Serikali imeombwa kuwekeza zaidi katika taasisi mbalimbali zinazofanya tafiti za magonjwa pamoja na kuboresha vifaa vya maabara zinavyowasaidia kupata majibu ya utafiti wafanyao.
Hayo yalisemwa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk. Salim Abdulla wakati wa uzinduzi wa taasisi hiyo ambayo zamani ilikuwa ni kituo cha utafiti wa malaria, Ifakara, mkoani Morogoro.
Dk. Abdulla alisema taasisi hiyo inatafiti magonjwa mbalimbali lakini inakabiliwa na changamoto ikiwamo uhaba wa fedha ambao unakwamisha baadhi ya utafiti ambao unalenga kutokomeza magonjwa kama malaria, kifua kikuu na vifo vya watoto wachanga.
Alisema ili utafiti uweze kufanikiwa lazima usaidiwe kifedha na kuwezeshwa kuwa na vifaa vya kisasa vya maabara.Alisema taasisi hiyo hivi sasa inatarajia kufanya utafiti kwa magonjwa ya kisukari, kuongezeka uzito na presha, magonjwa aliyosema yanaonekana kuongezeka zaidi na hayapewi kipaumbele huku yakipoteza zaidi maisha ya watu.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Leonard Mboera, alisema serikali itaendelea kuisaidia taasisi hiyo kufanya utafiti wa magonjwa mbalimbali ya binadamu na kuibua mbinu za kupunguza magonjwa na vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga.
CHANZO: Habarileo
0 comments:
Post a Comment