Thursday, 30 October 2008


*Yataka sheria ziachwe zifuate mkondo wake
*Yasubiri uamuzi kuhusu sakata la ufisadi
*Yaguswa na usanii wa kampuni ya Richmond
*Yaahidi Rais Obama au McCain kuja nchini

Na Hassan Abbas


BALOZI wa Marekani nchini, Bw. Mark Green amekuwa mwanadiplomasia wa kwanza nchini kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuhusu nini anachopaswa kukifanya saa chache kabla hajaamua hatima ya waliokwapua mabilioni kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). 

Balozi Green aliyesisitiza kuwa mafisadi si watu wa kuachwa hata kama ni vigogo na kutaka sheria zichukue mkondo wake, ameifafanulia Majira jinsi alivyoguswa baada ya kuona kampuni ya kimarekani ya Richmond ilivyohusika katika utata kwenye sekta ya umeme nchini. 

Balozi Green alisema hayo jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu uchaguzi wa Marekani, mtikisiko wa uchumi, hali ya kisiasa nchini na mtazamo wake kuhusu wagombea, maseneta Barack Obama na John McCain. 

EPA na Richmond 

Balozi Green alisema hawezi kujinasibu kuwa Marekani ni Taifa la mfano katika kupambana na rushwa, lakini alisisitiza kuwa katika miaka 232 ya Uhuru wa Taifa hilo, ujenzi wa jamii yenye kuwajibika kwa kufuata utawala wa sheria usiomwogopa mtu ndio msingi. 

"Rais Kikwete anafanya kazi kubwa ya kujenga Taifa. Lakini vita dhidi ya ufisadi inahitaji kutowaacha watu wakatamba. Sheria ichukue mkondo wake hata kama mtu ni mashuhuri kiasi gani. 

"Sisi Marekani tumekuwa na azma ya wazi kuwa kiongozi wa umma akiiba fedha za watu, anachunguzwa na kuchukuliwa hatua. Wamarekani ni wakarimu sana kutoa fedha zao kusaidia watu, lakini ni wakali sana wanapoona inafanyiwa ufisadi. Rais Kikwete akitumia sheria atafanikiwa," alisema Balozi Green na kusisitiza kuwa katika sakata la EPA, waliopoka fedha hizo wanapaswa kuwajibishwa. 

Akifafanua kuhusu hilo, Balozi Green alisema Rais Kikwete alitaja mikakati mizuri alipozungumza bungeni kuhusu namna atakavyowashughulikia mafisadi wa EPA. 

"Rais alitaja mikakati mizuri. Tunasubiri kuona atakavyoitekeleza," alisema. Akizungumza bungeni Agosti 21 mwaka huu, Rais Kikwete aliwapa mafisadi hao hadi Oktoba 30 (jana) wawe wamerejesha fedha hizo, vinginevyo ifikapo Novemba mosi (kesho) wawe wameburutwa kortini. 

Sakata la Richmond, kampuni iliyoshinda zabuni ya kufua umeme wa mamilioni nchini ikijieleza kuwa ilitokea Marekani, ni moja ya matukio yaliyoitikisa Serikali ya Rais Kikwete mwanzoni tu mwa utawala wake. 

Akilizungumzia sakata hilo, Balozi Green alisema Serikali ya Tanzania katika kupambana na rushwa inapaswa kufuata sheria bila kujali mhusika au kampuni husika imetoka nchi gani. 

"Suala la Richmond najua ilikuja ikafanya kazi kupitia kampuni iliyosajiliwa nchini. Lakini bila kujali kampuni hiyo ilitoka wapi, Serikali inapaswa kuchukua sheria haraka inapoona kuna ufisadi," alisema huku akikiri kuwa ukweli kwamba kampuni hiyo ilijieleza kutoka Marekani, ulimsumbua wakati wa sakata hilo, ingawa ubalozi wake hauwajibiki moja kwa moja katika mikataba inayohusu kampuni binafsi. 

Uchaguzi wa Marekani 

Balozi Green alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu wa nchi hiyo umekuwa na hamasa kubwa hasa kutokana na ushiriki wa Seneta Obama, Mmarekani mwenmye asili ya Afrika wa kwanza kuteuliwa na chama kikuu kuwania urais. 

"Ni kweli kwamba ushiriki wa Seneta Obama umeibua hamasa miongoni mwa Wamarekani wengi, hilo ni suala lisilo na ubishi. Lakini pia hata uteuzi wa Seneta McCain naye umeibua ushawishi katika baadhi ya nchi. 

"Wakati huku Afrika Obama anaonekana kuwa na ushawishi, McCain naye ni kivutio hasa katika nchi za Mashariki ya Mbali ambako kutokana na historia yake ya kushiriki vita ya Vietnamu na kwa miaka mingi aliyokaa kwenye Kamati ya Mambo ya Nje kwenye Bunge la Seneti, alishiriki masuala mengi yanayohusu eneo hilo," alisema Balozi Green ambaye ni mfuasi wa Republican. 

Alisema, akiwatathmini wagombea hao wawili, anaona kuwa wote kwa sera zao, wana uwezo wa kuisaidia Marekani iwapo mmojawapo ataingia Ikulu. 

"Ukiangalia sera zao, hakuna shaka kwamba wote (McCain na Obama) wana mikakati ya dhati kuisaidia Marekani na historia zao zinaonesha wana uwezo mkubwa," aliongeza. 

Akizungumzia somo ambalo nchi za Afrika zinaweza kujifunza kutokana na kampeni zinazoendelea sasa nchini Marekani, Balozi Green alisema kubwa ni umuhimu wa watu kujadiliana masuala ya kitaifa kwa uwazi na mwishowe kila mwananchi akawa na fursa ya kupiga kura na kumchagua kiongozi anayemtaka. 

"Siwezi kusema kuwa Marekani ina demokrasia ya kuigwa, sote bado tunajifunza kutoka kwa kila mmoja. Lakini kama ilivyoonekana, mijadala ya wazi ni kitu muhimu ili kujadili masuala ya kitaifa na mwishowe kuheshimu uhuru wa kupiga kura. Naamini mkiimarisha hili, Afrika na Tanzania zitafanikiwa," aliongeza. 

Msukusuko wa uchumi na Afrika 

Balozi Green alikiri kuwa uchumi wa Marekani umetikisika, lakini akazitoa wasiwasi nchi za Afrika hususani Tanzania, kuwa kiwango cha misaada ya Marekani hakitaathirika kutokana na hali hiyo. 

"Kwa mfano, miradi ambayo tumekubali kuisaidia Tanzania ilishapitishwa na fungu lake lipo, kwa hiyo haitaathirika, sioni sababu ya Watanzania kuwa na wasiwasi," alisisitiza. 

Pia alisema hofu ya miradi mingi iliyoanzishwa chini ya utawala wa chama cha Republican nayo kubatilishwa, iwapo kitaingia madarakani chama cha Democrat haina msingi, kwani wakati wa upitishaji wa miradi hiyo Wamarekani hukubaliana kwa pamoja bila kujali itikadi ya vyama. 

"Kwa bahati nzuri nilikuwa kwenye Baraza la Wawakilishi, ni mmoja wa wawakilishi waliopigania kupitishwa kwa sheria iliyounda shirika la Millenium Challenge Account, linalotoa misaada mbalimbali kwa Afrika ikiwamo Tanzania. 

"Bahati nzuri wakati wa kujadili masuala haya, wabunge walikuwa wamoja bila kujali itikadi. Kwa hiyo hakuna atakayeweza kuzuia miradi hii, iliamuliwa kwa sauti ya Wamarekani wote," alisema.

Obama au McCain kuja Tanzania 

Akizungumzia ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Marekani, Balozi Green aliisifu kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa zamani wa Marekani, Bw. Bill Clinton, ambaye ujio wake nchini na kazi za taasisi zake, ziliwafanya Wamarekani wengi kuijua au kuwa na nia ya kuijua Tanzania. 

"Hata ujio wa Bush, watu wanaweza kunipongeza kwa kufanikisha kuja kwake, lakini historia nzuri iliyowekwa na Clinton ndiyo iliyowazindua Wamarekani wengi kisha akaja Bush na baadaye mkutano wa Sullivan, lakini pia wadhifa wa Rais Kikwete kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, vimeifanya Tanzania kujulikana zaidi. 

Akizungumzia uwezekano wa ofisi yake kuhakikisha Rais ajaye wa Marekani anafuata nyayo hizo kwa kufika nchini, Balozi Green alisema: 

"Nitafurahi kuona siku moja Rais ajaye wa Marekani awe Seneta McCain au Seneta Obama anaitembelea Tanzania, kuimarisha uhusiano mzuri uliopo. Niko tayari kushughulikia hilo ili afike hapa. 

"Bahati nzuri Seneta McCain nimeshawahi kukutana naye wakati nikiwa kwenye Baraza la Wawakilishi, Obama hatujaweza kukutana kwa sababu wakati huo nikiwa kwenye siasa, yeye alikuwa bado yuko chini, lakini naamini wote watakuwa tayari kuja kuiona nchi hii nzuri," aliahidi. 

Balozi Green kitaaluma ni mwanasheria aliyepata kujaribu kuwania ugavana wa jimbo la Wisconsin kupitia chama cha Republican mwaka juzi akapoteza.

Chanzo:Majira

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget