zaidi pesa hizo ni hizi hizi walizopora toka kwa masikini.`` 

Alisema kinachoshangaza viongozi wanamuenzi Mwalimu kwa mambo madogo madogo kwa njia za kinafiki, lakini mambo ya msingi wanayaacha. 

Naye Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Methodius Kilaini, alisema hatua ya viongozi kuogopa kuwakamata mafisadi na kuwafungulia mashitaka kwa kigezo kwamba wakishinda kesi watatudai fidia, kinadhihirisha kwamba bado sheria zetu haziko imara. 

Alisema inasikitisha kuona viongozi wanahubiri kumuenzi Mwalimu, ilhali wakubwa wanaokula rushwa na mafisadi wanaachwa wanakula raha. 

``Mwalimu hakumuogopa fisadi wala mla rushwa eti kutokana na utajiri wake, kwa vile wakati huu imekuwa kinyume kwa viongozi wetu ndio maana mafisadi wanatamba,`` alisema. 

Askofu Kilaini alisema wakati rushwa ndogo ndogo zinapungua kutokana na kushughulikiwa kwa haraka na vyombo vya dola, lakini rushwa kubwa zinazowahusisha mafisadi zinazidi kukua kila kukicha, kwa vile hawaguswi. 

Kiongozi huyo alisema kama mbinu alizotumia Mwalimu kupamba na ufisadi zinaonekana zimepitwa na wakati, basi ni vema zikabuni mbinu nyingine na wala sio kukaa kimya. 

``Hivi sasa viongozi wetu hawana ujasiri wa kupamba na rushwa kama wakati wa Mwalimu asingekuwepo fisadi yeyote anayetamba mitaani,`` alisema.

CHANZO:Nipashe


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget