Na Mwandishi Maalum, Tabora
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ametetea mila ya chagulaga kuwa haisababishi wasichana wengi kupata mimba kabla ya wakati, huku akionya dhidi ya vitendo vya viongozi kugeuza mila za watu kuwa adui, na kuziua kwa kisingizio cha kutatua matatizo.
Chagulaga ni kati ya mila za wenyeji wa mkoa wa Tabora ambayo huhusisha wasichana kujipanga ili kuwapa nafasi wavulana kuwaendea na kuchagua wachumba, lakini mamlaka za mjini hapa zimeichukulia kama moja ya njia zinazoongeza idadi ya wanafunzi wa kike kupata mimba wilayani Uyui.
“Haya ndiyo maisha ya watu hawa miaka yote" alisema Rais Kikwete wakati akipokea taarifa ya utendaji wa serikali wilayani Uyui iliyoonyesha kuwa wanafunzi wengi hupata mimba kabla ya wakati wao na hivyo kujikuta wakipoteza nafasi ya kuendelea mbele kimasomo.
"Tusije kugeuza mila za watu kuwa adui na tukaanza kuua mila hizo kwa kisingizio cha kujaribu kutafuta majawabu ya baadhi ya matatizo yanayotukabili,” Rais aliwaambia viongozi wa wilaya hiyo juzi asubuhi ikiwa ni siku ya tano ya ziara yake mkoani Tabora.
“Haya ndio maisha yao ya miaka yote? Hapa mjini watoto wa kike wa shule wanapata mimba na wala hakuna Chagulaga. Tusije tukageuza mila kuwa ndiyo adui. Inawezekana kuwa mila hiyo inawezesha tatizo hilo, lakini ngoma zimekuwepo miaka na miaka, na tatizo la mimba siyo la miaka mingi kiasi hicho.
“Sote hapa tumecheza ngoma, tena usiku. Ni ngoma tu za kawaida za makabila yetu. Na wale wanaowapa mimba watoto wa shule pengine hata kwenye ngoma hawaji. Inawezekana kabisa kuwa watu wanaowapa mimba watoto hawa ni mizee ambayo hata kwenye ngoma haendi. Na je si kweli kuwa sisi sote tumecheza dansi na disko, na si tulirudi nyumbani salama.”
Rais alisema kuwa ni kweli kwamba tatizo lipo “laakini tulichambue zaidi ili kupata kiini chake cha msingi. Tusije tukaua mila za watu kwa visingizio tu. Hata kwetu kule tunayo mila ya kuchengula, na wala haina madhara ya kimaendeleo”.
Rais Kikwete, ambaye anatokea mkoa wa Pwani unaosifika kwa ngoma za sherehe, alisisitiza kuwa kwa jadi ya Waafrika kupata mimba nje ya ndoa ni aibu kubwa kwa familia yoyote na kwamba suala hilo halihusiani na mila yoyote.
"Na wala msije kukimbilia kupiga marufuku ngoma za watu, kwa sababu inawezekana kabisa ukasimamisha ngoma, lakini mimba zikaendelea. Kule Chunya (mkoa wa Mbeya) kuna mimba nyingi sana za watoto wa shule kuliko hata hapa, lakini hakuna Chagulaga,” alisema Rais Kikwete.
Awali, mkuu wa wilaya hiyo, Doreen Semali Kisamo alimwambia Rais Kikwete kuwa mila hiyo ya Chagulaga ni moja ya sababu ya mimba nyingi kwa watoto wa kike katika shule za sekondari wilayani humo.
Lakini alikuwa ameelezwa na viongozi wa wilaya hiyo awali kuwa moja ya sababu za kuwa na idadi kubwa ya wasichana wanaopata mimba ni mila za wakazi wa eneo hilo, hasa vijijini, ikiwamo ile ya Chagulaga.
Akiwa Tabora, Rais Kikwete alisimamisha kwa muda ziara yake Jumapili na kwenda Afrika Kusini kufungua kikao cha 10 cha Bunge la Afrika. Rais alirejea Dar es Salaam Jumatatu jioni na kurudi Tabora juzi asubuhi kuendelea na ziara yake.
Katika miaka miwili iliyopita, kiasi cha wanafunzi 44 wa kike wilayani humo walipata mimba.
Pia Rais Kikwete alishtushwa na ongezeko kubwa la watu wilayani humo na kutaka wahusika wa programu ya uzazi wa mpango, maarufu kama "Nyota ya Kijani" kuitupia macho wilaya hiyo.
Rais alielezwa kuwa ongezeko la watu katika wilaya hiyo kwa njia ya kuzaliana ni wastani wa asilimia 4.8 ikiwa ni kiwango cha juu sana ukilinganisha na cha taifa ambacho ni asilimia 2.8.
“Hizi ni takwimu si za kawaida. Ongezeko la asilimia 4.8 pengine ni kubwa kuliko katika eneo lolote nchini kwa sababu wastani wa taifa ni asilimia 2.8. Hii ni mara mbili ya wastani wa taifa,” alisema Kikwete.
Baada ya maelekezo hayo ya Rais, mzee mmoja kwenye mkutano huo alimweleza Rais Kikwete kuwa wakazi wa Uyui wanazaana sana kwa sababu “tunakula sana, na tunazaana sana, mkuu".
Lakini rais akasema: “Hili siyo jambo jema sana. It is striking (linastua). Wastani wa taifa ni asilimia 2.8. Nyota ya kijani lazima iangaze huku.”
Rais pia alionekana kushtushwa na idadi ya mauaji katika wilaya hiyo baada ya kutaarifiwa kuwa watu 34 wameauwa katika miezi sita iliyopita.
“Kwa nini mauaji ni mengi mno kiasi hiki? Watu 34 katika miezi sita ni wengi sana katika wilaya moja. Wilaya nyingine zinakaa mwaka mzima bila hata kuuawa mtu yoyote.”
Jana asubuhi, Rais Kikwete alitembelea kijiji cha Kigwa ambako aliweka jiwe la msingi kwenye soko jipya la kijiji/mji hicho katika shughuli iliyohudhuriwa na mamia ya watu.
Akijibu maombi ya baadhi ya viongozi wa kijiji hicho kumtaka atoe maagizo ili kijiji hicho kiwe na hadhi ya kata, Rais Kikwete alisema:
“Kazi yangu si kugawa kata, na wala kata haigawanywi katikati ya kipindi cha uchaguzi. Kwa sababu tukigawa kata katikati ya kipindi cha uchaguzi ni lazima tufanye uchaguzi mpya wa madiwani. Hata hivyo, kugawa kata siyo tatizo, ili mradi tu mfuate taratibu za ugawaji kata.”
Katika kijiji cha mfano cha Milenia cha Mbola, tarafa ya Ilolangula, Rais alikagua miradi inayofanyika chini ya dhana hiyo mpya ya kuendeleza vijiji na kuzungumza na wananchi.
Rais aliwaambia mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji hicho kuwa wakazi wa kijiji Milenia wanaokataa kuchangia magunia mawili ya mahindi kwa ajili ya chakula cha watoto wa shule wa kijiji hicho, wasipewe mbolea ya bure mpaka wametimiza masharti hayo.
“Nasikia baadhi yetu hamjachangia magunia mawili ya mahindi kutokana na mazao yenu kama yanavyosema masharti ya uzalishaji katika kijiji hiki. Sasa wale wanaokataa kuchangia kama ilivyokubaliwa, wanyimwe mbolea ya bure kuanzia sasa,” alisema.
Moja ya masharti ya misaada ya Milenia kwa kijiji hicho ni wakulima kupewa mbolea ya bure. Mradi huo unafadhiliwa na wafadhili mbali mbali.
Rais pia aliwaambia wakazi wa kijiji hicho kuthamini elimu kwa watoto wao. “Halitakuwa jambo linalowezekana kuwarithisha watoto wenu fimbo za kuchungia ng’ombe. Bila elimu watoto wenu watapata taabu sana katika miaka ijayo,” alisema.
Kijiji cha Ilolangula ndiko alikozaliwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment