Wanakijiji Ichonde wakimbia makazi
BAADHI ya wanakijiji cha Ichonde wilayani Kilombero, Morogoro, wamedaiwa kukimbia makazi yao kutokana na mateso ya viongozi wa kijiji hicho .Kwa nyakati tofauti wanakijiji hao walizungumza na Tanzania Daima, wakilalamikia mateso na fedheha wanazofanyiwa na viongozi wao wanapolazimishwa kuchangia elimu.
Haji Kawogo, mkazi wa Ichonde, alisema uongozi wa kijiji hutumia mgambo wa vijiji vingine kuwakamata nyakati za usiku, kuwafunga kamba na kuwaweka kwenye moja ya madarasa ya shule ya msingi kijijini hapo.
Alisema, wanakijiji hao hulazimishwa kuchangia elimu huku viongozi hao wakishindwa kuitisha mikutano ya kijiji na kuwasomea mapato na matumizi kama inavyotakiwa.
“Viongozi wetu wanatudhalilisha hasa sisi wanaume maana usiku umelala na familia yako wanakuvamia tena kwa kuwatumia mgambo wa vijiji vingine.
“…Wanatutoa nje ya nyumba zetu usiku, wanatufunga kamba na kutulazimisha kulala sehemu moja ndani ya darasa la shule ya msingi Ichonde,” alisema Kawogo.
Naye Asha Hassan, alisema kukosekana kwa maendeleo ya Kijiji cha Ichonde, kunasababishwa na uongozi mbovu uliopo hivyo aliiomba halmashauri ya wilaya kuingilia kati, ili kunusuru ubabe wa viongozi hao.
“Kijiji cha Ichonde, tunakosa maendeleo kwa sababu ya viongozi wetu, hawatushirikishi katika bajeti ya kijiji wanachojua ni kukusanya michango, lakini hawatuelezi kiasi kilichopatikana wala matumizi yake,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho Deogratias Makinda, akana tuhuma hizo na kueleza kwamba hana taarifa za kukamatwa, kufungwa kamba wala kulazwa katika shule ya msingi.
“Mimi sina dola ya kuwakamata wanakijiji, sina taarifa za wao kuteswa ndiyo kwanza nasikia hapa,” alisema mwenyekiti huyo.
Aidha, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ichonde, Salum Sadala, alikiri kwamba wapo wanakijiji wanaokamatwa na kupelekwa katika shule hiyo kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji wa maendeleo ya kijiji.
0 comments:
Post a Comment