Thursday, 30 October 2008

Picha kwa Hisani ya HAKINGOWI

Katika jamii zetu, wazee wana heshima ya pekee kama kisima cha hekima, kielelezo cha uadilifu na taa ya maisha. Wazee wana nafasi ya kipekee ya kujenga jamii; wanawakilisha kile kilicho bora; na kilichokomaa. Wazee ni dawa; lakini, wazee wanakuwa dawa ya matatizo pale tu wanapotenda mambo yanayoshabihiana na sifa za wazee.

Wazee wanapogeuka kuwa viranja wa vitendo vya aibu; wanapovaa migolole ya wavurugaji wa amani na vitendo vinavyoashiria kudharau mamlaka ya utawala wa sheria; wanapofikia ukomo wa matumizi ya busara na hekima na wanapojiingiza katika daraja la wapenda shari, wanaanza kupoteza baadhi ya sifa muhimu zinazokamilisha heshima ya mtu kuitwa mzee.

Jana asubuhi, kwa takribani saa mbili, watu waliojitambulisha kama wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walihamia kwenye Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, eneo la makutano ya barabara hiyo na Umoja wa Mataifa Dar es Salaam na kufanya viroja eti wakishinikiza kulipwa mafao yao.

Kitendo hicho sio tu kwamba kiliwabughudhi watumiaji wa barabara hiyo ambao walishindwa kuingia au kutoka mjini, bali kilisababisha hasara kubwa kutokana na kukwama kwa shughuli za biashara katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Kitendo kilichofanywa na watu hao, ambamo pia vijana walikuwamo, ni cha aibu.

Watu hao, walioonekana dhahiri kuwa na jazba kutokana na kile walichodai kutolipwa fedha zao, wameshawahi kufanya vituko vya aina hii kabla ya jana. Lakini kwa kuamua kufunga barabara, huku baadhi ya wanawake wakivua nguo, walionyesha mwisho wa ustaarabu wa mwanadamu katika kudai kile anachodhani ni haki yao.

Hekima na kumbukumbu zilielekea kuwahama wazee hao, walipodai kwamba walikuwa na nia ya kwenda ubalozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam 'kuishtaki' Serikali. Tunawashangaa watu wanaoamua kufikisha matatizo yao kwenye balozi za nchi za nje badala ya kutumia vyombo vilivyoanzishwa kushughulikia matatizo ya wananchi.

Lakini tunawashangaa zaidi wazee hao, ambao wengi wao walishuhudia kushushwa kwa bendera ya Mwingereza nchini tarehe 9 Desemba, 1961.
Kisha tunajiuliza: Tangu lini ubalozi wa nchi ya nje ukawa chombo cha rufaa kwa Watanzania?

Hivi anayeamua kulala barabarani, kuwasilisha matatizo kwenye nchi ya nje, kuvua nguo na kubakia na sidiria hadharani na kulumbana na vyombo vya kikatiba vya dola atakuwa na hekima gani ya kuweza kukemea watoto watakaokosa uelewa wa uraia na maadili mema? Je, uchuro wa kukaa uchi ndio urithi ambao wazee wanawakabidhi watoto wao?

Kwa heshima zote ambazo tunazo kwa wazee wa Tanzania na wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunadhani wazee waliolala barabarani jana wamepotoka. Tunakubali kwamba wazee na wastaafu wanaoidai Serikali wana haki ya kufanya hivyo. Pengine maandamano ya jana yalifanywa kwa lengo la kuitikisa serikali ambayo tayari nayo ina majibu yake.

Lakini suluhisho la tatizo hili lilishafikiwa na hapakuwa na sababu za mgogoro huu ambao umedumu kwa miaka 30, kuondoka katika ustaarabu wa majadiliano yaliyokubalika. Huu ni wakati mwafaka kukumbushana ukweli kuhusu tatizo la malipo ya baadhi ya wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Serikali kwa muda wote imekuwa ikizingatia makubaliano ya awali, yakiwamo mapendekezo ya kamati ya mwaka 1997.

Historia ndefu ya mgogoro huo pamoja na kufikishana mahakamani kudai mapunjo yaliyotokea kwa kesi namba 95 ya mwaka 2003, iliyowezesha kuwapo kwa hati ya makubaliano ya Septemba 25, 2005 iliyokaziwa hukumu na Jaji Oriyo, inatufanya tuamini kwamba ipo haja ya mambo mengi kuwekwa bayana ili kila Mtanzania na kila mhusika aelewe.

La msingi ambalo tunaliona katika makubaliano hayo ni serikali kukubali kulipa wadai hao 31,831 jumla ya shilingi bilioni 117 kwa misingi ya staili ya kila mmoja kulingana na taarifa zao. Taarifa zilizopo ni kuwa jumla ya shilingi bilioni 114.2 zimelipwa kwa wastaafu hao hadi kufikia Agosti 5 mwaka huu na utaratibu wa malipo unaendelea.

Tunaunga mkono kauli ya serikali kama ilivyosema katika taarifa yake, haiwezi kuendelea kulipa fedha bila kuhakiki. Shinikizo linaloletwa na wazee la kulipwa wote bila kufanyika uhakiki ni sawa na kupoteza dira ya uendeshaji wa hesabu za Serikali. Hili halikubaliki. Fedha za Serikali lazima zitolewe kwa uangalifu.

Nchi haiwezi kuendeshwa kwa kukiuka sheria, lakini pia serikali inayomwaga fedha bila kuhakiki ina tatizo kubwa, kwa maana haifuati sheria ila mkumbo, na hii ni hatari. Kama hati ya makubaliano ilikuwa na fomula ya malipo, inakuwaje sasa wastaafu hao wanashinikiza kulipwa mafao kwa kukokotoa mafao yao kwa fomula yao ambayo haiko mahakamani?

Tunarudia. Kitendo walichofanya wastaafu hao ambao tunawaheshimu kutokana na umri wao ni uchuro usiokubalika, kwani wametumia mbinu za kihuni zinazotofautiana sana na umri wao. Matendo ya wazee yanaangaliwa na wengi, lakini kwa maandamano ya jana na vitendo vyao pale, kunabaki swali nani atawakemea watoto wa Tanzania watakapokuwa wanafanya vitendo kama vya wazee wao?

Je, nani atafidia hasara iliyopatikana kutokana na muda ambao watu walizuiwa kufanya shughuli zao za kiuchumi? Katika fikira za kawaida kama nia ilikuwa kuzuia viongozi ambao ndio watumiaji maarufu wa barabara hiyo wasipite, kwa nini wazee hao wasiwafuate wahusika ofisini kwao ili wengine waendelee na shughuli zao?

Bado tunaamini kuwa mahakama zetu hazijapoteza dira, hivyo ni vyema kwanza wastaafu hao wangeendelea kudai haki zao huko kama walivyofanya kufikia mwafaka wa malipo wa sasa. Haitakuwa ajabu kama kitendo cha wazee kitatekwa na ushabiki wa kisiasa. Wanasiasa wachovu watadandia hoja ya maandamano ya jana ya wazee.

Lakini huu sio wakati wa ushabiki, bali bi wakati wa kusimamia misingi ya maadili na utamaduni wa taifa. Hakuna ushabiki wowote utakaohalalisha vitendo vya wazee ambavyo ndani yake kuna mbegu za kujidhalilisha. Tunawapenda, tunawaheshimu na kuwaenzi wazee wetu. Ndio maana tunasononeka tunapowashuhudia wakifanya mambo ambayo yanamomonyoa maadili ya kitaifa na utamaduni wa Mtanzania.

NASHAWISHIKA KUAMINI KUWA MZAZI WA MWANDISHI WA TAHARIRI HII SI MIONGONI MWA WAZEE HAO WANAODAI HAKI ZAO.KUWAAMBIA BABU NA BABA ZETU "WAACHE UTOTO" SIO LUGHA YA BUSARA.KWA BAHATI NZURI,MWANDISHI WA TAHARIRI HIYO,KAMA ILIVYO KWA WATUMISHI WA EX-EAC, NAE KUNA SIKU ATASTAAFU,NA KWA VILE SUALA LA MAFAO KWA WASTAAFU LIMEKUWA KAMA ZAWADI BADALA YA HAKI (HENCE KULAZIMISHA WASTAAFU KUTUMIA NJIA ZINAZOISHIA KUITWA "UTOTO") HUENDA HUO UTAKUWA WAKATI MZURI KWAKE KUELEWA KWANINI WAZEE WETU WALIFANYA HUO ANAOITA "UTOTO".

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget