*Wajitoa kusimamia uchaguzi mkuu mwaka 2010 *Waenda shule wajazana ofisini kupiga soga *Serikali yasambaza fomu shuleni zisainiwe
Na Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya kuaminika kuwa mgomo wao uliokuwa uanze jana nchi nzima umeyeyuka, walimu sehemu mbalimbali nzima walifanya mgomo baridi.
Uchunguzi wa gazeti hili kutoka mikoa mbalimbali nchini umeonesha kuwa jana, siku iliyokuwa iwe ya kwanza ya mgomo, walimu wengi hawakufundisha au kuingia madarasani huku wanafunzi wengi wakionekana kuguswa na hali hiyo.
Lakini wakiwa katikati ya huzuni ya kutotimizwa madai yao na kuzuiwa kugoma, baadhi ya walimu sasa wamefikia hatua za mbali zaidi ya kutoigia darasani sasa kuamua pia kuachana na shughuli zozote za kuwasaidia wanasiasa.
Kutoka mjini Tanga, mwandishi wetu Mashaka Mhando anaripoti kuwa baadhi ya walimu wa jijini humo wametangaza kutoshiriki kusimamia wala kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Walimu wengi huajiriwa kwa muda na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi sehemu mbalimbali nchini.
Walimu hao wakizungumza nje ya ofisi za Chama Cha Walimu Tanznia (CWT) mkoani humo, kwa masharti ya kutotajwa majina, walisema hawaoni umuhimu wa kushiriki upigaji kura na kusimamia uchaguzi huo, kwa kile walichodai kuwa viongozi wanaposhinda wanatumia madaraka yao kuwanyanyasa.
“Hivi kweli tutapiga kura ili iweje? Hatutamchagua kiongozi yeyote mwaka 2010 wala kazi ya kuandikisha kura hatuitaki, kama wanataka kieleweke wayakamilishe madai yetu kwanza,” alisema mmoja wa walimu hao anayefundisha shule ya msingi.
Kutoka Dar es Salaam, wanafunzi walikosa masomo katika shule mbalimbali.
Ingawa walimu waliozungumza na gazeti hili walikataa kutamka waziwazi kuwa wanaendesha mgomo baridi, lakini walisema kama kuna mgomo wa aina hiyo, basi hiyo inabaki kuwa ni siri ya mwalimu mmoja mmoja.
Mwalimu Mkuu wa shule moja ya msingi jijini Dar es Salaam aliyezungumza kwa masharti ya jina lake kutochapishwa gazetini, alisema: "Kama kuna mgomo baridi hiyo ni siri ya walimu wenyewe, lakini tumetii amri ya mahakama ndiyo maana unaniona na walimu wangu tupo hapa (ofisini)."
Mwalimu huyo aliliambia gazeti hili kuwa kwa sasa wanasubiri uamuzi mwingine utakaotangazwa na CWT, wakati 'wakiendelea na kazi.'
Katika shule hiyo, walimu wengi walikuwa wamekaa ofisini wakiendelea na mazungumzo.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili katika shule hiyo, walisema walikuwa hawajafundishwa somo lolote hadi gazeti hili lilipofika shuleni wapo kwa kile walichokieleza kwamba walisikia walimu wamegoma kufundisha kwa sababu hawajalipwa mishahara yao.
Katika Shule ya Msingi Tandale hadi ilipofika saa 5:30 asubuhi wanafunzi wa darasa la tano walidai kuwa walikuwa hawajafundishwa somo lolote kinyume na ilivyo kawaida.
Waliopoulizwa kama walifahamu ni kwa nini hawakufundishwa somo lolote hadi muda huo kinyume na ilivyo kawaida, walidai kwamba wamesikia walimu wanadai mishahara yao.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bibi Sarah Mwaseba, alisema wao wanatii tamko la Mahakama na wanaendelea kusikilizia.
Alipoulizwa kama wanaendelea kufundisha kwa ari, alijibu: "Tunaendelea kufundisha na tunaamini kuwa watatupatia haki yetu japo hawajatamka rasmi ni lini watalipwa rasmi."
Katika shule zingine ambazo gazeti hili lilitembelea malalamiko ya wanafunzi kutofundishwa yaliendelea kujitokeza huku wengine wakisema wamefundishwa japo somo moja.
Baadhi ya wanafunzi walieleza kuwa walimu walikuwa wakiingia darasani na kuwapa maswali mawili au matatu.
Katika shule ya msingi Mtoni gazeti hili lilidokezwa kuwa jana asubuhi walimu walikuwa na kikao cha dharura kujadili masuala mbalimbali. Kuwepo kikao hicho kulithibitishwa na mmoja wa walimu (jina tunalihifadhi).
Alidokeza kuwa kuna waraka umekuja kutoka serikalini unaowataka warejee darasani na madai yao yatakuwa yametimizwa ifikapo Novemba au Desemba.
"Walimu hawakubaliani na uamuzi huo hivyo kuna mgomo ambao unaendelea kichinichini ambapo walimu hawatafanya baadhi ya mambo hadi Serikali itakapowalipa madai yao," kilidokeza chanzo chetu.
“Sisi wenyewe tu wakati tunaangalia kwenye luninga tulipandwa na jazba...nasi tungekuwa pale pasingetosha yaani mpaka mwalimu afikie hatua ya kulia kwa ajili ya haki yake. Serikali ijue kwamba tumechoka...kwa nini lakini hivi bila sisi patatoka viongozi kweli hapa nchini?” walisema kwa masikitiko makubwa.
Joyce Kassiki kutoka Dodoma anaripoti kuwa mkoani humo baadhi ya walimu jana wamefika shuleni lakini hawakuingi madarasani ikiwa kama njia mojawapo ya kutimiza azma yao ya kugoma.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, walimu hao walidai kuwa lengo la kugoma lilikuwa ni kuishinikiza Serikali ili iwalipe malimbikizo pamoja na madeni yao.
“Sote kwa pamoja tuliazimia kugoma ifikapo Oktoba 15 mwaka huu, yaani leo (jana), tunashangaa eti mgomo unasitishwa wakati lengo letu halijatimia,” alisema mwalimu mmoja kwa masharti la kutotaka kuandikwa jina lake gazetini.
Mwalimu mwingine naye alisema kuwa walimu hawakuwa na nia ya kugoma, lakini lengo lao kubwa likikuwa ni kupewa pamoja na kulipwa madeni na malimbikizo yao ya mishahara.
“Nashindwa kabisa kuielewa Serikali, yaani huwa haipendi kushughulikia matatizo ya wafanyakazi mpaka wagome au watishie kugoma ndio inaanza kutafuta suluhu.
"Hivi kwa nini huwa haifanyi utaratibu huo mapema wakati inakuwa inaelewa madhara na matatizo ya migomo?,” alihoji mwalimu huyo.
Taarifa zilizokusanywa na mwandishi wetu Masau Bwire kutoka mikoa mbalimbali zinaonesha kuwa walimu wengi jana walifika ofisini, kusaini vitabu vya mahudhurio kisha kukaa tu na kupiga soga.
Walimu waliozungumza kwa njia ya simu walisema hawako tayari kufanya kazi na endapo watalazimishwa kwa vitisho, wataifanya kwa kulipua hadi Serikali itakapowatekelezea madai yao.
Walipoulizwa na gazeti hili sababu za kutoingia darasani wakati wako kazini, walisema hawana ari ya kufanya kazi na walilazimika kwenda kazini kutokana na vitisho vya Serikali kuhusu hatua za kinidhamu dhidi ya walimu ambao wasingefika kazini.
"Tumetishwa sana na Serikali na tumepata taarifa kwamba juzi wakurugenzi wa manisapaa zote walikutana na walimu wakuu wote na kuwaeleza kuwa kila baada ya siku tatu wapeleke kwa Ofisa Elimu wa Manispaa husika majina ya walimu ambao hawatafika kazini ili wachukuliwe hatua.
"Kwa kuwa hatukujua hatua zipi zitakazochukuliwa na Serikali dhidi ya walimu wasiofika kazini, tumeamua tuje kazini tusaini vitabu vyao vya mahudhurio, lakini kamwe hatutaingia madarasani kufundisha," walisisitiza walimu wa Dar es Salaam.
Mkoani Dodoma, tofauti na sehemu nyingine, walimu wa walipitishiwa fomu zilizotolewa na wakurugenzi wa wilaya kwa agizo la Katibu Tawala wa Mkoa huo zikiwataka walimu wajiorodheshe na watie saini kama wanaendelea na mgomo au wanafanya kazi.
"Tumepewa fomu zenye sehemu mbili sehemu ya kwanza inawataka walimu wanaoendelea na mgomo wajiorodheshe na kutia saini na sehemu ya pili inawataka walimu wanaoendelea na kazi pia wajiorodheshe na kusaini, lakini hakuna hata mmoja aliyesaini popote. Tutakuwapo kazini lakini hatutafanya kazi mpaka haki yetu itakapopatikana," walisema walimu hao.
Mkoani Mara, wilayani Musoma Mjini walimu jana walidaiwa kuandamana hadi ofisi za CWT mkoani humo wakiutaka uongozi wa chama hicho utoe msimamo kuhusu mgomo huo uliozuiwa na mahakama.
Habari zilizopatikana kutoka mjini hapo zilisema kuwa viongozi wa mkoa wa CWT baada ya kuona hali si shwari kwa kuzongwa na umati wa walimu walihofu kukutwa na yale yaliyomkuta Rais wao, Bw. Mukoba juzi katika ukumbi wa Diamond Jubilee na kulazimika kuwatuliza walimu hao, kwa kuwaomba warudi kazini hadi saa saba mchana chama kitakapotoa tamko rasmi kuhusu mgomo huo.
Wilayani Tarime walimu asubuhi ya jana walikusanyika katika shule ya Msingi Turwa ambapo kiongozi wa CWT wilayani humo, Bw. Machunde Magabe, alidaiwa kuwataka walimu waende kazini kusaini vitabu vya mahudhurio na kupumzika ofisini, wakisubiri muda wa kazi umalizike ili warudi majumbani kwao.
Mjini Tanga hali katika mkoa huo ilielezwa kuwa mbaya zaidi kwani katika Shule ya Msingi Masiwani, hadi saa nne asubuhi alikuwapo mwalimu mmoja tu.
Mjini Tabora, walimu walidaiwa kukaa makundi makundi katika maeneo ya kazi wakijadili hatma ya madai yao na jinsi Serikali inavyojitahidi kuulaghai umma wa Watanzania katika kushughulika madai yao.
"Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora leo (jana) amekuwa akizungukia kila shule kuwataka walimu waingie madarasani kufundisha lakini haikuwezekana, tumemwambia tutaingia madarasani kufundisha kwa moyo kama tutalipwa haki zetu," alisema mwalimu wa mjini hapo.
Kilimanjaro, kama jijini Dar es Salaam walimu waligawanyika wapo waliogoma kuingia madarasani na pia wapo walioingia madarasani na kufundisha, wakidai kuwa wanatii amri ya Mahakama na agizo la wakurugenzi wao kupitia barua walizozisambaza shuleni zikiwataka waendelee na kazi kwa kuwa madai yao yanashughulikiwa kisheria.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Rais wa CWT, Bw. Mukoba alisema hatua hizo za wanachama zitasaidia Serikali kutambua kuwa mgomo wa walimu halikuwa shinikizo lake bali ni mpango wa wanachama katika kudai haki na maslahi yao.
"Serikali ilidai ninashinikiza mgomo wa walimu ili nipate umaarufu eti kwa lengo la kugombea ubunge mwaka 2010 yaliyotokea jana (juzi) katika ukumbi wa Diamond Jubilee na yanayoendelea kutokea mikoani, yananisaidia kuijulisha Serikali kuwa mgomo wa walimu haukuwa shinikizo langu ila ulikuwa ni mpango na mkakati wa wanachama wote katika kudai haki yao," alisema Bw. Mukoba CHANZO: Majira |
0 comments:
Post a Comment