WAKATI serikali ikishutumiwa na viongozi wa madhehebu ya Kikristo, juu ya Tanzania kutaka kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC) na kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amekutana kwa siri na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kujadili masuala hayo.Kikao hicho cha faragha cha viongozi hao wawili, kilichukua zaidi ya saa moja katika mazungmzo yao yaliyofanyika jana katika ofisi za Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa 11:30.Membe alikutana na Pengo jana ikiwa ni siku moja baada ya kardinali huyo kurejea nchi akitokea Vatican ambako alikwenda kwa shughuli za kanisa.Akizungumza na Tanzania Daima, baada ya kumalizika kwa kikao hicho nyeti, Waziri Membe alikiri kuwa na kikao cha faragha na kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki nchini, lakini hakuwa tayari kusema nini walichojadiliana, kwa madai kuwa, hayapaswi kuwekwa hadharani kwa sasa.“Unajua Kardinali Pengo ni kiongozi wa kiroho wa ngazi ya juu sana, kila tunapokuwa na masuala mazito ya kitaifa, tunapenda kupata ushauri wake pamoja na viongozi wengine wa kiroho ili kuona wanasemaje,” alisema Waziri Membe.“Mbali na suala la OIC na Mahakama ya Kadhi, tumezungumza mambo mengi ya kitaifa ambayo mimi sipaswi kueleza zaidi kwa undani, kwani unaweza kumuuliza Baba Kardinali mwenyewe kama atataka kukueleza, lakini ni mambo ambayo yanahusiana na maisha ya Watanzania wote,” alisema Waziri Membe.Kuhusu mjadala unaoendelea juu ya Tanzania kujiunga na OIC na jinsi hali ilivyo kwa sasa nchini, Waziri Membe alisema ni mambo ya kupita na utulivu utarejea hivi karibuni.“Hali ya amani na utulivu itarudi hivi karibuni, hakuna shida, serikali ina amini na inawahakikishia wananchi kuwa hakuna vurugu kuhusiana na hilo wala suala lingine lolote.“Watu watulie, wafanye kazi, serikali itakutana na wadau wote na nasema tena, hakuna tatizo kubwa hapa, tutahakikisha suala hili linaisha kwa amani bila kusababisha vurugu zozote,” aliongeza Membe.Akizungumzia madai yaliyotolewa na Jumuiya ya Maaskofu wa CCT, kumtaka ajiuzulu hivi karibuni, alisema kuwa hilo hataki kuliongelea kwani amechoka, aachwe apumzike kwanza.Jitihada za kumtafuta Kardinali Pengo, kuzungumzia juu ya kikao hicho cha siri ziligonga mwamba baada ya kuambiwa kuwa, ameingia kwenye kikao kingine na uongozi wa Kanisa la Mt. Joseph na haijulikani kingeisha saa ngapi.Mwishoni mwa wiki iliyopita maaskofu wanaounda Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), walielezea kusikitishwa, kushtushwa na kupinga ushawishi unaojengwa na serikali wa kutaka Tanzania iridhie kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Askofu Peter Kitula ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alisema hawatakuwa tayari kukubalia kwa vyovyote vile kuona chama fulani cha siasa kikijaribu kutafuta ridhaa ya wapiga kura kwa gharama ya kutishia umoja wa kitaifa na amani ya nchi.“Hapa ieleweke kuwa ni hatari na kamwe isiruhusiwe njia hii kutumika ili mradi chama fulani kishike dola hata kama ni kwa gharama ya kuvunjika kwa umoja wa kitaifa na amani ya nchi hii! Jambo hili hatutalikubali kwa vyovyote vile kwa chama chochote kitakachokubali mambo haya mawili aidha wakati wa kampeni za uchaguzi au wakati wowote ule,” lilisema tamko hilo la CCT lililoambatanishwa na majina ya maaskofu 64 wa nchi nzima.Pasipo kufafafanua huku wakisema kwamba CCT, haifungamani na chama chochote cha siasa, maaskofu hao katika tamko lao walisema, iwapo itafikia hatua ya Tanzania kujiunga na OIC na Mahakama ya Kadhi kuridhiwa, basi wao watalazimika kufikiria upya jinsi ya kukishauri chama hicho tawala kwa kuzingatia kile walichokieleza kuwa ni manufaa ya Watanzania.“Kipekee wakati huu, kutokana na yanayoendelea kujadiliwa bungeni, tunatoa tahadhari kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kutoruhusu kabisa kuendelea kwa mjadala huu kama ambavyo tumekuwa tukiomba mara kwa mara kwa nyakati tofauti zilizopita,” linasema tamko hilo.Pamoja na hilo, maaskofu hao walimtaka Waziri Membe, kujiuzulu wadhifa wake kutokana na hatua yake ya kujenga ushawishi wenye mwelekeo wa kidini wa kuiingiza nchi katika OIC.Mbali ya hayo, tamko lilisema kuwa hatua ya Tanzania kujiunga OIC inakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 19 (2) na Sheria ya Vyama vya Siasa nchini.Askofu Kitula alisema, wanapinga Tanzania kujiunga na OIC kwa maelezo kuwa, katiba ya jumuiya hiyo imejipambanua wazi kuwa na malengo ya kuendelea na kuulinda Uislamu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa, lenye watu wa imani nyingine za dini.Akifafanua askofu huyo alisema, katika Ibara ya 1 (11) ya Katiba ya OIC, kuna kipengele kinachosomeka ‘kusambaza, kuendeleza na kuhifadhi mafundisho ya dini ya Kiislamu….kuendeleza utamaduni wa Kiislamu na kuulinda urithi wake’, maelezo ambayo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ambayo inahimiza uhiari na uhuru wa mtu binafsi katika masuala yanayohusu kueneza dini au masuala ya imani.Askofu Kitula ambaye alisoma tamko hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCT, Akofu Donald Mtetemela, aliyesaini tamko hilo, alisema uamuzi wa kujiingiza katika masuala ya namna hiyo ni wa hatari, kwani yanaweza kuleta migogoro kutokana na kuwapo kwa dhana ya udini.Maaskofu hao walimtaka Waziri Membe kuachana na kauli zake juu ya umuhimu wa kuingia kwenye jumuiya hiyo ya Kiislamu na kuhoji aliyemtuma kufanya hivyo.
Thursday, 30 October 2008
Picha kwa hisani ya BONGOPICHA
CHANZO:Tanzania Daima
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment