Thursday, 23 October 2008


Soma kwa makini stori hizi kisha make your own conclusion

STORI YA KWANZA:
Waziri Membe akana kuubeba msalaba OIC
Na Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernad Membe, amekuja juu akisema baadhi ya watu wamekuwa wakimtwisha mzigo kwamba, ameingiza Tanzania katika Jumuiya ya nchi za Kiislam Duniani (OIC), kitu ambacho si kweli.

Kauli hiyo ya Membe ni ya kwanza kuitoa hadharani tangu kuibuka kwa kasi kwa mjadala huo, ambao unaonekana kuigawa nchi katika misingi ya kiitikadi.

Akizungumzia hilo jijini Dar es Salaam jana, Membe alisema si kweli kwamba Tanzania imekwishajiunga na OIC na wala yeye hajasema lazima ijiunge.

Membe akifafanua huku akionekana kuguswa na tuhuma hizo dhidi yake kutokana na kutamka hilo bunge katika hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema uamuzi wa kujiunga au la, uko kwa wananchi.

"Nimekuwa kimya, kuachia na kusikiliza watu waseme, jamani, Tanzania haijajiunga na OIC wala sijasema lazima ijiunge," alisema na kuongeza:

"Uamuzi wa kujiunga au kutojiunga utakuwa chini ya wananchi, wasomi, NGOs na ninyi waandishi wa habari, ndiyo mtakaoamua."

Membe alikuwa akifafanua kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Iran, ambao unaonekana na baadhi ya watu kama wenye nia ya kuingiza nchi OIC.

Akifafanua zaidi, alisema watu wasiingize vitu visivyokuwa na msingi kwa ajili ya kutunga na kuzungumzia hisia, na kushauri wasome historia kufahamu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Membe huku akionekana kuchukizwa na fikra mbovu za kupandikiza udini katika nchi, alisema Watanzania ni watu wanaoheshimika duniani kwa umakini wao, ni aibu na haipendezi kujadili udini.

Alisema kama ni kujiunga na OIC ni jambo la kuamua, kwani Uganda ambako kuna Waislam asilimia 10 imeweza kujiunga huku Wakristo wakiwa ni asilimia 66 na wengine wapagani.

"Sasa jamani, msitake kunichinganisha na watu wangu, nawaambieni tena na tena, Tanzania haijajiunga na OIC na haitaweza kujiunga uamuzi huo ni ridhaa ya wananchi," alisisitiza.
CHANZO: Mwananchi

STORI YA PILI KUHUSU SUALA HILOHILO:
Waziri: Tanzania kujiunga OIC ni dhahiri
23 Oct 2008
By Muhibu Said

Tanzania inatarajia kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) wakati wowote katika siku zijazo baada ya serikali kuweka bayana azma hiyo jana.

Azma hiyo ya serikali iliwekwa bayana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi, alipozungumza na Nipashe jana, ikiwa ni wiki chache tangu Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe, aliambie Bunge kwamba, hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na jumuiya hiyo.


Balozi Iddi alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC, unatarajiwa kuanza wakati wowote na kwamba, hatua ya mwanzo ya mchakato huo, viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano watakutana na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa ajili ya kupata msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.

Naibu Waziri huyo alisema hayo alipoulizwa na Nipashe kama mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC umeshaanza au la tangu Waziri Membe atoe kauli hiyo bungeni, mjini Dodoma, Agosti 22, mwaka huu.

``Bado hatujaanza mchakato. Kuna kikao tunachotaka kwanza kufanya kwa ajili ya kushauriana na wenzetu wa Zanzibar ili tuwe na msimamo mmoja kuhusu hilo. Ilikuwa tuanze sasa, lakini Mheshimiwa Waziri (Membe) hayupo na Bunge linatarajiwa kuanza,`` alisema Balozi Iddi.

Alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC ni mrefu, ambao unatarajiwa pia kulishirikisha Baraza la Mawaziri kufikia maamuzi.

Balozi Iddi alisema hatua nyingine ya mchakato, ambayo serikali inatarajia kuichukua, ni kutoa elimu kwa umma ili kuwaondoa uoga wote walioonyesha hofu iwapo Tanzania itajiunga na jumuiya hiyo.

``Hao wanaopinga, ni waoga tu, hawajaeleweshwa kwani haina maana Tanzania itakuwa nchi ya Kiislamu. Zipo nchi kama vile Uganda zimejiunga na OIC, lakini hazijabadilika kuwa nchi za Kiislamu. Tutawaelewesha wakati ukifika, tunavyo vyombo vya kuelimisha hilo,`` alisema Balozi Iddi.

Agosti 22, mwaka huu Waziri Membe wakati akifunga mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na IOC.

Waziri Membe alisema serikali mwaka huu, ilifanya kikao na Baraza la Wawakilishi kuhusu suala hilo na kugundua kuwa nchi 21 zimejiunga na jumuiya hiyo.

Alisema kati ya nchi hizo, zimo pia nchi za Wakristo ambazo zimejiunga na hazijapata madhara yoyote.
``Tumeshakusanya takwimu za nje na kuona hakuna madhara yoyote ya kujiunga na IOC, bora tu kufuata taratibu,`` alisisitiza Waziri Membe.

Alisema suala hilo lilileta utata awali kwa sababu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, marehemu Ahmed Hassan Diria, alipeleka ombi la Zanzibar kujiunga kwenye jumuiya hiyo bila kuishirikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, alisema suala hilo limefanyiwa kazi na serikali na kuona kuwa hakuna madhara kujiunga na IOC.

Siku chache baada ya Waziri Membe kutoa kauli hiyo bungeni, viongozi wa makanisa na baadhi ya wasomi, akiwamo Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Dk. Methodius Kilaini, walipinga vikali kauli hiyo ya serikali.

Wengine waliopinga suala hilo, ni Askofu Stefano Msangi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT Tanzania, Dk. Alex Malasusa, Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi.

Hata hivyo, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mnyamani, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mohammed Iddi, amekuwa akijitokeza kuwapinga maaskofu kuhusu kauli zao za kupinga suala hilo.
CHANZO:Nipashe

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget